22.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Wachumi: Ni bajeti chungu kwa makabwela

Dk. Philip Mpango
Dk. Philip Mpango

NA WAANDISHI WETU,

WAKATI mjadala wa mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2016/17 ukiendelea kupasua vichwa vya wananchi, wabobezi wa masuala ya kiuchumi wamebaini kwamba kundi la watu wa kipato cha chini ndilo litakaloumia katika utekelezaji wa bajeti hiyo. MTANZANIA Jumamosi linaripoti.

Mapendekezo ya bajeti hiyo ambayo yaliwasilishwa bungeni katikati ya wiki hii  na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, yameainisha mambo kadha wa kadha ambayo yatasaidia utekelezaji wa bajeti hiyo.

Katika mapendekezo hayo ya bajeti, serikali imepanga kukusanya Sh trilioni 29.5 kutoka vyanzo vya mapato, ikiwamo kodi, misaada na mikopo, mapato yasiyotokana na kodi pamoja na mapato ya Halmashauri, huku ikilenga kukusanya kiasi kikubwa kutoka vyanzo vya ndani.

Baadhi ya wabobezi wa masuala ya uchumi nchini waliozungumza na gazeti hili wametazama mapendekezo ya bajeti hiyo kwa jicho la kuumizwa kwa wananchi wa tabaka la chini.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taassi ya Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi (ESRF), Dk. Oswald Mashindo, alisema utekekelezaji wa bajeti hiyo una kila mazingira ya kuwaumiza wananchi wa kipato cha chini  kwa namna moja au nyingine.

Alisema pamoja na bajeti hiyo kutenga kiwango cha kuridhisha katika  maendeleo, lakini suala la kodi litachochea moja kwa moja kuwaumiza wananchi wa kipato cha chini.

Alisema ongezeko la kodi limelenga kuwabana wananchi wa tabaka la kati ambao wengi wao wanavipato vya wastani vyenye kuweza kuhimili msukosuko wa uchumi.

Alisema ndani ya kundi hilo kuna wafanyabiashara wengi ambao siku zote wanapopandishiwa kodi, wao huwabebesha mzigo huo wa kodi wananchi wa kipato cha chini ambao ndio wateja wao wakubwa.

“  Ukweli ni kwamba kundi litakaloathirika zaidi na utekelezaji wa bajeti hii ni kundi la watu wa kawaida, masikini…ukiniuliza wanaathirikaje nitakwambia kwamba mara nyingi wafanyabiashara wanapopandishiwa kodi mzigo huo huwahamishia walaji.

“ Wanaoathirika zaidi ni watu wa tabaka la chini kwa sababu matabaka yanayofuata juu wanaweza kuhimili uchumi na mapato yao ni makubwa zaidi…siku zote unapokuwa na kipato kizuri mitikisiko yoyote unaweza ukahimili kwa sababu unacho cha kuweza kuhesabu lakini mtu wa kipato cha chini anaweza kuumia zaidi,” alisema Dk. Mashindo.

Aliongeza kwamba kwa mujibu wa vipimo vya uchumi katika kiwango cha vigezo vingi vya kupima kiwango cha umaskini (MPI) asilimia zaidi ya 60 ya Watanzania wanaishi katika tabaka la watu wa kipato cha chini huku aslimia 10 ni masikini kabisa.

Alisema kupitia vipimo hivyo, asilimia 30 walau wanavipato vya wastani huku wachache miongoni mwao ndio wenye vipato vya juu.

Hata hivyo alisema serikali inaweza kupunguza ukali wa maumivu ya bajeti kwa watu wa tabaka la chini kama ukusanyaji wa mapato utalenga kuwahudumia watu wa tabaka hilo

“ Watu wa tabaka la kati pamoja na juu hawataguswa kabisa na maumivu ya bajeti licha ya kwamba watabanwa, makundi haya ndiyo yenye wafanyabiashara ambao hata wakibanwa na kodi, wao watasafirisha maumivu ya kodi kwa watu wanaoishi tabaka la chini.

