Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI inawashikilia raia 16 kutoka Lebanon, Pakstan na Somalia kwa mahojiano baada ya kupita chumba cha wageni mashuhuri (VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere huku wakiwa na vibali vinavyotiliwa shaka.
Hatua ya kushikiliwa raia hao imetokea siku tatu tangu Rais Dk. John Magufuli kumwagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumsimamisha kazi Naibu Kamishina wa Idara ya Uhamiaji, Grace Hokororo.
Hokororo alisimamishwa kazi na Majaliwa baada ya kutuhumiwa kuingiza raia 50 wa Somalia na kuwapa vibali vya kuishi nchini kinyume cha sheria.
Habari za uhakika ambazo MTANZANIA ilizipata jana kutoka vyanzo vya kuaminika ndani ya vyombo vya dola, zinasema uamuzi wa kuwashikilia raia ulitolewa na mamlaka za juu.
Habari zinasema walipohojiwa walisema walikuwa nchini kwa ajili ya mapumziko.
Hata hivyo, jambo ambalo lilionekana kuwashangaza maofisa wa ni raia hao baada ya kufika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, kupitishwa chumba cha wageni mashuhuri (VIP).
“Ni kweli watu hawa wanashikiliwa na Idara ya Uhamiaji baada ya kuingia nchini kwa njia ambazo hazitambuliki kisheria.
“Wamehojiwa na maofisa wetu wakasema wamekuja hapa kwa ajili ya mapumziko…sasa watu wanajiuliza wana hadhi gani ya kupitia sehemu ya watu maarufi (VIP).
“Jambo hili tunaona lina ukakasi mkubwa,”kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kilisema baada ya kukamatwa watu hao, Katibu Mkuu wa Wizara wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira na Kamishina wa Idara ya Uhamiaji, Dk. Anna Makalala, jana jioni walilazimika kukutana uwanja wa ndege kwa kikao kizito kushughulikia suala hilo.
“Ni kweli watu hawa wamekamatwa leo (jana) baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kupitia VIP.
“Jambo hili ni zito kwa sababu Katibu Mkuu na Kamishnaa wa Uhamiaji wapo hapa wanaendelea na kikao ambacho kimechukua karibu saa mbili hivi…tuwe na subira nadhani Serikali itatoa majibu tu,”kilisema chanzo chetu.
Alipoulizwa kuhusu kushikiliwa kwa raia hao, Meja Jenerali Rwegasira alijibu: “Nani kakwambia kuna jambo hilo, sina taarifa yoyote ile na wala sipo uwanja wa ndege kama wewe unavyodai”.
Pamoja na kugoma kutoa ufafanuzi huo, inaelezwa kuwa Meja Jenerali Rwegasira aliendelea na kikao hicho ambacho kilimazika karibu saa moja za usiku.
MAJALIWA
Wiki iliyopita, Majaliwa alimsimamisha kazi Hokororo baada ya kikao kizito na makamisha kilichofanyika makao makuu ya idara hiyo.
Alimwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kuunda tume ya uchunguzi kuhusu utoaji wa vibali uraia.
Alisema haiwezekani raia wa kigeni wanaingizwa nchini na kunapewa vibali vya kuishi bila ya kufanyiwa uchunguzi wa kina.
“Idara ya Uhamiaji tunaitegemea kusimamia mipaka yetu na kuziba mianya ya watu kuingia bila ya kufuata taratibu, lakini kwa mapenzi yake ofisa huyu ameruhusu Wasomali kuingia bila kufuata taratibu.
“Tulidhani ni kitu gani kilimsukuma kutoa vibali kwa Wasomali hao ambao hawakuwapo nchini, wameingia na kupewa vibali moja kwa moja kwa mapenzi yake tu, hii ni dosari hatuwezi kuivumilia.
“Hawa Wasomali aliowapa vibali vya kuishi wala hawakuwa wanaishi nchini wameingia tu na kupewa vibali, hivyo Rais ameagiza ofisa huyo akae pembeni na achunguzwe kujua ni kitu gani kilimsukuma kutoa vibali,” alisema.