27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

WACHINA ‘SAMAKI WA MAGUFULI’ KWENDA MAHAKAMA YA KIMATAIFA

Na KULWA MZEE – DAR ES SALAAM

KAMPUNI ya uwakili ya L & B inayowatetea raia wa China – maarufu ‘Wachina wa Samaki wa Magufuli’, waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya uvuvi haramu katika ukanda wa uchumi wa bahari ya Tanzania, inatarajia kwenda Mahakama ya Kimataifa ya Bahari kuwasilisha malalamiko yao kama hukumu yao haitatekelezeka, imefahamika.

Miongoni mwa malalamiko hayo ni kutaka kujua hatima ya madai yao ya meli ya Tawariq 1 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 2.3 na samaki waliokutwa kwenye meli hiyo wakiwa na thamani ya zaidi ya Sh bilioni mbili.

Hatua hiyo imefikiwa kutokana na uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu kwamba suala hilo lirudi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako amri ya kurejeshewa vitu hivyo ilitolewa.

“Tunatarajia kuiandikia barua Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutaka utekelezaji wa hukumu iliyotolewa Agosti mwaka 2014. Katika uamuzi wa Jaji Ama-Isario Munisi, Mahakama Kuu imetutaka kufuata uamuzi wa mahakama hiyo ya chini.

“Tunatakiwa kudai kupitia hukumu ya Mahakama ya Kisutu iliyoamuru baada ya kuwaachia huru washtakiwa kwamba warejeshewe hati zao za kusafiria, meli na samaki.

“Tumetoa nafasi ya kutosha kwa Serikali kujifikiria   ijue italipaje mali hizo, muda wote huo hatukuweza kupeleka madai hayo nje kwa sababu ya uzalendo, tumezingatia uchumi wa nchi pia.

“Muda unavyozidi kwenda madai hayo yanaongezeka, hiyo ni tathmini ya awali iliyofanywa zaidi ya miaka 10 iliyopita, meli si ya Wachina, meli ni ya wanahisa wa Tawariq 1.

“Watu wengi walichangishana fedha wakanunua meli, hawataki utani na fedha zao, endapo hatutapata uamuzi wa wateja wetu kulipwa, tutapeleka hukumu zote Mahakama ya Kimataifa ya Bahari.

“Hayo ni maagizo ya wateja wetu, kwamba hukumu isipotekelezwa tulipeleke suala hilo nje,” alisema mmoja wa mawakili hao wa wadai.

Kwa mujibu wa wakili huyo, katika mahakama hiyo ya nje, gharama nyingi zitaongezeka na Serikali itaanza kudaiwa kwa siku zote ambazo meli hiyo ilikuwa haifanyi kazi kwa sababu ilipokuwa ikifanya kazi ilikuwa inaingiza fedha kila siku.

“Serikali itadaiwa fedha za mikataba ya mabaharia na wafanyakazi wote, malipo ya mawakili, ndugu wa mtuhumiwa aliyefariki dunia watadai fidia na gharama za kesi nje,” alisema.

 

WALIVYOKAMATWA

Wachina hao, walikamatwa mwaka 2009 na boti ya askari wa doria wa Tanzania walioshirikiana na askari wa Afrika Kusini na Botswana. Leseni waliyokuwa nayo ilikuwa imemaliza muda wake Desemba mosi, mwaka 2008.

Waliachiwa na Mahakama ya Rufaa Machi 28, 2014, lakini walikamatwa tena na kushtakiwa upya kwa mashtaka hayo hayo yaliyofutwa.

Agosti mwaka 2014, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliwaachia huru na kuamuru Jamhuri iwarejeshee mali zao, ikiwamo meli ya Tawariq 1.

Septemba mosi, mwaka 2014, wadai waliwasilisha barua mbele ya Msajili wa Mahakama hiyo wakiomba mahakama iwarejeshee vielelezo vilivyotolewa mahakamani wakati kesi namba 38 ya mwaka 2009 mbele ya Jaji Radhia Sheikh, iliposikilizwa.

Barua hiyo ilivitaja vielelezo hivyo kuwa ni Meli ya Uvuvi ya Tawariq 1 pamoja na Sh 2, 074,249,000 za tani 296.3 za samaki walizokutwa nazo raia hao ambavyo vilitolewa Oktoba mosi, mwaka 2009 mbele ya Jaji Radhia.

 

Mahakama Kuu

Uamuzi wa kuwataka wadai kudai utekelezaji wa hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ulitolewa na Jaji Munisi kutokana na hoja za Jamhuri.

Wakili wa Serikali Mkuu, Timony Vitalis katika hoja za pingamizi mwishoni mwa mwaka jana, alidai Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, isingeweza kusikiliza maombi ya ‘Wachina wa Samaki wa Magufuli‘ wanaotaka kurejeshewa meli iliyozama na samaki kwa sababu amri ya kurejeshewa ilitolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Upande huo wa Jamhuri ulidai mwombaji katika maombi hayo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Tawariq, Said Mohammed, hakuwa na sifa ya kukabidhiwa mali hiyo, hivyo uliomba mahakama itupilie mbali maombi ya kutaka kurejeshwa meli hiyo na zaidi ya Sh bilioni mbili za tani 296.3 za samaki.

Maombi hayo yalitokana na kesi iliyokuwa inawakabili nahodha wa meli, Hsu Chin Tai na Wakala wa Meli ya Tawariq 1, Zhao Hanquing.

Wakili Vitalis alidai haiwezekani maombi hayo yapelekwe Mahakama Kuu kwa sababu Mahakama ya Kisutu ilikwisha kuamuru mali akabidhiwe mshtakiwa wa kwanza aliyekuwa kapteni wa meli hiyo.

Alidai Mahakama ya Rufaa ilikwisha kufuta mwenendo wa kesi ya msingi wa Mahakama Kuu, hivyo maombi hayo yalikuwa batili na yasingeweza kusikilizwa na kutolewa amri mbili katika mahakama mbili kuhusu kitu kimoja.

Wakili huyo alidai kwamba mahakama hiyo isingeweza kuamuru mkurugenzi huyo kurejeshewa mali wanazodaiwa kwa kuwa si kampuni yake.

Jamhuri ilidai kama wadai walikuwa na hoja waziwasilishe katika mahakama iliyotoa amri hiyo ambayo ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mdai katika maombi hayo alikuwa ni mwajiri wa Wachina hao, Said Mohammed ambaye anawakilishwa na mawakili Kapteni Ibrahim Bendera na John Mapinduzi.

Mawakili hao walifungua kesi hiyo kwa hati ya dharura dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), wakidai fidia ya meli ya Tawariq 1 na Sh bilioni 2.074 ambazo ni gharama za samaki zilizofanyiwa uthamini Oktoba mosi, 2009.

Meli hiyo ilifanyiwa uthamini mwaka 2008 na kuonyesha thamani yake ni Dola za Marekani milioni 2.3. Ripoti hiyo ilitolewa na Kampuni ya Cambodia Shipping Services Ltd.

Akijibu hoja za Jamhuri, Kapteni Bendera alidai waliwasilisha maombi hayo mahakamani hapo kwa sababu Mahakama ya Kisutu ilikataa kurejesha mali hizo kwa mshtakiwa wa kwanza.

Kapteni Bendera alidai waliwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu kwa sababu vielelezo vilitolewa katika mahakama hiyo wakati wa kusikilizwa kesi ya msingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles