27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wagonjwa 1,500 wapatiwa matibabu MOI

Na VERONICA ROMWALD

 – DAR ES SALAAM

TAASISI ya Mifupa Muhimbili (MOI) imejivunia mafanikio ya upasuaji zaidi ya wagonjwa 1,500 ambao wangehitaji kwenda nje ya nchi kufuata matibabu mbalimbali.

Matibabu hayo ni yale ya upandikizaji wa nyonga bandia, goti bandia, upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu, upasuaji mkubwa wa mgongo na  upasuaji mkubwa wa ubongo.

Mwingine ni upasuaji mkubwa wa kurekebisha mfupa wa kiuno, upasuaji wa mifupa (watu wazima na watoto), upasuaji wa kuzibua njia za maji kichwani kwa matundu kwa watoto (ETV).

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dar Salaam jana, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa taasisi hiyo, Dk Samuel Swai alisema kwa hatua hiyo wameokoa zaidi ya Sh bilioni 10.

Pamoja na hayo, alisema wameanzisha wodi mpya ya kisasa ya kulaza wagonjwa na kuwafanyia upasuaji siku wanayopelekwa hosipitali na kuruhusiwa kurudi nyumbani (Same day surgery).

“Tunapoanza mwaka 2019 tunataka kwenda na mpango mkakati ujulikanao kama tiba kwa wakati, lengo la mkakati huu ni kuhakikisha kila mgonjwa anayefika MOI anapata huduma bora na kwa wakati.

“Kutekeleza adhma hii tumeanzisha wodi mpya na ya kisasa ya kulaza wagonjwa na kuwafanyia upasuaji siku hiyo hiyo na kuruhusiwa kurudi nyumbani (Same day surgery) ambayo tayari imeanza kazi na kuonyesha matunda chanya,” alisema.

Aidha Dk Swai alisema walengwa wa wodi hii ni wagonjwa wenye maumivu ya goti na bega wanaohitahi upasuaji kwa njia ya matundu (Shoulder and Knee Athroscopy).

“Wengine ni wagonjwa wenye vivimbe vidogo vidogo sehemu mbalimbali za mwili  na wengine ambao watabainishwa na madaktari,” alisema.

Alisema wagonjwa hawa hawahitaji kukaa muda mrefu wodini kusubiri upasuaji.

“Mpango huu umekuja kutokana na ongezeko la vyumba vya upasuaji kutoka sita hadi tisa pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba na vitendanishi hivyo kufanya idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji kuongezeka maradufu,” alisema Dk Swai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles