Mohamed Hamad, Kiteto
Jeshi la Polisi Wilayani Kiteto, mkoani Manyara, linawashikilia watu 10 wanaodaiwa kuwa wahamiaji haramu kutoka nchini Ethiopia na Somalia, na Wanzania watatu wakiwa na tunguri saba ili ziwasaidie kuvuka nchini kuelekea Afrika Kusini.
Akizungumza na Mtanzania Digital, leo Jumanne Novemba 27, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Agostini Senga, amesema, watuhumiwa hao walikamatwa Septemba 25, mwaka huu asubuhi katika Kijiji cha Njia Panda ya Kiteto kuelekea Afrika Kusini.
Kamanda Senga amesema Watanzania watatu waliokamatwa ni pamoja na madereva wawili na mganga wa kienyeji mmoja aliyekuwa akiwaongoza njia na tunguri zao.
“Kwa mujibu wa mganga huyo ambaye jina limehifadhiwa, alisema lengo la kuwa na tunguri hizo ni wasikamatwe na kutiwa nguvuni na hatimaye wavuke kuelekea nchini Afrika Kusini,” amesema.
Amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote ili sheria ifuate mkondo wake kwani upelelezi umeshakamilika
“Ni kosa kisheria kusafirisha au kusaidia kusafirisha wahamiaji haramu, ikithibitika faini ni Sh milioni 20 na kutaifishwa chombo hicho cha usafiri,” amesema.