WADAU na wapenzi wa muziki wa injili nchini, wametoa wito kwa waratibu wa tamasha la muziki wa injili wakati wa Pasaka, Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam, kuongeza wigo wa kufanyika katika nchi zote za Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa mmoja wa mashabiki wa Tamasha hilo linalobeba malengo ya kuutukuza ufalme wa Mungu na mengineyo ikiwemo kupata fedha za kusaidia makundi maalumu katika jamii, Anna Shibamla wa jijini Dar es Salaam, umefika wakati sasa tukio hilo likawa la nchi za Afrika Mashariki.
“Unajua Tamasha la Pasaka tayari lina sura ya kimataifa kwa sababu limekuwa likiwaleta pamoja waimbaji kutoka nchi mbalimbali, lakini kwa mawazo yangu umefika wakati sasa likawa linafanyika katika nchi za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi,” alisema Anna.
Wazo hilo limeungwa mkono na Jasmin Jeremiah wa Ilonga Kilosa, mkoani Morogoro kwa kusema hiyo itachangia kwa kiasi kikubwa waimbaji wa nchi moja kufahamika katika nchi zote za ukanda wa Afrika Mashariki, hivyo kuongeza wigo wa kupata soko la huduma yao ya uimbaji.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, Alex Msama, amesema ni wazo zuri kwani huduma na malengo yake vitazidi kupanuka na kubeba sura ya kimataifa zaidi.