RAMADHAN HASSAN -DODOMA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema wale wote walioweka mabango kwenye mitandao ya kijamii kutia nia katika nafasi za ubunge na udiwani wapo hatarini kukosa nafasi ya uteuzi wa chama kutokana na kuanza kampeni kinyume na utaratibu wa chama hicho.
Pamoja na hilo, CCM kimewataka viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi kuhakikisha suala la kuhesabu kura linakuwa wazi na hadharani mbele ya wanachama wote kama ilivyokuwa kwenye upigaji kura wa kutafuta mgombea urais wa Zanzibar, uliompa ushindi Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Wakati tamko hilo la CCM likija tangu CCM ilipotangaza utaribu kwa watia nia kupita kwenye ofisi za CCM kuuliza utaratibu kuanzia Julai Mosi mwaka huu, makundi ya wana CCM wamekuwa wakisambaza mabango kwenye mitandao ya kijamii yakieleza kugombea udiwani au ubunge jambo ambalo linaelezwa ni ushawishi na kuanza kampeni kabla ya muda.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola ukurasa wa 52 (b) inazungumzia makatazo ya vitendo fulani fulani wakati wa uchaguzi ambapo aliwaomba wahusika kuvizingatia.
Alisema kwa sasa kuna watu wamekuwa wakiweka mabango na vipeperushi katika mitandao ya kijamii ambapo alidai jambo hilo ni kosa kisheria hivyo aliwaonya na kuwataka kuacha mara moja.
“Kwa wale watuhumiwa ambao hawafanyi vitendo vinavyotokana na rushwa lakini bado wanakiuka kanuni za chama hususani zile zinazokataza matumizi ya mabango, vipeperushi kwa maana mabango ama kipeperushi kinaweza kuwa cha mtandaoni , tumeanza kuona watu wanajibandika mtandaoni natangaza nia, ndugu yangu ile ni kosa, umeanza kampeni kabla ya wakati. Kule ni kujipitisha kabla kimtandao kwa wanachama.
“Vipi yule ambaye hawezi kujipitisha kwa mtindo huo? Chama chetu kinaamini katika haki na usawa wa binadamu kampeni chafu vurugu za wapambe unajua wapambe ni matatizo sana na upotoshaji wa makusudi, matusi.
“Hawa wataadhibiwa na Kamati za Siasa za Kata, Wilaya na waache mara moja kufanya vitendo hivyo na watuhumiwa hao watalazimika kutii amri iliyotolewa na kamati hiyo.
“Sasa kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ninawaonya muache mara moja kutumia mabango na vipeperushi kabla ya mchakato wa uchaguzi. Fomu zitaanza kuchukuliwa kesho (leo), wewe unajipiga picha, unaweka katika mapango na vipeperushi ni kinyume na taratibu tulizojiwekea. Ambao hawataacha basi tutaona namna nzuri ya kuwasaidia,” alisema Polepole.
FOMU YA UBUNGE, UDIWANI
Pamoja na hali hiyo Polepole alisema kuwa kumekuwa na maneno mengi kuhusu kiwango cha kuchukua fomu za udiwani na ubunge.
Alisema kwa mujibu wa kanuni ya wateuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola (Bunge na Serikali) inasema kwamba katika nafasi ya udiwani ni Sh 10,000, ubunge Sh 100,000, uspika wa bunge Sh 500,000 na urais ni Sh milioni moja.
Alisema kwamba mara baada ya kutoa fedha kwa ajili ya kuchukua fomu michango mingine ni ya hiari na mtu halazimishwi kutoa.
“Yamekuwepo maneno mitandaoni kuhusu kiwango halisi cha fomu ya wagombea katika nafasi za ubunge na udiwani kwanza Chama Cha Mapinduzi, kinazuia michango holela katika kipindi hichi cha uchaguzi chama chetu kinaongozwa kwa mujibu wa misingi na kanuni.
