Na HADIJA OMARY-LINDI
UMOJA wa Waganga wa Tiba za Asili, Mkoa wa Lindi (UMAWATI), unatarajia kuwakutanisha waganga wa tiba hizo kwenye kongamano litakalofanyika katika Manispaa ya Lindi mkoani hapa.
Hayo yameelezwa jana na Mwenyekiti wa UMAWATI Mkoa wa Lindi, Abubakari Kapunda, alipotembelea ofisi za waandishi wa habari Mkoa wa Lindi, mjini hapa.
Kwa mujibu wa Kapunda, kongamano hilo linatarajiwa kufanyika Novemba 18, mwaka huu, kwa kuwashirikisha waganga zaidi ya 150 wa tiba za asili.
“Kongamano hilo litashirikisha waganga kutoka katika wilaya za Nachingwea, Liwale, Ruangwa, Kilwa, Lindi Mjini na Lindi Vijijini.
“Lengo la kongamano hilo ni kuwaunganisha kwa pamoja waganga hao ili pamoja na mambo mengine, waweze kufahamu haki zao za msingi pamoja na kukumbushana umuhimu wa kujisajili katika baraza la tiba za asili ili waweze kutambuliwa na Serikali,” alisema Kapunda.
Kwa upande wake, Katibu wa UMAWATI, Twalibu Mtasiki, aliwashauri waganga hao kujitokeza kwa wingi katika kongamano hilo ili waweze kupata elimu ya namna ya kuboresha tiba zao.
“Kongamano hili ni muhimu sana kwa sababu washiriki watabadilishana uzoefu na mbinu za kufanikisha tiba bila kuleta madhara katika jamii.
“Kwa maana hiyo, nawaomba wale wote wenye sifa za kushiriki, wasisite kufanya hivyo kwani watapata mbinu mbalimbali za tiba na kuondokana na utoaji wa tiba za kizamani,” alisema.