Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Mkurugenzi wa Kampuni ya Wahenga Aluminium, John Ryoba amejitolea kujenga vyoo vya walimu katika Shule ya Sekondari Kisungu iliyopo Kata ya Kinyerezi Wilaya ya Ilala ili kuwaboreshea mazingira ya kufanyia kazi.
Shule hiyo iliyoanzishwa Machi 30, 2007 kwa sasa ina wanafunzi 961 lakini haina vyoo vya walimu hali inayosababisha kuchangia vyoo na wanafunzi.
Akizungumza wakati wa mahafali ya 12 ya wanafunzi wa kidato cha nne, Ryoba amesema ameguswa kujenga vyoo hivyo ili kuwaboreshea walimu mazingira ya kufanyia kazi.
“Walimu 44 wanafundisha watoto 900 hawana sehemu ya kujisaidia ni jambo la fedheha sana, naamini wazazi wengi wana vipato vya kawaida lakini lazima tujibane kwa kushirikiana na Serikali tuboreshe mazingira ya shule,” amesema Ryoba.
Aidha ameahidi kutengeneza uwanja wa michezo shuleni hapo pamoja na kuwapatia vifaa vya michezo.
Mkurugenzi huyo amesema pia atagharamia masomo kwa wanafunzi watakaopata daraja la kwanza sambamba na kutoa nafasi kwa wahitimu wawili kufanya kazi katika kampuni yake wakati wakisubiri matokeo.
“Hakuna mtu atakayeandika ukurasa wa maisha yako isipokuwa wewe mwenyewe, elimu itawasaidia kupambana na changamoto ambazo mtakabiliana nazo hivyo, lazima msome kwa bidii ili mpate kazi nzuri au muendeshe biashara au kukuza vipaji vyenu muwe mashujaa,” amesema.
Naye Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Arnold Tenganamba, amesema ina vyumba 16 na kati ya hivyo 10 ni vibovu na vinavyotumika ni sita huku kimoja kikigeuzwa kuwa ofisi ya utawala.
Hata hivyo amesema tayari wamepokea Sh milioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa na kwamba watabaki na upungufu wa madarasa matano.
“Tumekuwa tukifanya jitihada za kufundisha licha ya kuwa na changamoto na ufaulu umekuwa ukipanda mwaka hadi mwaka. Mwaka 2016 ufaulu ulikuwa asilimia 54, 2017 asilimia 36, 2018 asilimia 64, 2019 asilimia 60 na 2020 asilimia 65,” amesema Mwalimu Tenganamba.
Amesema pia wana upungufu wa walimu wa sayansi, hawana jengo la utawala na mashine ya kudurufu maandishi ni mbovu.
Kwa upande wao wahitimu wamesema msingi bora waliopata toka kwa walimu wao umewajenga kitaaluma na elimu ya makuzi ambayo imewasaidia kujitambua na kwamba watafanya vema katika mitihani yao.
Katika mahafali hayo pia wazazi na walezi walikula keki na wahitimu na kuchangia zaidi ya Sh 200,000 kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za shule hiyo.