27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wahitimu DIT watakiwa kuchangamkia mikopo ya Halmashauri

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

Mkuu wa Wilaya (DC) Ilemela, Hassan Masala amewataka wahitimu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Kampasi ya Mwanza kuchangamkia mikopo inayotolewa na Halmashauri yake ili kupata mitaji ya kufanya kwa vitendo kile walichojifunza darasani.

Aidha, hii ni mara ya kwanza kwa DIT kutoa wahitimu wa Stashahada ya Utengenezaji Bidhaa za Ngozi ambapo leo wanafunzi watano wamehitimu kozi hiyo.

Akizungumza katika mahafali ya tatu ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza, Masala ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, alisema serikali ya awamu ya sita imelenga kuendeleza na kuanzisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kuleta mageuzi na kuongeza thamani kwenye mazao ya kimkakati ikiwa ni pamoja na zao la ngozi na bidhaa zake.

“Serikali imelenga pia kufufua viwanda ambavyo kwa sasa havina ufanisi. Kwa kufanya hivyo itasaidia kutengeneza ajira kwa wahitimu wa vyuo vyetu na wakati huo huo kuimarisha uchumi wetu,” amesema.

Amesema pia kuwa serikali inalenga kupiga vita umasikini kwa kuweka mazingira mazuri kwa wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu, ikiwemo DIT ili waweze kujiajiri, jambo linalowezekana endapo wahitimu watakuwa na moyo wa uthubutu wa kuanzisha biashara, kampuni au viwanda kwa kutumia elimu na ujuzi walioupata vyuoni.

“Kwa vile Taasisi hii inatoa wataalam wazuri na wenye uwezo mkubwa, serikali ingependa kuona wahitimu wa DIT Kampasi ya Mwanza wanatoa mchango mkubwa katika kupiga vita umaskini na katika juhudi ya kufikia azma ya Tanzania ya viwanda,” amesisitiza.

Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Prof Preksedis Ndomba amesema ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira, DIT imekuwa ikiendesha mafunzo yake kiubunifu zaidi ikiwa ni mafunzo ya darasani, atamizi za teknolojia (incubator) na mafunzo ya vitendo viwandani.

Amesema mafunzo ya kitaalam yanaendelea kuimarishwa kwa kuendesha mitaala inayokidhi mahitaji ya soko na kuongeza bajeti ya vifaa vya kufundishia na kujifunza ili kuwashirikisha wanafunzi katika kutatua changamoto za kisayanasi na ufundi zinazoikabili DIT na jamii kwa ujumla.

“Uanzishwaji wa atamizi una lengo la kuwawezesha wahitimu kuingiza bunifu zao sokoni ili wajiajiri na kuanzisha viwanda vidogo vidogo.

“Katika mpango wa mafunzo kwa vitendo DIT imekua ikishirikiana taasisi nyingine na viwanda vya ndani na nje ya nchi, pamoja  na Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) ili kukuza ujuzi wa wanafunzi,” amesema Prof Ndomba.

Mwenyejiti wa Baraza la DIT, Dk. Mhandisi Richard Masika, amesema Baraza linasimamia vyema utekelezaji wa tamko la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa wakati akizungumza na vijana mkoani Mwanza mapema Juni mwaka huu, la kuifanya Kampasi kuwa kituo cha umahiri cha teknolojia ya ngozi na teknolojia zinazoshabihiana katika kanda ya Afrika Mashariki na kati.

Aidha, amesema Baraza limetoa maelekezo kwa Menejimenti ya DIT mpaka kufikia mwaka 2023 iwe imefikia kwenye viwango vya juu vya teknolojia ambapo amepewa taarifa kuwa agizo hilo limeanza kutekelezwa.

Katika mahafali hayo wanafunzi 32 wamehitimu ambapo 27 wamehitimu stashahada ya Sayansi na Teknolojia ya Maabara na wengine watano wamehitimu Stashahada ya utengenezaji bidhaa za ngozi. Pia wanafunzi wengine 160 wamehitimu kozi fupi ya utengenezaji simu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles