Na Walter Mguluchuma-Katavi
NI visa na mikasa, ndivyo unaweza kusema baada ya kuibuka mtafaruku mkubwa katika Kijiji cha Sitalike wilayani Mpanda mkoani Katavi, baada ya wachungaji watatu wa Kanisa la Uzima na Ufufuo kuibuka na kudai wana uwezo wa kumfufu marehemu.
Wachungaji hao walifika kwenye kijiji hicho kuendesha maombi ya siku tatu mfululizo marehemu Raymond Mirambo aliyezikwa Mei 7, mwaka huu, aweze kufufuka.
Akisimuliwa tukio hilo jana, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Christopher Anjelo, alisema awali wachungaji hao walifika ofisini kwake na kutaka kupewa ushirikiano kwenye maombi hayo ya kumfufua marehemu huyo.
Alisema wachungaji hao walifika kwenye ofisi ya kijiji na kujitambulisha kuwa wao ni wachungaji wa Kanisa la Uzima na Ufufuo kutoka kijiji jirani cha Nsimbo na wamekwenda kwa wito wa ndugu wa marehemu, Raymond Mirambo.
“Walipofika hapa walisema wanataka kufanya maajabu ambayo ni ya historia nchini ya kufanya maombi mfululizo na kumfufua marehemu Raymond aliyekuwa amefariki dunia na kuzikwa hapa kijijini.
“Kwa kuwa walisema wao ni watu wema sisi kama viongozi wa kijiji tuliwapa baraka wachungaji hao kufanya maombi ya kumfufua marehemu.
“Tulikwenda nao hadi nyumbani kwa marehemu na kuwakuta ndugu wakiwa wanasubiri maombi ya kumfufua ndugu yao kuweza kumrudisha tena kwenye uhai,” alisema Anjelo.
Hata hivyo, maombi hayo yalifanyika kwa siku saba mululizo, mchana na usiku bila mafanikio hali iliyowafanya ndugu wa mrehemu Raymond kupatwa na hasira na kuhisi wachungaji hao ni matapeli.
“Inakuaje maombi yanafanyika kwa siku saba marehemu hafufuki? Ndugu wanahisi kuna jambo na maombi haya yalikuwa yakigharamu fedha pamoja na chakula kwa ndugu na jamaa waliokusanyika nyumbani kwa marehemu.
“Hapo ndipo walipoanza kupambana nao kwa maneno hali iliyozusha vurugu kubwa,” alisema.
Kutokana na vurugu hizo viongozi hao wa kijiji walikwenda kwenye eneo hilo la maombi na kukuta ndugu wa marehemu wanapambana kwa maneno na wengine wakitishia kuwapiga watu hao, ndipo uongozi huo ulipoamua kuingilia kati.
“Tumewaondoa chini ya ulinzi wa serikali ya kijiji na kama tusingefanya hivyo hali ingekuwa mbaya zaidi.
“Bahati nzuri nao baada ya kuona hali imebadilika walitii agizo la serikali ya kijiji na kuondoka,” alisema Anjelo.