26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau wa Uvuvi watakiwa kutunza kisiwa cha Goziba

Renatha Kipaka, Muleba

Wadau wa uvuvi katika kisiwa cha Goziba kilichoko wilayani Muleba mkoani Kagera wamehimizwa kukitunza kisiwa hicho kwa kuwa ni chanzo kikubwa cha mapato.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Elias Kayandabila alipotembelea kisiwa hicho juzi kwa ajili ya kuona shughuli za uvuvi hususan wa dagaa zinavyofanyika.

Amesema shughuli ya uvuvi wilayani humo ndio chanzo kinachoingiza mapato makubwa sana kwa wilaya ya Muleba.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Muleba mkoani Kagera, Elias Kayandabila(aliyevaa barakoa), akimsikiliza mdau wa uvuvi.

Hata hivyo amesema kisiwa cha Goziba peke yake kwa mwezi mapato yanayokusanywa ni Sh milioni 40 mpaka Tsh milioni 45, huku asilimia 20 ya mapato yao ikirudishwa kijijini kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa zahanati, vyumba vya madarasa, nyumba za watumishi na ujenzi wa gati.

“Nimetembea na kujionea shughuli mbalimbali za uvuvi zinazoendelea kisiwani hapa, dagaa wa Muleba ni wasafi na hawana mchanga kwasababu hawaanikwi chini hivyo nawakaribisha sana wafanyabiashara na wadau wengine kuja kununua dagaa hawa wanaoandaliwa katika hali ya ubora kutoka visiwa vya Muleba. Na tukumbuke kuwa tayari soko la dagaa limefunguliwa eneo la Magarini, kijiji Katembe, kata ya Nyakabango,” ameeleza Kayandabila.

Hata hivyo, amesema kuwa taratibu zote za ununuzi zinafanyika katika soko hilo ikiwemo utoaji wa vibali vya usafirishaji hivyo kuondoa usumbufu kwa wanunuzi wanaotoka ndani na nje ya nchi ambapo hapo awali wasafirishaji iliwalazimu kufuata vibali Bukoba.

Aidha ameleeza kuwa pamoja na Visiwa vya Muleba kuzalisha kwa wingi zao la dagaa, ulikuwa huwezi kukuta mahali popote takwimu zikionesha dagaa wametoka katika wilaya ya Muleba, kwa hali hiyo tangu soko lifunguliwe sasa takwimu sahihi za usafirishaji wa dagaa zinaonekana hali ambayo imepelekea kupata ushuru wa huduma (Service Levy) na hivyo kuinua mapato ya Halmashauri.

Kayandabila amesema kuwa wananchi wamekuwa wakiibua miradi ukiwemo mradi wa ujenzi wa gati na Halmashauri inapokea na kuunga jitihada zao.

Ameeleza kuwa endapo gati hili likikamilika litasaidia sana maegesho ya mitumbwi na meli lakini pia abiria kushuka na kupanda katika boti na meli hizo kwa mazingira wezeshi.

“Nimeona ipo haja ya kukamilisha ujenzi wa daraja kwani boti zinazotoka kuvua na kuleta samaki mwaloni hazina utaratibu mzuri wa kusimama hivyo kupelekea kuwa na vurugu wakati wa kuuza mazao ya samaki. Pia litarahisisha abiria kupanda na kushuka katika boti na meli kwa urahisi,” ameeleza ndugu Kayandabila.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles