KAMPALA, UGANDA |
LICHA ya Jeshi la Polisi nchini Uganda kupambana na kuwakamata wafuasi 20 wa mwanamuziki na mwanasiasa ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi maarufu kwa jina la Bobi Wine, idadi ya watu wanaojiunga kwenye maandamano hayo inazidi kuongezeka kupitia maeneo mbalimbali nchini humo.
Baadhi ya wafuasi wa mwanasiasa huyo wamedaiwa kupambana na askari huku wakishinikiza kuachiliwa huru kwa Bob Wine ambaye ni kipenzi cha wananchi hususani vijana.
Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Kampala Kaskazini, Michael Musana, amesema wamewakamata wafuasi hao na kuwaweka rumande ambao wanaamini Bob Wine ndiye rais wao.
Hata hivyo, makumi ya waandamanaji waliongezeka mitaani juzi na jana licha ya vitisho, vipigo, utesaji na kuumizwa kutoka kwa Jeshi la Polisi.
Maandamano hayo yameitishwa ili kulishinikiza Jeshi la Polisi kumwachilia huru Bob Wine, huku wakisisitiza kuwa wapo tayari kuendeleza mapambano kama yaliyofanyika miaka 30 iliyopita ya vita na mateso wakati wa kuikomboa Uganda.
Taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari zikimkariri msemaji wa Jeshi la Polisi wa Jiji la Kampala, Luke Owoyesigyire, akisema watuhumiwa wote waliokamatwa kwenye maandamano mjini humo wamewekwa rumande katika makao makuu ya polisi barabara ya Kira.
“Tumewakamata watu wengi na tutawafungulia mashtaka ya kufanya maandamano haramu. Askari wetu wapo maeneo mbalimbali kuhakikisha tunadhibiti mikusanyiko yoyote haramu,” alisema Owoyesigyire.
Awali, polisi walitangaza kuwakamata watu 15 kwa madai ya kuandamana bila kibali ikiwa ni kinyume cha sheria.
Ameongeza kwa kusema: “Wote tuliowakamata awali wamefunguliwa kesi mahakamani na kurudishwa rumande. Wengine tumewakamata leo (jana) wapo rumande pia, lakini hivi karibuni watafikishwa mahakamani.”
Maandamano hayo yanafanyika baada ya kikosi cha kumlinda Rais Yoweri Museveni kumkamata Bob Wine Jumatatu wiki hii alipokuwa kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arua ambako alikuwa akimpigia kampeni mgombea binafsi na mshindi wa uchaguzi huo, Kassiano Wadri.
Kikosi hicho kinamtuhumu Bob Wine kushiriki kwa kuhamasisha wafuasi wake kushambulia msafara wa Rais, kumiliki silaha kinyume cha sheria pamoja na uhaini.
Watuhumiwa wengine ni wabunge Gerald Karuhanga (mbunge wa Ntungamo), Paul Mwiru (Jinja), Kassiano Wadri (Arua) na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Makindye Mashariki, Mike Mabikke, pamoja na wafuasi 29 ambao wamefunguliwa kesi ya uhaini huko Gulu na watakaa rumande hadi Agosti 30, mwaka huu.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi nchini humo limeanzisha operesheni maalumu dhidi ya waandamanaji katika vijiji mbalimbali ambavyo wakazi wake walishiriki kuurushia mawe msafara wa Rais.
Kauli ya familia
Familia ya Bob Wine kupitia kaka yake, Eddie Yawe, ambaye alimtembelea mwanamuziki huyo gerezani pamoja na mkewe, Barbra Itungo Kyagulanyi, amesema hawana imani na Serikali ya Uganda kulinda usalama wa ndugu yao baada ya kumkuta katika hali mbaya kiafya.
“Bob Wine yuko hai, anaimarika baada ya tukio lililomtokea, lakini ni vigumu kumtambua kutokana na hali yake. Tulikwenda na tabibu wetu ili atoe huduma ya matibabu, lakini walikataa kumruhusu kuingia ndani. Ni hali mbaya na inakatisha tamaa kumwona Bob Wine akiwa katika hali ile, ni kama vile niko ndotoni kabisa. Maisha yake yapo kwenye hatari sana na anaonekana kama vile hajiwezi wala kujitambua, pia miguu yake haina ushirikiano,” alisema Yawe.