Na Mwandishi Wetu, Njombe
Wajasiriamali washonaji wa vikapu wa vijiji vya Ikando na Ibumila Halmashauri ya wilaya ya Njombe mkoa wa Njombe wameiomba serikali kuwatafutia soko la uhakika la kuuzia bidhaa zao sambamba na halmashauri kuwatambua katika mikopo ya wanawake.
Wakizungumza na Mtanzania Digital washonaji hao wamesema wanakabiliwa na changamoto ya kukosa soko la uhakika na hivyo kulazimika kuuza bila ya faida licha ya nguvu kubwa wanayotumia katika utengenezaji.
‘’Tunatumia nguvu kubwa katika utengenezaji soko la uhakika hakuna,lakini pia tunachangamoto ya mitaji.tuiombe halmashauri yetu itutembelee na sisi ili tukuze biashara yetu,’’alisema Maria Mhema
Maria alisema kuwa wanashona vikapu ili kujikwamua kiuchumi lakini soko limeua likisua sua hali inayowalazimu kuuza kwa hasara ili wapate fedha za mahitaji kwa ajili ya kusaidia familia.
‘’Malighafi kama nyasi ambazo zinaota kando ya mito kipindi hiki cha kiangazi zimekua zikisumbua kupatikana hivyo tunafata mbali kidogo na hapa sasa ukiangalia namana ya uandaaji ikiwemo rangi hadi kikamilike kwa kweli tunapata hasara ila tunafanya tu kwa sababu tumezoea,’’alisema.
Naye, Furaha Kilasi aliiomba serikali kuwatambua ili kuwasaidi kutafuta soko la nje kwa sababu la ndani halijabadilisha maisha yao.
“Nina watoto wanne nimewapeleka shule kwa sababu ya ushonaji wa vikapu lakini hii haitoshi,watoto hawa wanatakiwa kula,kuvaa na mimi mwenyewe niwe na kitu kingine cha kufanya ili tu nijikomboe kimaisha’’alisema Furaha.
Kwa upande wa Sayuni Kaduma alisema soko la vikapu sio rafiki kwa sababu bei zake ziko tofauti.
“Bei ziko tofauti soko sio zuri unakuta mteja anakuagiza bidhaa ukimpelekea anaanza kujishushia bei yeye mwenyewe au anakwambia havina ubora wakati huo sapo ulishamtumia pamoja na bei zake”alisema Sayuni.