“Michango yote katika ngazi yoyote ni lazima kwanza ijadiliwe na ipitishwe na Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya eneo husika licha ya kwamba kamati za siasa zina mamlaka ya kuweka mapendekezo ya michango hii, napenda ifahamike kwamba inabaki kuwa ni michnago ya hiyari ni marufuku kwa mwana CCM kulazimishwa kuchanga michango kwenye chama chetu
“Mwana CCM anayeamini ana mchango na anapenda kujitoa kwenye chama chetu afanye hivyo kwa hiari yake katu na kamwe asilani mchango usiwe kigezo cha kumpa ama kumnyima mgombea fomu
“Mtu akishapewa fomu yake unaweza kumweleza chama kimepitisha harambee kwa hiyo wanachama wote wanakaribishwa kuchangia sasa iwe hiyari yake kuchangia ama kutochangia ndani ya vikao tutajua huyu amejitoa kwenye chama ama hakujitoa kwenye chama ni jambo la vikao,” alisema.
UTARATIBU WABADILIKA
Katibu Mwenezi huyo wa CCM, alisema kuwa Mkutano Mkuu umefanya marekebisho ambapo katika nafasi ya udiwani zoezi la kupata mgombea litaanza na Mkutano Mkuu wa Kata baadaye Kamati ya Siasa ya Kata, kisha Kamati ya Siasa ya Wilaya, Mkoa na Halmashauri Kuu ya Mkoa ambayo itatoa jina moja.
“Safari inaanzia kwenye kura za maoni katika eneo husika linalohusika na uchaguzi katika Mkutano Mkuu wa Kata ambako wenyeviti wa mashina (mabalozi) watashiriki pale watapiga kura za maoni ili tupate picha halisi ilivyo hata kama watakuwa wagombea watano wataingia katika kura za maoni na watapata nafasi ya kujieleza na kura za maoni zitapigwa.
“Baada ya kura za maoni kupigwa vikao vya kuwachuja na kuweka mapendekezo vitaanza, itaanza Kamati ya Siasa ya Kata, itakuja Kamati ya Siasa ya Wilaya, itakwenda Kamati ya Siasa ya Mkoa, Halmashauri Kuu ya Mkoa ambayo ndiyo itatoka na jina moja la ambaye ndiyo atapeperusha bendera ya chama kwenye udiwani kwenye kata husika,” alisema Polepole.
Kwenye nafasi ya ubunge na uwakilishi, alisema wataanza na kamati za siasa za wilaya na kwa upande wa Zanzibar ni Kamati ya Siasa ya Jimbo ambapo wagombea watajieleza ni kwanini wanagombea.
Alisema baada ya hapo kamati ya siasa itaweka mapendekezo na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu Taifa wataweka mapendekezo baada ya hapo wataenda Kamati Kuu na kisha wataenda Halmashauri Kuu Taifa ambao wao watajadili hatimaye kuchukua jina moja ambalo ndiyo atakuwa mgombea wa CCM.
MAMBO HADHARANI
Aidha, Polepole alisema wakati wa zoezi la uhesabuji wa kura ni lazima mambo yote yawe hadharani kama alivyoagiza Mwenyekiti wa chama hicho Rais Dk. John Magufuli.
“Mwenyekiti wa CCM ameweka utaratibu vizuri na mfano wenyewe ni jinsi mchakato wa zoezi la kupiga kura za maoni kuwekwa wazi kwa dhahiri shahiri hadharani
“Tunasema kipindi hiki weka masanduku mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wawe 1,000 au 1,500 na wale waliogombea kila mmoja ashiriki kuhesabu mpaka tutakapomaliza mchakato huo, tunataka mchakato wa uchaguzi uwe huru uwe wazi na wa haki.
“Na kama kama mmejipanga mpo huru kuuweka Live tuone demokrasia ilivyo ndani ya CCM, tunasisitiza wakurugenzi na makatibu wa wilaya na mikoa muwe na mawasiliano ya haraka katika makao makuu ya chama,” alisema.
WAGOMBEA KUONDOLEWA
Aidha, Polepole alisema nafasi ambazo ni za watendaji ndani ya chama ambao watagombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa mwaka huu ikaonekana kwamba watakizorotesha chama katika uchaguzi hawatateuliwa.
“Nafahamu ni haki ya mtu kuchukua fomu na kugombea, nataka niliseme jambo hili kwa unyenyekevu mkubwa sana, kanuni ya uongozi na maadili ukienda katika ukurasa wa 18 inazungumzia haki na wajibu wa mwanachama.
“Inasema, mwanachama atakuwa na haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi lakini endapo kugombea nafasi nyingi kutasababisha kuzorota kwa uhai wa chama hatateuliwa.
