Na Editha Karlo, Kigoma
Wadau wa kupinga ukatili kwa wanawake na watoto mkoani Kigoma wametakiwa kuungana na kufanya kazi kwa pamoja ili kukabiliana na changamoto zinazosababisha kesi nyingi za ukatili na udhalilishaji kwa watoto kushindwa kufikishwa mahakamani.
Katibu Tawala msaidizi wa huduma za serikali za mitaa katika sekretarieti ya Mkoa wa Kigoma, Moses Msuluzya ametoa kauli hiyo katika warsha ya siku tatu ya wadau wa kupinga ukatili mkoani Kigoma ulioitishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya wanawake (UN WOMEN) ili kujadili changamoto za kukabiliana na tatizo hilo.
Msuluzya amesema kuwa kumeonekana kuwepo kwa changamoto kubwa ya kuendelea kwa matendo ya ukatili na udhalilishaji kwa watoto na wanawake mkoani Kigoma kutokana na baadhi ya taratibu za kisheria kutofuatwa ambazo zinaharibu ushahidi na kufanya kesi nyingi kutofika mahakamani au kutochukuliwa hatua stahiki kwa ushahidi kukosekana.
Kwa upande wake Mkuu wa dawati la jinsi kutoka jeshi la polisi mkoa Kigoma, Doris Sweke amesema kuwa jumla ya kesi 881 za ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto zimeripotiwa katika dawati la jinsia la jeshi la Polisi mkoani Kigoma huku kati ya hizo kesi 138 pekee ndio zimefikishwa mahakamani.
Sweke amesema kuwa Ushirikiano hafifu kutoka kwa waathirika wa matukio hayo na wakati mwingine kuharibu ushahidi au kuwakana watuhumiwa imechangia kufanya kesi nyingi zinazoripotiwa kutokuwa na ushahidi thabiti wa kuwatia hatiani watuhumiwa.
Mratibu huyo ametaja kesi nyingi zinazofikishwa kwenye dawati kuwa ni mimba za utotoni, ubakaji na udhalilishaji kijinsia ambapo kesi nyingi zimewahusisha waathirika na watuhumiwa kuwa na mahusiano ya kindugu ambayo yamechangia kuharibiwa kwa ushahidi au walalamikaji kutofuatilia mashauri yao polisi na hivyo tuhuma hizo kushindwa kufikishwa mahakamani kwa kukosa ushahidi.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya wilaya Kigoma, Eva Mushi amesema kuwa ushahidi usiotia shaka ndiyo pekee unaoweza kumfanya hakimu kutoa hukumu stahiki kwa watuhumiwa na kwamba waathirika na familia wamekuwa chanzo cha kuharibu ushahidi.
Mushi amesema kuwa pamoja na elimu inayotolewa kwa jamii na kuogezeka kwa taarifa za matukio ya ukatili na udhalilishaji kijinsia bado wanao hukumiwa kwa makosa hayo imekuwa chini kwa sababu waathirika, watuhumiwa na familia kuamua kuitoa kesi mahakamani na kumaliza suala hilo kifamilia hivyo ni ngumu kwa makosa hayo kupungua kwa sasa.
Mratibu wa mpango wa kupinga ukatili na unyanysaji kijisnia kwa wanawake na watoto kutoka shirika la UN Women, Lucy Tesha amesema kuwa warsha hiyo imelenga kuwaweka pamoja wadau kutathmini na kuweka mpango wa baadaye wa kujadili mbinu zenye mafanikio katika mapambano dhi ya vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto mkoani Kigoma.