Na NORA DAMIAN,DAR ES SALAAM
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Free Pentekoste (FPTC), David Batenzi, amewatahadharisha wachungaji wa kanisa hilo kuepuka kuwekwa mifukoni na vikundi vya watu na badala yake waliongoze kanisa hilo kama Mungu anavyokusudia.
Amesema baadhi ya makanisa yamekuwa yakiendekeza ubaguzi kwa kuwapa kipaumbele watu wenye fedha kitendo alichokitafsiri kuwa ni umaskini wa viongozi wa roho.
Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa Misheni ya Kunduchi iliyoenda sambamba na kumsimika mchungaji kiongozi wa misheni hiyo, alisema hatarajii kanisani kuwe na matabata au madaraja.
“Kwenye makanisa mengine mtu akitoa ‘dau’ kubwa misa ndio inakuwa ndefu, mnajaribu kumhonga Mungu…kanisani hatutarajii kuwe na matabaka au madaraja kwa sababu ya watu fulani wenye fedha.
“Wote ni sawa mbele za Yesu, damu iliyoosha matajiri ndio hiyo hiyo iliyoosha watu wa hali zote,” alisema Askofu Batenzi.
Pia aliwaasa waumini na viongozi wa kanisa hilo kudumisha maombi ili maisha yao yaendelee kung’arishwa na kufanya upya ndani ya Mungu.
“Wapentekoste mmesahahu hata maombi na kufunga, mchungaji, mzee wa kanisa kushinda na njaa saa 12 anaona shida.
“Ndoa inatikiswa, kazi inayumba omba, tuongeze kiwango cha maombi kitafungua milango ambayo hatukuitarajia katika maisha yetu,” alisema.