Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
WAKATI dunia ikiadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia Duniani, Kampuni ya Ekima Consultants na wadau wa maendeleo wameandaa tamasha la wanawake lenye lengo la kuwawezesha na kuwahamasisha kujikwamua na changamoto baada ya janga la Uviko-19.
Tamasha hilo lenye kaulimbiu ya ‘Anza Upya’ linalotarajiwa kufanyika Desemba 9 jijini Dar es Salaam lina lengo la kukuza uwezo wao katika kuchangia maendeleo endelevu.
Mada zitakazotolewa zitaangazia afya ya akili, ustawi, uwezeshaji wa kifedha na kiuchumi, kujijali na afya ya wanawake ambazo zitatolewa na wataalamu kutoka sekta ya afya, taasisi za kifedha, mashirika na makampuni binafsi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, mwandaaji wa tamasha hilo,m Mkurugenzi wa EKIMA Consultants, Marion Elias, amesema linawalenga wanawake walioajiriwa na waliojiajiri wenye umri kuanzia miaka 25 hadi 65.
Amesema kama sehemu yao ya kushiriki kwenye kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia Duniani, tamasha hili litakuwa na mada zitakazomwezesha mwanamke kutambua viashiria vya ukatili wa kijinsia au kiuchumi na kuchukua hatua ili kujilinda yeye na jamii kwa ujumla.
“Moja ya vikwazo vinavyowakabili wanawake ni ukatili wa kiuchumi na masuala ya usimamizi wa fedha, tunalenga kutatua baadhi ya changamoto zinazodhoofisha ukuaji wao kiuchumi ikiwemo mipango ya kujiwekea akiba, ukosefu wa huduma za kifedha kama vile huduma za kibenki na mikopo, mipango duni ya uwekezaji, mgawanyo mbaya wa rasilimali na nyingine,” amesema Marion.
Amwsema pia washiriki watajengewa uwezo na kuhamasishwa katika mambo mbalimbali ikiwemo kutumia ujuzi, uvumbuzi na ubunifu ili kukuza biashara na taaluma zao na kutimiza malengo waliyojiwekea.
“Tunataka kuona maendeleo ya kudumu ya kweli na yenye faida yatakayomwezesha mwanamke kujiendeleza, kujisimamia na kuweza kupiga hatua katika maisha,” amesema.
Naye Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Kampuni ya ‘Active Mama’ inayojihusisha na masuala ya mama na mtoto, Ernestina Mwenda, ametaja changamoto zinazowakabili wakinamama baada ya uzazi, ikiwemo kushindwa kuendelea na ajira na kwamba wanatarajia kuhamasisha wanawake kutafuta mbinu mbadala za kujiendelea kiuchumi baada ya kujifungua.
Amehimiza makampuni na mashirika mbalimbali kutumia tamasha kama fursa ya kuwazawadia wafanyakazi na wateja wao kwa kuwawezesha kushiriki kwenye tamasha hilo linalotarajiwa kukutanisha wanawake zaidi ya 200 kutoka mikoa mbalimbali.