“ Unatakiwa ujue kwamba haya makundi ya juu katika kipato yanaweza yasijue kama kumepandishwa kwa bidhaa ya bia , lakini wale wa tabaka la chini ambalo lina idadi kubwa ya wananchi lazima maumivu hayo yawaguse kwa kiasi kikubwa,” alisema Dk. Mashindano

Mtazamo huo wa wachumi unaakisi taarifa ya 8 ya Benki ya Dunia kuhusu hali ya Uchumi wa Tanzania ambayo iliwasilishwa hapa nchini mwezi uliopita.

Taarifa hiyo ilitanabaisha kwamba pamoja na uchumi wa Tanzania kwa wastani umekuwa juu, lakini asilimia 50 ya wananchi wake bado ni maskini.

Akizungumza katika uzinduzi wa taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini, Bella Bird alisema ndani ya kiwango kiwango hicho cha umasikini, Watanzania milioni 12 ni masikini wa kupindukia.

Alisema kundi la Watanzania ambao ni maskini wa kupindukia wengi wao wanaishi chini ya kipato cha Sh. 1,300 kwa siku.

Katika muktadha huo huo naye Profesa wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Haji Semboja, alisema kuna uwezekano wa wananchi wasio na kazi kuumia zaidi katika utekelezaji wa bajeti hiyo.

Alisema kutokana na hali hiyo inahitaji kila mtu kutafuta kazi ya kujishughulisha ili aweze kuingia kwenye mzunguko wa fedha.

“Serikali itakuwa inatumia fedha kwenye uwekezaji ambao nao unategemea huduma kutoka kwa wananchi hivyo wale watakao changamkia ajira iwe ya kuajiriwa au kujiajiri  ndio watakaofaidi lakini wale ambao hawajishughulishi na kitu chochote lazima wataumia,” alisema Profesa Semboja.

“Nashauri kama alivyosema waziri watu wasikae vijiweni badala yake wachangamkie fursa zitakazotokana na uwekezaji utakaofanywa sehemu mbalimbali.

“Wale watu ambao walizoea kukaa na kusubiri kuomba vijiweni hawataweza kumudu maisha yao lakini wale wanaoingiza kipato wataendelea kupata,” alisema.

Hata hivyo alisema inabidi watu wakubali kujinyima baadhi ya vitu ambavyo si vya lazima kwa maendeleo ya baadae.

“Kuna kitu kinaitwa ‘Trade Off’ kwamba lazima uwekeze leo kwa manufaa ya baadae na mtu unapotaka kuwekeza lazima ukubali kutumia fedha zako kwenye uwekezaji huo.

Alisema ni lazima wananchi wakubali kuchangia kuleta maendeleo kwa kujitoa badala ya kuendelea kutegemea misaada na serikali kuhakikisha inatoa huduma nzuri.

“Wananchi waache kupenda kufanyiwa kila kitu na badala yake wachangie kupata mapato na wasipochangia tutaishia kuombaomba,” alisema.

Alisema ni asilimia 20 tu ya mapato inayochangiwa moja kwa moja kutoka kwa wananchi na kwamba zingine zinatoka bandarini asilimia 43 huku asilimia 35 ikichangiwa na kampuni kubwa.

Akizungumzia kuhusu huduma za utalii kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) alisema inaweza kupunguza watalii kwasababu bado hakuna huduma nzuri za kwenda sambamba na kodi hiyo.

“Sina taarifa sahihi kwamba watalii wanaweza wasije kwasababu ya kodi na tatizo lililopo Tanzania ukilinganisha na Kenya ni kwamba hakuna huduma nzuri za kuwashawishi kuja kufanya utalii hivyo kuongeza kodi kunaweza kukachangia kuwapoteza zaidi,” alisema.

Kuhusu Kenya kufuta kodi ya aina hiyo alisema inatokana na nchi hiyo kupoteza watalii kwasababu ya masuala ya usalama.

“Wanachofanya wao ni kujaribu kuwavuta kwa namna nyingine tofauti na ile ya huduma nzuri za hoteli, viwanja vya ndege na miundombinu mingine,” alisema Semboja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles