24.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wahitimu elimu ya juu wahimizwa kujiajiri

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Serikali imesema haiwezi kuajiri wahitimu wote wa vyuo vya kati na vyuo vikuu kwenye sekta ya umma bali inachofanya ni kuwahamasisha kutafuta fursa katika sekta binafsi au kujiajiri.

Akizungumza wakati wa mahafali ya 37 ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji NIT, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amesema malalamiko ya ukosefu wa ajira yamekuwa mengi huku Serikali ikinyooshewa kidole dhana aliyodai kuwa ni mbaya kwani wako walioajiriwa sekta binafsi na wana masilahi na maisha mazuri.

“Serikali haiwezi kutoa ajira kwa watu wote wanaomaliza, tuna vyuo vingapi, wanafunzi wangapi kila mwaka wanahitimu.

“Sisemi kwamba hamtapata ajira Serikalini lakini lazima mjiandae kwa yote ikitokea hujapata unaendelea kusubiri jiulize nini ambacho unaweza kufanya,” amesema Waitara.

Wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) wakiwa kwenye mahafali yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho.

Aidha amewataka wahitimu hao kutoridhika na elimu waliyoipata na kwamba ambao wana nafasi ya kujiendeleza waendelee na wale ambao hawana fursa wajiajiri au kuajiriwa.

“Mtaani maisha si rahisi sana lazima ujipange, wewe una cheti wenzako wana ‘degree’ kwenye kozi hiyo hiyo, ‘masters’ na mwingine ana PHD ungekuwa wewe ndiyo mwajiri ungemchukua yupi…lazima mtafakari hilo,” amesema.

Waitara pia amekipongeza chuo hicho kwani ni kati ya taasisi 23 zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ambayo inafanya vizuri.

Naye Mkuu wa chuo hicho Profesa Zacharia Mganilwa, amesema kina program 25 za ngazi ya stashahada, 15 za shahada ya kwanza, 9 za stashahada za uzamili na shahada ya uzamili.

“Chuo kinazalisha wataalamu watakaoweza kudumu kwenye mashirika ya uchukuzi na usafirishaji na kuendelea kukuza pato la taifa,” amesema Profesa Mganilwa.

Amesema pia idadi ya wanafunzi imeongezeka kwa asilimia 67 kutoka wanafunzi 7,752 mwaka 2016/17 hadi kufikia wanafunzi 12,980 mwaka 2021/22 huku kikiwa na wafanyakazi 346 na kati yao wanataaluma ni 224.

Aidha amesema chuo kimeendelea kuwajengea uwezo wanataaluma wake ambapo mpaka sasa watumishi 65 wanajiendeleza kimasomo ndani na nje ya nchi na kati yao 30 wanachukua shahada ya uzamivu, 30 shahada ya uzamili na watano shahada ya kwanza.

“Tupo kwenye mchakato wa kukipandisha hadhi chuo, nchini hapa hatuna chuo kikuu cha usafirishaji na hata Afrika ni vichache,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la chuo hicho, Profesa Bavo Nyichomba, amewaasa wahitimu kutumia maarifa waliyoyapata kwa kujiajiri au kuajiriwa na kutafuta fursa hadi nje ya nchi.

Katika mahafali wahitimu 1,880 kati yao wanawake wakiwa ni 727 walitunukiwa astashahada, stashahada, stashahada ya uzamili, shahada na shahada ya uzamili katika fani tofauti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles