HERIETH FAUSTINE NA TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili ambao ni raia wa China kwa tuhuma za kumteka mwenzao, huku wakitaka kulipwa Dola za Marekani 19,000 ambazo ni zaidi ya Sh milioni 40.
Watuhumiwa hao ni Wang Young Jing (37) na Chen Chung Bao (35), ambao wanadaiwa kumteka nyara mfanyakazi wa Kasino ya Le Grande, Liu Hong (48) ambaye naye ni raia wa China.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 23, mwaka huu baada ya jeshi hilo kupata taarifa ya watu wasiojulikana kumteka Liu ambapo watekaji hao walitoa sharti ya kulipwa Dola za Marekani 19,000 ili waweze kumwachia.
“Baada ya kupata taarifa za kutekwa kwa mfanyakazi huyo, tuliunda kikosi kazi kwa ajili ya ufuatiliaji wa tukio hilo, ndipo tulipobaini kuwa wateka nyara hao walikuwa katika Hoteli ya Palm Beach.
“Tulifika katika hoteli hiyo na kuanza kukagua chumba kimoja hadi kingine, tulipofika chumba namba tisa na kugonga wahusika waligoma kufungua, wakati polisi wanajiandaa kuvunja mlango, ndipo mtuhumiwa mmoja Wang Young Jing, aliamua kufungua mlango na kukamatwa akiwa na Liu Hong ambaye ni mtekwaji,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema askari walipoingia katika chumba hicho walimkuta aliyetekwa nyara akiwa hajitambui, huku akiwa na majeraha usoni yaliyosababishwa na kupigo.
Alisema polisi walimkamata mtuhumiwa Chen Chung Bao (35), ambaye ndiye aliyekodi chumba hicho.
Alisema katika chumba hicho walikuta vipande viwili vya taulo ambavyo walikuwa wakivitumia kumfunga mikono, kamba za plastiki na bomba la sindano.
Alisema watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
Katika tukio jingine, Kamanda Sirro, alisema kupitia msako mkali uliofanyika pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam, wamefanikiwa kuwakamta watuhumiwa 57 kwa makosa mbalimbali.
Alisema baadhi ya watuhumiwa hao ni pamoja na wahalifu wanaotoka katika vikundi vya Panya Road, Black Amerika, Taifa Jipya na Kumi Nje Kumi Ndani.
“Kupitia msako mkali tuliofanya tumefanikiwa kukamata watuhumiwa 57, ambapo katika Mkoa wa Temeke tulikamata 21, Ilala 19 na Kinondoni 17
“Watuhumiwa hao tumewakamata kwa nyakati tofauti maeneo ya Kivule, Mbagala, Buguruni, Kiluvya, Gongo la Mboto, Tandika, Ukonga, Banana, Kunduchi, Kawe na Keko kwa makosa mbalimbali yakiwemo kuvunja nyumba usiku na kuiba, kuvuta na kuuza bangi, kuuza na kunywa gongo,” alisema.