NA MWANDISHI WETU
IDADI ya makada wanaotajwa kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa inaweza kufikia 30, baada ya wengine wengi kutarajia kujitokeza kuanzia wiki ijayo, MTANZANIA Jumamosi limedokezwa.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka katika vyanzo mbalimbali vya habari ndani na nje ya CCM zinadai kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka na pengine hata kufikia wagombea 35, kutokana na baadhi ya makada waliohudhuria vikao vya juu vya chama hicho vilivyofanyika wiki iliyopita mjini Dodoma kuonyesha nia ya kuingia katika kinyang’anyiro hicho baada ya kipenga kupulizwa.
Mtoa taarifa mmoja ambaye pia anaongoza kitengo nyeti ndani ya CCM (hatutamtaja jina ili kulinda kibarua chake), alilidokeza gazeti hili kuwa hadi sasa kuna makada 25 ambao wameonyesha nia, miongoni mwao wakiwa ni wale waliokwisha kujitangaza kuwania nafasi hiyo kubwa nchini.
“Tutegemee idadi kuongezeka zaidi baada ya kipenga kupulizwa, wapo waliokuwa na nia muda mrefu na walibaki na siri ya kusubiri kipenga, wapo walioshindwa kujizuia kutokana na shauku ya kutaka nafasi hiyo, ndiyo maana wengine walionyesha nia ya wazi na wengine walijitangaza,” alisema.
Kati ya makada hao 30 wanaotajwa kujitosa kuwania urais, 25 tayari walionyesha nia kwa muda mrefu na wengine kujitangaza kwa nyakati tofauti.
Miongoni mwao ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta.
Wengine ni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe.
Pia yupo Balozi Amina Said Alli, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashari, Makongoro Nyerere, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
Wengine ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, Jaji Mstaafu Agustino Ramadhan, Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emanuel Nchimbi, Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala, Shamsi Vuai Nahodha, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Waziri wa Katiba na Sheria, Asha Rose Migiro.
Pia wamo Makamo wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Billal, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Balozi Mstaafu Agustine Mahiga, Mkurugenzi wa zamani wa Usalama wa Taifa, Dk. Hassy Kitine na Profesa Sospeter Muhongo.
MTANZANIA Jumamosi limebaini kuwa kinyang’anyiro cha mwaka huu cha kuwania urais kupitia CCM kimeweka historia mpya, kwa kuwa na idadi kubwa ya makada walioonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo.
Baadhi ya makada wakongwe waliozungumza na gazeti hili walidai kuwa kinyang’anyiro cha mwaka 1995 ndicho kilikuwa kinashikilia historia ya makada wengi kujitokeza, lakini historia hiyo inaweza kuvunjwa katika uchaguzi huu utakaofanyika mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili, Kada mkongwe wa chama hicho, Khamis Chifupa, alisema katika kinyang’anyiro cha mwaka huo makada takribani 17 walijitokeza kugombea urais kupitia CCM.
Kwamba hali ya ushindani katika kinyang’anyiro cha kumpata mgombea urais wa mwaka 2005 hakikufua dafu kwa sababu waliojitokeza kugombea urais hawakuzidi 15.
Duru zaidi zinadai kuwa, kinyang’anyiro cha mwaka huu cha kumpata mgombea urais kupitia CCM kimeonekana kuwavutia zaidi vijana, ambao nao wamediriki kujitosa katika mbio hizo na hivyo kufanya idadi kuwa kubwa zaidi.
Tofauti na chaguzi zilizopita, ambako ilikuwa ni nadra kuona sura za vijana, mwaka huu vijana kama January Makamba, Mwigulu Nchemba na Dk. Hamis Kigwangala ni miongoni mwa waliojitokeza wazi kutangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM.
Katika muktadha huo, siku chache baada ya chama hicho kupuliza kipenga cha kufungua mbio za kuwania urais, tayari baadhi ya makada wamejitokeza kuweka wazi nia zao za kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
Baadhi ya makada wanaotarajiwa kutangaza nia ya urais sambamba na kueleza matarajio yao endapo wataikwaa nafasi hiyo nyeti kuanzia leo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye atautangazia umma jijini Arusha.
Wengine ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira ambaye anatarajia kutangaza nia yake ya kuwania urais kesho jijini Mwanza, wakati Bernard Membe yeye akijipanga kufanya hivyo kijijini kwake, Rondo.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere, anatarajiwa kutangaza azma yake ya kuwania urais Juni Mosi, huko kijijini kwao Mwitongo, Wilaya ya Butiama, pia Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya naye atatumia siku hiyo kufanya hivyo.
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, anatarajiwa kutangaza nia Juni 4, jijini Dar es Salaam, huku Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akitarajiwa kutangaza nia yake Juni 21.
Hata hivyo, kati ya Juni mosi hadi Juni tano, inatarajiwa makada wengi watajitokeza kutangaza nia zao za kuwania urais kupitia CCM.