28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wahitimu Kairuki watakiwa kutafuta tiba ya Ukimwi

Na TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM


KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya, amewataka wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU) kutatua changamoto za afya zinazoikabili jamii ikiwamo kutafuta tiba ya ugonjwa wa Ukimwi.

Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la kwanza la wahitimu wa chuo hicho juzi, Ulisubisya, alisema jamii imezungukwa na changamoto nyingi zinazowasubiri wahitimu hao kuzitatua.

Alisema hakuna kinachoshindikana na kinachotakiwa ni kujituma na kujitoa kwao katika kupambana na changamoto hizo.

“Hakuna kinachoshindikana duniani bali kujituma na inawezekana changamoto nyingine zinawasubiri wahitimu wa chuo hiki kutatuliwa ikiwa ni pamoja na utafiti wa tiba ya Ukimwi,” alisema.

Ulisubisya Alisema watumishi hao wa sekta ya afya hawatakiwi kukaa ofisini bali kujitoa na kusikiliza matatizo yanayoikabili jamii.

“Ninasisitiza kuwa taasisi hii lazima iendelee na itafanikiwa iwapo tu waliohitimu hapa watarudisha nguvu kazi kwa taasisi hii na kutoa huduma bora za afya,” alisema.

Pia alisema ameagiza kuongeza majengo yatakayowezesha kuongeza udahili wa wanafunzi katika chuo hicho.

“Elimu inayotolewa katika chuo hiki imekuwa bora na msaada mkubwa wa kutengeneza rasilimali watu wanaolisaidia taifa, hivyo chuo kinatakiwa kuongeza udahili kwa kuongeza majengo,” alisema.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa HKMU upande wa Taaluma, Profesa Moshi Ntabaye, alisema wamefanikiwa kutoa wataalamu 1,889 tangu kuanzishwa kwake na 40 tu ndio walitoka nje ya nchi.

“Haya ni mafanikio makubwa kwa kuwa tumechangia wataalamu wa afya kwa nchi yetu zaidi ya 1,800 na mwaka huu tuna wahitimu 230,” alisema Profesa Ntabaye.

Wataalamu 230 wa afya katika fani mbalimbali wamehitimu HKMU na kutunukiwa shahada na vyeti na Mkuu wa chuo hicho, Balozi Salim Ahmed Salim, huku idadi ya waliosoma masomo ya shahada ya udaktari wa binadamu ni 153.

Katika hatua nyingine, Makamu Mkuu wa HKMU, Profesa Charles Mgone, alisema kati ya wahitimu hao, 126 ni wanawake na wanaume ni 104.

Alisema wahitimu hao wamesoma kuanzia ngazi ya astashahada, stashahada, shahada na shahada za uzamili.

“Wahitimu tulionao wa shahada za uzamili wako 13, shahada ya udaktari wa binadamu 153, shahada ya uuguzi 32, stashahada ya uuguzi 21 na astashahada ya uuguzi 11,” alisema.

Pia alisema katika shahada za uzamili wahitimu wa fani ya udaktari wa magonjwa na afya za watoto wako watano, magonjwa ya wanawake wako watatu, ustawi wa jamii wako watatu na sayansi ya afya ya jamii wako wawili.

Alisema katika mwaka huu wa masomo wamedahili wanafunzi wapya 293.

“Shahada ya uzamili ya magonjwa na afya za watoto tumedahili wanafunzi saba, shahada ya udaktari wa binadamu wanafunzi 146, shahada ya uuguzi 48 na stashahada ya uuguzi wanafunzi 92,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles