Na CLARA MATIMO-MWANZA
WAGONJWA 11 wasiojiweza wamepatiwa huduma ya upasuaji baada ya taasisi ya kimataifa ya Lions Club kuwalipia gharama zinazofikia Sh milioni mbili.
Taasisi hiyo yenye makao yake nchini Marekani inayojishughulisha kusaidia watu wasiojiweza, imewezesha upasuaji huo kwenye Hospitali ya Bukumbi iliyopo Wilaya ya Misungwi kupitia tawi lake la mkoani Mwanza.
Akizungumza hospitalini hapo alipokwenda kuwaona wagonjwa hao mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, aliiomba taasisi hiyo kuendelea kushirikiana na Serikali ili kupunguza changamoto zilizopo katika jamii.
“Lions Club imekuwa ikifadhili mambo mengi katika jamii yetu kwa ajili ya kusaidia changamoto ambazo inakabiliana nazo, niwaombe muendelee kuwa na moyo huo, mmekuwa wadau wakubwa sana kwa maendeleo ya taifa, mnajitoa sana, naamini na taasisi zingine zitafuata nyayo zenu,” alisema Mongela.
Rais wa Lions Club Tanzania, Bakari Omar alisema wanavutiwa na jinsi ambavyo hospitali hiyo inavyothamini kwa kutunza misaada wanayoitoa na jinsi inavyowafikia walengwa maana walijenga wodi zaidi ya miaka 30 iliyopita, lakini hadi leo bado inahudumia wagonjwa.
Kwa upande wake, Rais wa Lions Club Tawi la Mwanza, Mahesh Choudhary, alisema wanayapa kipaumbele magonjwa ya upasuaji kwa sababu ni hatarishi kwani mgonjwa asipofanyiwa upasuaji kwa wakati athari zake ni kubwa anaweza kupoteza maisha.
“Unapokuwa na uvimbe sehemu yoyote ya mwili ni hatarishi kwa sababu usipopata matibabu ya upasuaji haraka athari zake ni kubwa ndiyo maana klabu yetu tukaona tujikite sana kwenye eneo hilo ila tunatoa msaada wa elimu na mahitaji mengine,” alisema Choudhary.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Bukumbi, Dk. Suzan Charles, alisema wagonjwa hao 11 wamefanyiwa upasuaji mbalimbali ikiwemo kina mama kutolewa uvimbe kwenye kizazi, tezi dume, macho, koo na meno na wote wanaendelea vizuri.
Baadhi ya wanufaika akiwemo Mariana Gervas na Perepetua Simon, walisema wamesumbuliwa na maumivu muda mrefu, lakini walishindwa kumudu gharama za matibabu kwa sababu wana vipato vya chini.