Na Denis Sinkonde, Songwe
Waumini wa Dini ya Kiisilami nchini wametakiwa kuitumia Sikukuu ya Eid kuyaendeleza mema waliyoyafanya katika kipindi cha mwezi mtukufiu wa ramadhani sambamba na kuhamasisha kuendeleza amani iliyopo nchini.
Wito huo umetolewa leo Mei 3, 2022 na Mkuu wa wilaya ya Ileje mkoani Songwe, Anna Gidarya Katika msikiti wa wilaya uliopo Itumba mjini huku akisema kipindi cha mfungo uwe mwendelezo wa kuyaishi maisha ya kuhamasisha upendo amani na mshikamano na kukemea maovu yanayotokea kwenye jamii.
“Kutokana na jamii kutumia muda mwingi kwenye shughuli za kidunia bila kutafuta elimu ya dini ndio chanzo cha kuongezeka maovu kwenye jamii,” amesema Gidarya.
Amesema siku ya Eid El FITR ni siku ya kumtukuza mwemyezi Mungu na si siku ya kufanya maovu kama inavyokaliliwa na watu kufanya maovu ambayo yanahatarisha amani kwenye jamii.
Sambamba na hayo Gidarya amewakumbusha waumini wa Kiisilamu kuendelea kukumbushana zoezi la kitaifa linalotatajiwa kufanyika Agosti 23, 2022 ambalo ni sensa ambayo hufanyika nchini kila baada ya miaka 10.
Shekhe wa wilaya ya Ileje Khamis Simbeye amewataka waumini wa dini ya kiisilami na jamii kwa ujumla kuendelea kutenda matendo mema ikiwemo kuishi kwa upendo na kuwasaidia watu wenye mahitaji mbalimbali ikiwepo wagonjwa, yatima, wajane na wasiojiweza.
Baadhi ya waisilamu ambao wamehudhuria Katika msikiti huo wamewaomba viongozi wa dini nchini kuendelea kushikamana kwa pamoja ili kuhakikisha elimu ya kidini inaifikia jamii ili kuepukana na matukio ya ukatili ambayo yanaongezeka kila siku.