Na ELIUD NGONDO- SONGWE
BAADHI ya wafanyabiashara wilayani Ileje mkoani Songwe, wameiomba Serikali kutengeneza miundombinu mizuri ya kufanyia biashara katika mpaka wa Isongole ambao unatenganisha nchi za Tanzania na Malawi.
Hayo yamesemwa jana na baadhi ya wafanyabiashara wanaofanyia shughuli zao katika daraja la Mto Songwe ambao ndio mpaka wa nchi hizo mbili za Tanzania na Malawi.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Andakson Kamendu, alisema wao wamekuwa wakifanya biashara zao katika eneo hilo mpaka ambapo kuna daraja la Mto Songwe, hivyo miundombinu iliyopo si rafiki kwa shughuli hizo.
Alisema Serikali kuu imeanza kutekeleza ujenzi wa barabara ya kutoka Mpemba hadi Isongole kwa kiwango cha lami, hivyo kukamilika kwake itakuwa ni fursa ya kuongeza uchumi kwa wananchi.
Alisema wamekuwa wakiuza bidhaa zao mpakani hapo wakiwa wamekaa juani kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu ambayo ingewawezesha kufanya biashara hizo kiurahisi.
Naye Elia Mwampashi, alisema mpaka huo ukiwekewa miundombinu mizuri unaweza kuwa chanzo kikubwa cha kuongeza mapato kwa Serikali ya Tanzania kutokana na nchi nyingi kupitishia mizigo hapo.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Joseph Mkude, alisema Serikali ipo katika mkakati wa kutengeneza barabara ya Isongole hadi Mpemba kwa kiwango cha lami.
Alisema wakandarasi wapo katika hatua ya kujenga makambi ambayo yatatumika wakati wa utengenezaji wa barabara hiyo, hivyo miundombinu ya kibiashara ikiwekwa vizuri itakuwa ni fusa ya kuongeza uchumi.