“Nasema hili kwa unyenyekevu mkubwa wewe ni mwenyekiti wa chama , ndiyo mkuu wa siasa ya kata ndiyo unaisimamia serikali ukaona ukagombee ikiwa kwenda kugombea kwako kutazorotesha chama chetu na kukiweka kwenye hali ya kutokupata ushindi.
“Napenda kuwatamkia mapema kwamba kanuni inasema hatutakuteua ila kuchukua fomu ni haki yako na kwa wenyeviti wa wilaya, mikoa na wajumbe wa halmshauri kuu ya CCM,” alisema.
UCHAGUZI WA JIMBO
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM kuanzia leo Julai 14 hadi 17 ni kuchukua na kurejesha fomu ya ubunge na udiwani na Uwakilishi kwa upande wa Zanzibar.
Julai 20 hadi 21 mikutano mikuu ya kufanyika kwa kura za maoni kwa majimbo na wilaya kwa wagombea ubunge na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Julai 30, mwaka huu vikao vya kamati za siasa za jimbo, kuwajadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za wilaya .
Agosti 1 na 2, vikao vya kamati za siasa za wilaya, kujadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za mikoa.
Agosti 4 na 5, vikao vya kamati za siasa za mikoa, kuwajadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu Halmashauri kuu ya CCM ya Taifa kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibari kutoa mapendekezo kwa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar.
BARAZA LA WAKILISHI
Ratiba hiyo iliyotolewa na CCM inaonesha kuwa Julai 14 hadi 17, itakuwa muda wa kuchukua na kurejesha fomu za kuomba kuteulwia kwuania nafasi za Baraza la Wawakilishi.
Julai 20 hadi21 Mikutano Mikuu ya CCM ya Majimbo/Wilaya, kupiga kura za maoni za wagombea wa ubunge na ujumbe wa Baraza la Wakilishi.
Julai 30, vikao vya kamati za siasa za CCM za Jimbo, kuwajadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za wilaya.
Agosti 1 na 2, kutakuwa na vikao vya kamati za siasa za CCM za Wilaya, kujadili wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa kamati za siasa za mikoa.
Agosti 4 hadi 5, vikao vya kamati za siasa za mikoa, kuwajadili wagombea na kutoa mapendelkezo yake kwa Kamati Kuu.
UBUNGE , UJUMBE BLW VITI MAALUMU
Ratiba hiyo ya CCM inaonesha pia kuwa Julai 14 hadi 17, itakuwa nafasi ya kuchukua na kurejesha fomu kwa ajili ya viti maalumu.
Julai 23 mikutano mikuu ya UWT ya mikoa kupiga kura za maoni kwa wagombea viti vya mkoa na makundi mengine isipokuwa kundi la vijana na wazazi.
Julai 30, Baraza la Vijana la mkoa kupiga kura za maoni wagombea wa Viti Maalumu kundi la Vijana.
Julai 31, Baraza la Wazazi la Mkoa, kupiga kura za maoni kwa wagombea wa viti maalumu kundi la Wazazi.
Agosti 04-05, kamati za siasa za mikoa , kutoa mapendekezo yake yatakayowasilishwa kwenye Baraza Kuu la UWT Taifa.
Agosti 08 Baraza Kuu la UVCCM, kupiga kura za maoni kwa wagombea wa ubunge na uwakilishi Viti Maalumu kundi la Vijana.
Agosti 9, mwaka huu Baraza Kuu la Wazazi, kupuga kura za maoni kwa wagombea ubunge na uwakilishi Viti Maalumu kundi la Wazazi.
Agosti 10, Baraza Kuu la UWT, kupiga kura za maoni kwa wagombea ubunge na uwakilishi viti maalumu na kuandaa mapendekezo yatakayowasilishwa kwenye NEC.
UDIWANI
Kwa upande wa udiwani fomu zitaanza kutolea kuanzia leo Julai 14 hadi 17, mwaka huu, ambapo Julai 27 itakuwa mikutano ya kura za maoni kwa madiwani.
Juali 29, vikao vya kamati za siasa za kata kujadili wagombea na Julai 30 vikao vya kamati ya siasa kutoa mapendekezo yake kwenda kamati za siasa za wilaya.