26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa aipeleka nchi Arusha

lowassaABRAHAMU GWANDU NA ELIYA MBONEA, ARUSHA

NYUMBA za kulala wageni katika Jiji la Arusha na viunga vyake zimeanza kufurika kutokana na makundi ya watu yanayowasili jijini hapa kushuhudia mwanzo wa ‘Safari ya Matumaini’ ya Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, anayoianza rasmi leo.
Mwanasiasa huyo mwenye ushawishi mkubwa miongoni mwa makada wa CCM walioonyesha nia ya kugombea nafasi ya urais kupitia chama hicho, anatarajiwa kutangaza nia leo kuanzia saa 8 mchana katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta, jijini hapa.
MTANZANIA Jumamosi limeshuhudia pilikapilika katikati ya Jiji, Mitaa ya Kaloleni, Makao Mapya, Levolosi na maeneo ya pembezoni ambako kuna nyumba za kulala wageni, baadhi ya watu wakiulizia vyumba ambapo katika nyumba nyingi kuna kibao kinachosomeka ‘vyumba vimejaa’.
Baadhi ya wageni hao ambao walizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotaja majina yao, walisema pamoja na kukosa vyumba, wako tayari kulala nje hadi watakapoianza ‘Safari ya Matumaini’ pamoja na Lowassa.

“Kukosa vyumba si tatizo kwetu, tutalala hata uwanjani, tumesubiri sana siku hii ambayo Mzee (Lowassa) alianza kuitaja tangu mwaka 2013, tunamshukuru Mungu imefika na tutaanza safari ya matumaini pamoja naye,” alisema mmoja wa wageni hao.
Kujaa huko kwa nyumba za kulala wageni, hoteli baadhi ya watu usiku wa kuamkia jana na leo walilazimika kulala kwenye magari.
Taarifa kutoka kambi ya Lowassa zinaeleza kuwa, watu wengi kutoka kada mbalimbali, wanatarajia kushiriki mkutano huo ambao Waziri Mkuu huyo wa zamani pamoja na mambo mengine, atautumia kueleza matarajio yake endapo chama chake kitamteua kugombea urais.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, miongoni mwa waliokwisha kuwasili jijini humo ni pamoja na wajumbe wa NEC wa chama hicho wapatao 187, huku wengine 93 wakitarajia kuwasili usiku wa kuamkia leo.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa mbali na wajumbe hao, pia wenyeviti wa mikoa 23 nchini nao watakuwepo leo katika uwanja huo wa Sheikh Amri Abeid Kaluta.
Wazee maarufu, akiwemo Kingunge Ngombale Mwiru, Pancras Ndejembi, Kanali Mwisongo na Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Mirisho Sarakikya, nao pia wanatajwa kushiriki tukio la leo.
Mbali na kufurika kwa wageni katika Jiji la Arusha wanaosubiri kwa hamu hotuba itakayotolewa na Lowassa hii leo, pia mavazi, ikiwamo sare za CCM zenye utambulisho maalumu kwa ajili ya siku hiyo nazo zimepanda bei maradufu.
Wajasiriamali wanaouza fulana zenye picha na maandishi yanayomtaja Lowassa ambazo zilikuwa zikiuzwa kati ya Sh 10,000 na 15,000, sasa zinauzwa kwa kati ya Sh 20,000 na 25,000, hata hivyo, pamoja na kupandishwa bei bado zimekuwa adimu.
“Fulana hii shingo ya mduara ni Sh 20,000 na hii ya shingo ya v (form six) nauza Sh 25,000 kaka, karibu na zimebaki chache sana mpaka tuagize nyingine shughuli itakuwa imeshafanyika, bora uchukue hii,” alisema mmoja wa wajasiriamali aliyekuwa ametandaza nguo hizo na sare za chama katika moja ya mitaa jijini hapa.

Mbali na kukamilika kwa maandalizi yote ya hotuba muhimu inayosubiriwa kwa hamu na Watanzania ya ‘Safari ya matumaini’, kumekuwa na shamra shamra kila kona, ambapo kila mtaa watu wamekaa vikundi wakijadili kwa heri na wengine kwa shari ‘Safari hiyo ya Matumini’.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Robinson Meitinyiku, alisema tayari maandalizi yamekamilika, kinachofanyika ni vikao vya Kamati ya Maandalizi ambayo yeye ni mjumbe.
“Mimi ni mjumbe tu kwenye kamati, lakini si msemaji, ila ninachokuhakikishia ni kwamba maandalizi yote yamekamilika, ikiwamo mapokezi ya wageni mbalimbali, wakiwemo viongozi wa serikali wa sasa na wastaafu, wanachama wa CCM, wakereketwa wa maendeleo na wananchi wa kawaida,” alisema.
HALI YA UWANJA
Maandalizi katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa yalianza tangu juzi mapema asubuhi.

Tofauti na miaka yote, pengine tangu uwanja huo ujengwe unaweza kuwa haujawahi kupambwa kama ambavyo ulianza kupambwa jana, ambapo kazi hiyo ilitarajiwa kukamilika saa 8:00 mchana jana.
Baadhi ya mapambo yaliyokuwa na rangi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), yalionekana kutawala zaidi katika viwanja hivyo, huku mahema kwa ajili ya tahadhari ya mvua na jua yakiwa yamefungwa.
Mbali na mahema hayo, pia magari makubwa ya mizigo yalikuwa yakipishana kuingiza vifaa mbalimbali kwa ajili ya kazi hiyo ya upambaji, tayari kwa shughuli nzima ya kesho.

VYOMBO VYA HABARI
Mkutano huo wa kutangaza nia wa Lowassa kama ambavyo umekuwa ukitangazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari unatarajiwa kurushwa moja kwa moja pia na vyombo vya habari kutoka ndani na nje ya nchi.
Baadhi ya vyombo vya habari kutoka ndani ambavyo vitarusha moja kwa moja mkutano huo ni pamoja na Televisheni ya ITV, Channel Ten, Clouds TV, EATV, ambapo kwa upande wa redio ni Clouds FM, Magic FM na East Africa Radio.
Lakini pia vyombo vya habari kutoka nchini Kenya navyo vipo mkoani Arusha tayari kwa kufuatilia mkutano huo.
Vyombo hivyo ni pamoja na Televisheni ya Citizen, Nation na gazeti la The Standard.
Kuanza kwa Safari hiyo ya Matumaini ya Lowassa, kumekuja baada ya kukamilika kwa adhabu aliyopewa sambamba na makada wenzake ndani ya chama, baada ya kudaiwa kuanza kampeni na ushawishi kabla ya wakati.
Makada waliokuwa wamepewa adhabu na CCM, mbali na Lowassa, alikuwemo pia Bernard Membe, Steven Wasira, William Ngeleja, January Makamba na Frederick Sumaye.

Tayari vikao vya juu vya CCM vimekwisha kutoa ratiba kamili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, ambapo kwa upande wa urais zoezi la uchukuaji fomu kwa ngazi ya urais litaanza Juni 2, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles