30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Wadaiwa sugu kodi ya ardhi Simiyu wapewa miezi miwili

Na Derick Milton, Simiyu

Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Simiyu, Essau Mwakatumbula ametoa muda wa miezi miwili kwa wadaiwa wote sugu wa kodi ya ardhi mkoani humo kuhakikisha wanalipa kodi hizo ndani ya muda huo kabla ya hatua kali za kisheria hazichakuliwa.

Essau amesema kuwa katika mkoani humo wapo wananchi ambao wanadaiwa kiasi kikubwa cha kodi, wakiwemo waliofikisha zaidi ya miaka 10 bila kulipa kodi hiyo licha ya kukumbushwa mara kwa mara.

Kamishina Msaidizi huyo ametoa wito huo leo Alhamisi Julai 1, 2021 akiwa wilayani Maswa wakati wa Maofisa wa ardhi kutoka Wizara ya Ardhi Dodoma, pamoja na Ofisi ya mkoa kutembelea wilaya hiyo kwa ajili ya kuangalia ukusanyaji wa kodi hiyo pamoja na kutembelea wadaiwa.

Amesema kuwa katika mkoa huo wadaiwa sugu ni wamiliki wa makampuni na kwamba baada ya muda huo kumalizika hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa katika baraza la ardhi zitachukuliwa na kutaifishwa kwa mali zao.

“Tuna wadaiwa sugu hasa wamiliki wa kampuni, tunatoa muda hadi Septemba, Mwaka huu kila mdaiwa afike katika ofisi za ardhi kwenye halmashauri yake kwa ajili ya kuingia makubaliano ya namna gani ataweza kulipa kodi anayodaiwa ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema Mwakatumbula.

Aidha, ametoa rai kwa wananchi kujenga tabia ya kulipa kodi ya ardhi kwa wakati kwani kiasi kinacholipwa ni kidogo sana na siyo kulimbikiza madeni na kushindwa kulipa ndani ya muda unaotakiwa.

Kwa upande wake Ofisa ardhi Wilaya ya Maswa Vivian Mkamba amesema kuwa Ofisi yake imeendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wadaiwa sugu wa Kodi ya ardhi.

“Mpaka sasa idara imewafikisha katika Mahakama ya ardhi zaidi ya watu 40 kutokana na kutolipa kodi hiyo kwa muda mrefu, na kati ya hao 12 wamelipa tayari na wengine waliobaki kesi zao zipo Mahakama bado,” amesema Vivian.

Aidha ameongeza kuwa mbali na kuchukua hatua hizo, idara hiyo imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari na matangazo ya kulipa kodi ya ardhi kwa hiari na wakati.

“Wakati mwingine tunaamua kuwapelekea akra zao kwenye makazi yao wenyewe na kuwakumbusha kulipa kodi hiyo na umuhimu wake kwa maendeleo ya Taifa,” amesema Vivian.

Naye Ofisa ardhi kutoka Wizara ya Ardhi Henerietha Ghozi amesema kuwa Wizara inawataka wadaiwa wote kuhakikisha wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria ili kuondoa usumbufu wa kuuziwa mali zao na kufutiwa miliki zao.

“Kama Wizara ya Ardhi tunawataka wadaiwa wote wa kodi ya pango la ardhi mkoa wa Simiyu kuhakikisha wanalipa madeni yao yote ili kuepuka usumbufu wa kuuziwa mali zao au kututiwa miliki zao,” amesema Ghozi.

Upande wake, Eraston Mitanda mmoja wa wadaiwa ameishukuru Maofisa hao kwa kumkubusha kulipa deni, huku akibainisha chanzo cha kushindwa kulipa ni kutokuwa na uelewa nani anatakiwa kulipa hata akiwa mzee.

“Mimi nilifikiri sisi watu ambao ni wazee na tumestaafu kazi za umma, serikali imetusamehe kulipa kodi hii, nashukuru kwa elimu ya leo na nitahakikisha naenda kulipa Kama ankra ambayo nimeletewa inavyooleza,” amesema Mitanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles