28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyabiashara wachangia waathirika Kagera

majaliwaNa Khamis Mkotya

WAFANYABIASHARA pamoja na mabalozi wa nchi mbalimbali, wametoa misaada yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.4, kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea mwishoni mwa wiki mkoani Kagera na kusababisha vifo vya watu 17.

Wadau hao walitoa msaada huo jana walipokutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo walitoa michango mbalimbali ikiwamo fedha taslimu, ahadi za  mabati, mifuko ya saruji na mahitaji mengine ya kibinadamu.

Katika hafla hiyo, iliyohudhuriwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, Sh milioni 646 taslim zilichangwa wakati zaidi ya  Sh milioni 700 zilikuwa ni ahadi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwashukuru mabalozi na wafanyabiashara hao kwa kuguswa na tukio hilo na kushirikiana na Serikali kusaidia watu walioathiriwa na tetemeko hilo.

Alisema tetemeko hilo kubwa na la kwanza kutokea Tanzania mbali na matetemeko madogo ambayo yamekuwa yakitokea kupitia Bonde la Ufa.

Alisema tukio hilo limeleta maafa makubwa, licha ya watu 17 kupoteza maisha baadhi ya miundombinu imeharibika, ikiwamo nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 kupata nyufa.

“Leo (jana), nimewaita hapa kwa ajili ya jambo moja tu, kama mnavyofahamu mwishoni mwa wiki tulipata maafa makubwa kule mkoani Kagera, ni tukio kubwa na limeleta madhara makubwa.

“Hali ni mbaya na familia nyingi ziko nje zinahangaika, tunahangaika kwa kushirikiana na wadau kuangalia namna ya kuwasaidia ndugu zetu. Tutashukuru kwa msaada wowote kutoka kwenu, majanga huwa yanakuja ghafla wakati watu wakiwa hawajajiandaa.

“Natumia fursa hii kuwashukuru wale wote walioanza kuchangia wakiwamo wabunge walioridhia kukatwa posho zao ili zipelekwe Kagera,” alisema.

Katika kuhakikisha watu mbalimbali wanapata fursa ya kuchangia, Majaliwa alisema Serikali imefungua akauti maalumu kupitia Benki ya CRDB namba 0152225617300 yenye jina la Kamati ya Maafa Kagera na Swiftcode ikiwa ni CORUtztz.

Alisema Serikali pia inafanya mpango wa kutangaza akaunti za M-Pesa, Tigo Pesa na Airtel Money na watu watakaochangia watatangazwa kupitia vyombo vya habari.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Reginald Mengi, aliishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa wafanyabiashara katika kukabiliana na janga hilo.

“Wafanyabiashara wamenituma niseme, wapo nyuma yako na nyuma ya Serikali, kwani jambo hili linashughulikiwa na Serikali kwa kushirikiana na wafanyabiashara pamoja na misaada kutoka nje.

“Pia wamenituma niseme, uwezo wa kifedha walionao umetokana na huruma za Mungu, lakini pili uwezo walionao umetoka hapa hapa Tanzania, hivyo misaada wanayotoa ni njia mojawapo ya kumshukuru Mungu.

“Hata hivyo misaada ya kwanza itatoka Tanzania, kwani Tanzania itasaidiwa na Watanzania wenyewe. Wenzetu watasaidia kwa huruma zao,sisi tunasaidia kama wajibu wetu,” alisema.

Balozi mbalimbali zilizoguswa na tukio hilo, ni pamoja na ubalozi wa Kuwait nchini uliotoa msaada wa Dola za Marekani 10, 000 na Euro 10, 000.

Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo, mwakilishi wa balozi wa nchi hiyo hapa nchini, Mohamed Al-Amir alisema nchi yake imeguswa na tukio hilo na kueleza kuwa Tanzania na Kuwait zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali.

Ubalozi wa China uliahidi kutoa Sh milioni 100, ubalozi wa Japani vifaa vya ujenzji, ubalozi wa Kenya umetoa msaada wa mablanketi, mabati, magodoro na dawa mbalimbali, huku ubalozi wa Korea ukiahidi kutoa mahitaji ya kibinadamu.

Kwa upande wa wafanyabiashara, Kampuni ya Mohamed Enterprises imetoa mchango wa Sh milioni 100, wakati Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi akitoa mchango wa Sh milioni 110.

Mfanyabiashara Subash Patel aliahidi kutoa mabati ya kuezekea madarasa 50 yenye thamani ya Sh milioni 150, huku Kampuni ya Kamal Industries ikitoa Sh milioni 50 na Kampuni ya Kagera Sugar ikichangia Sh milioni 100 na tani 10 za sukari.

Hata hivyo, makampuni matatu ya mafuta ambayo ni GBP, Oili Com na Moil yameahidi kujenga shule mbili za sekondari zilizoanguka kutokana na tetemeko hilo ndani ya mwezi mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles