27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Sura tatu wanufaika wa TASAF

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), unaweza kutumika kama kipimo cha watu kujijenga na namna kila mtu anavyoweza kuwa na mipango yake bila kujali ana kitu kidogo kiasi gani.

Tangu kuanzishwa kwa mfuko huu, mamilioni ya watu wamenufaika kwa kupewa fedha taslim, wengine mifugo kama ng’ombe na mbuzi.

Wanufaika hawa wamegawanyika ambapo baadhi yao walipata fedha hizi lakini maisha yao bado yameendelea kuwa ya chini na hawana matumaini ya kunyanyuka, wengine wamepiga hatua na wako tayari kuachia wenzao ambao wanaamini ni masikini zaidi yao.

Pia kuna fungu la tatu la watu mbalimbali wakiwamo viongozi ambao hawaamini kwamba kaya masikini zinaweza kujikwamua kwa kupewa fedha taslim ama wanaamini kiasi wanachopewa ni kidogo sana na hivyo hakiwezi kuwasaidia kwa namna yoyoye ile.

Mtanzania Digital ilipata fursa ya kutembelea Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, ambapo iliweza kuona makundi ya wanufaika ambao walipewa fedha hizo na sasa wapo tayari kutoka na kuachia wengine wanufaika huku wengine wakidai bila kuendelea kupata ruzuku hiyo maisha yao yatakuwa mashakani.

Jolenice Bahati (70), ambaye ni mjane kupitia Tasaf anaweza kutunza wajukuu zake wawili na vitukuu nane, ingawa anasema bado anataka ruzuku hiyo iendelee.

Bahati ambayo kupitia fedha hizo anaweza kupata bima ya afya, anasema ana bata nane wenye vifaranga 12, kuku wane, na mbuzi watatu ambao anawaongeza kila anapopata fedha za Tasaf.

Anne Chacha (68) anasema “Mtu anayesema hii fedha ni kidogo na haisaidii ni mwendawazimu, mimi nilianza kupewa Sh 48,000 ambayo iliniwezesha kukuza mtaji wangu ambapo mwanzo nilikuwa nauza chai na mbege, sasa nimebadilisha na nauza genge ambalo limenifanya nijenge nyumba yangu.”

Kwa upande wa Federica Swai (50), anasema Tasaf imememfanya atoke kwenye vibarua vya kufua nguo kwenye majumba ya watu ili kukimu maisha hadi kuwa mfugaji anayejitengemea na kusomesha watoto wake.

Swai ambaye ni mkazi wa Kata ya Njoro Mtaa wa Viwanda, anasema kwa sasa anafuga bata, mbuzi, kuku, ngombe na sungura.

“Mwanzo niliuza baadhi ya mifugo nikakopa na hela kidogo kasha nikanunua ng’ombe mmoja na sasa wapo wakubwa watatu na ndama,” anasema.

Kwa sasa mama huyu anasema amepiga hatua na anaweza kukubali kutoka kwenye mpango huo kwa hiyari ili watu wengine waingie.

“Sasa kama nilikuwa nategemea vibarua vya kufua kwa watu ili nile, ama kuzunguka kuomba unga ili watoto wale sasa hivi ninamifugo yangu hapa kwanini nisikubali kutoka ili wengine wenye uhitaji kama niliokuwa nao waingie nao wapate maisha kama yangu?,” anasema.

Kwa upande wa Zainabu Bakari Swai, ambaye pia waliingia kwenye mpango huo pamoja mwaka 2015, anasema anaamini bado inibidi azidi kupata fedha hizo za ruzuku ili aweze kuendesha maisha.

Anasema kuwa anajishughulisha na biashara ya kukaanga ndizi na samaki, lakini changamoto ya kupanda kwa bei ya mafuta ya kupikia imekuwa ikiyumbisha pia mtaji wake.

Mkurugenzi wa Mifumo na Mawasiliano kutoka Tasaf, Fariji Mishael, anasema kwa ujumla wanufaika wa mpango huo wamepega hatua huku wengine wakiwa wameweza hadi kumudu kujenga nyumba za kisasa.

“Kuna improvement kubwa, wapo waliofanikiwa hadi kujenga nyumba lakini haimaanishi kwamba ruzuku yet undo pekee iliyotumika, kuna njia nyingine wametumia hadi wakafika huko,”anasema.

Mishael pia anaamini watumishi wa halmashauri wakiwamo wale wa kilimo na mifugo wakitumika vizuri kwa kutoa elimu kwa wanufaika hawa, matokeo mazuri zaidi yataonekana.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Rashid Gembe, anasema Tasaf si kwamba imesaidia watu kuinua maisha yao pekee bali pia watoto kuweza kwenda shule.

“Kuna waliokuwa hawaendi shule kwa kisingizio cha madaftari, nguo ama vitu vingine kama hivyo, lakini wazazi wao wakipata hizi fedha wanaweza kumudu hayo majukumu na watoto wakaenda shule,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles