Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wadau wa Mazingira wameipongeza Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa kutengeneza vifaa vya kukusanya taarifa za uchafuzi wa hewa ambavyo vimetumika katikaJjiji la Dar es Salaam chini ya mradi wa kimataifa wa C 40 kwa kipindi cha mwezi Mei hadi Novemba.
Matokeo ya utafiti huo yameonesha kwamba hali ya uchafuzi hewa katika Jiji hilo sio mbaya sana isipokuwa kwa maeneo machache ikiwa ni pamoja na Dampo la Pugu na Shule ya Msingi Vingunguti hasa muda wa usiku.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumanne Desemba 14, 2021 wakati wa makibidhiano ya Ripoti ya Uchafuzi wa Hewa iliyokusanywa kwa kipindi hicho, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’ilabuzu Ludigija amesema DIT imeonesha ukomavu mkubwa katika teknolojia kwa kutengeneza kifaa hicho ambapo kwa kuagiza nje ya nchi ingekuwa gharama kubwa.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa inayojishughulisha na masuala ya Mazingira iitwayo Stockhom, Philip Osano amesema DIT kwa kutengeneza vifaa hivyo wanatakiwa kupewa kazi katika nchi zote za Afrika.
DC Ludigija amesema uwekezaji wa serikali kwa Taasisi za teknolojia kama DIT una manufaa makubwa kwa taifa kwasababu nchi inapata vifaa ambavyo vingeagizwa nje ya nchi na ukarabati wake kuwa mgumu.
“Kwa namna ya kipekee sana naomba niwapongeze DIT kwasababu wanafanya kazi kubwa sana, kutengeneza kifaa hiki ni jambo kubwa sana hivi vitu tunaona vinatengenezwa nje tu lakini DIT wametengeneza maana yake hata kifaa kikiharibika ni rahisi kufanya ukarabati,” amesema Ludigija.
Amesema serikali imejipanga kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakua safi ndio maana imeanza kusafisha jiji hivyo upimaji huo wa uchafuzi mazingira itasaidia kuimarisha hali ya usafi.
Aidha, amewataka wawakilisha katika mkutano huo kutoka katika Halmashauri za jiji la Dar es Salaam kupeleka taarifa za matokeo ya utafiti huo kwa wakurugenzi wao zikiwa kwa ufupi na zinazoeleweka ili iwe rahisi kutekelezaji katika kuimarisha usafi wa mazingira.
Naye Osano amesema, “Kwa kweli DIT wamefanya jambo kubwa wanatakiwa kupewa kazi hii katika nchi zote Afika, hatujawahi kuona kifaa hiki kikitengenezwa katika nchi zetu Afrika,” amesema Onesmo.Â
Kwa upande wake Mhadhiri wa DIT, Dk. Asinta Manyele amesema vifaa hivyo vya kukusanya taarifa vilipatikana vichache kutoka nje ya nchi hivyo DIT iliamua kutengeneza vingine 14 hapa nchini.
“Tulipata vifaa vichache kutoka nje ya nchi lakini wakati wa Corona hali ilikua mbaya katika kupata vifaa, DIT ambao ndio tumepewa kazi ya kufunga vifaa, kukusanya taarifa na kuzitunza ilibidi tutengeneze wenyewe vifaa vyetu kupitia Design Studio-DIT, vifaa vyote vimefanya kazi nzuri,” amesema Dk. Manyele.
Ameongeza kuwa vifaa hivyo ambavyo vinakusanya taarifa ya uchafuzi mazingira vinakusanya taarifa kila baada ya dakika mbili na kutuma na kwamba, vimefungwa katika Manispaa zote za jiji la Dar es Salaam katika vituo vitatu kila Manispaa isipokua Kigamboni vimefungwa viwili.
Naye Afisa Mazingira wa Jiji la Dar es Salaam, Valence Urasa amesema mradi huo una manufaa makubwa kwao kwani unasaidia kuwapa taarifa ya kuthibiti tatizo hilo na kwamba kupunguza magari kuja mjini watu watumie mwendo kasi na pia usimamizi wa sheria kwa wenye viwanda itasaidia uthibiti.