26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wafugaji washauriwa kutumia chanjo ya ndani

Gustaphu Haule -Tanga

WAFUGAJI wameshauriwa kutumia chanjo zinazozalishwa nchini kwakuwa zimefanyiwa utafiti kutokana na vimelea vya magonjwa yanayoshambulia mifugo yao.

Meneja wa Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), unaojihusisha na utafiti wa chanjo za mifugo mkoani hapa, Dk. Imna Malele, alitoa ushauri huo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari wa Kanda ya Mashariki waliotembelea kituo hicho.

Ziara ya waandishi hao iliratibiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), baada ya mafunzo ya siku mbili yaliyolenga kuahamasisha waandishi wa habari kuandika zaidi habari za sayansi zinazotokana na tafiti zinazofanywa na vituo vya utafiti vya hapa nchini.

Dk. Malele alisema chanjo zinazozalishwa nchini zina uhakika na ni bora kwa matumizi ya mifugo waliopo nchini kwakuwa kila tafiti wanazofanya zinatokana na vimelea vya magonjwa husika yanayoshambulia mifugo hapa nchini.

Alisema kituo chake wanafanya tafiti za magonjwa mbalimbali ikiwemo kideli (mdondo), kimeta, chambavu, ugonjwa wa ngozi wa mifugo, homa ya mapafu na magonjwa mengine ya mifugo na kwamba hakuna haja ya kuhangaika na chanjo za nje wakati chanjo za ndani zinajitosheleza.

Aliwataka wafugaji kuhakikisha wanaifanyia uchunguzi mifugo yao kabla ya kuitibia kwakuwa kufanya hivyo inasaidia kujua tiba sahihi dhidi ya magonjwa yanayoshambulia mnyama husika.

“Kuchanja mifugo ni jambo muhimu kwa kuwa bila kufanya hivyo mfugaji anaweza kupoteza mifugo yake kwa asimilia 90, maana wanyama wengi hufa wasipopata chanjo, na ushauri wangu kwa wafugaji kuwa watumie chanjo za ndani kwakuwa ni za uhakika,” alisema Dk. Malele.

Alisema sasa chanjo zilizofanyiwa utafiti na maabara hiyo zinapatikana katika mikoa mbalimbali ya Arusha, Iringa, Sumbawanga, Dodoma, Tanga, Mtwara na Pwani, huku akiwaomba waandishi wa habari  watangaze zaidi umuhimu wa chanjo za hapa nchini.

Ofisa Mtafiti Mkuu Kiongozi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia, Dk. Bakari Msangi, alisema vituo vya utafiti wa masuala ya sayansi vilivyopo nchini vinafanya kazi kubwa, lakini taarifa zake hazifiki kwa jamii.

Alisema kutokana na hali hiyo, Costech imeamua kuja na mpango maalumu wa kutangaza tafiti hizo na ndiyo maana kwa sasa wameanza kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo zaidi katika kuandika habari za sayansi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles