25 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

11 wagunduliwa saratani ya shingo ya kizazi

Na KHAMIS SHARIF

– ZANZIBAR

WANAWAKE 11 kati ya 3013 waliopimwa saratani ya shingo ya kizazi awamu ya kwanza wamegundulika kuwa na maradhi hayo na wengine 48 wameonyesha kuwa na dalili za ugonjwa huo.

Hatua za kuwapatia matibabu zimeanza mapema mwezi uliopita baada ya kuanza kukamilika kwa upimaji wa saratani hiyo.

Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed alieleza hayo jana katika hafla ya kuwaaga na kuwapongeza madaktari kutoka Jimbo la Jiangsu nchini  China baada ya kukamilisha awamu ya kwanza ya mradi wa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi.

Mradi huo ulianza Desember 3 na kumalizika 25 katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar.

Mohamed alisema katika awamu ya kwanza ya uchunguzi wa maradhi hayo, wizara ilipanga kuwafanyia uchunguzi wanawake 3,000 lakini kutokana na mwamko mkubwa wa wananchi kupenda kujua afya zao idadi hiyo iliongezeka na kufikia 3013.

“Hatukufikiria kwamba wanawake wangejitokeza kwa idadi kubwa kama hii kufanyiwa uchunguzi, lakini kila siku idadi yao iliongezeka.

“Niwatake akinamama wa Zanzibar kujitayarisha kwa uchunguzi wa awamu ya pili ya mradi huo mwakani ambapo tumepanga kuwafanyia uchunguzi wanawake 10,000 katika Hospitali mbalimbali za Unguja na Pemba”.alisema Waziri huyo.

Aidha aliongeza kuwa wajibu wa kwanza wa Wizara ya Afya ni kukinga na baadaye kutibu, hivyo uamuzi wa kufanya uchunguzi wa afya na kujua tatizo mapema ni rahisi kulipatia ufumbuzi kuliko kuliacha na baadaye likasababisha madhara makubwa.

Jimbo la Jiangsu nchini China limekuwa likitoa misaada mbalimbali hususan sekta ya afya kwa Zanzibar tangu mwaka 1964 na sasa wameanzisha hatua nyingine ya kufanya uchungzi wa maradhi yanayowasumbua wananchi.

Katika hatua hiyo, Waziri Mohamed aliiomba Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuongeza wataalamu na vifaa tiba katika awamu ya pili ya mradi huo ambao utawahusu watu wengi zaidi.

Kwa upande wake, Balozi wa mradi wa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, Mgeni Hassan Juma alisema Serikali inataka kuona uchunguzi wa maradhi hayo unakuwa jambo la kawaida kwa kila mwanamke.

Alisema Serikali inajiandaa kuwapa mafunzo madaktari wazalendo na kuongeza vifaa tiba ili kila hospitali iweze kufanya uchunguzi baada ya kumalizika kwa mradi huo wa miaka mine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles