Na HARRIETHÂ MANDARI- GEITA
WACHIMBAJI wadogo wa Kitongoji cha Nyakafulu wilayani Mbogwe, wamejitolea kuanza ujenzi wa nyumba za watumishi ili kuondoa adha kwa watoa huduma za afya kusafiri mwendo wa kilomita 10.
Ujenzi huo wa nyumba mbili za watoa huduma ni moja ya mradi ambao upo kwenye miradi sita yenye gharama ya zaidi ya Sh milioni 200.
Miradi mingine ni ujenzi wa madarasa, ofisi ya mtendaji na ukarabati wa zahanati.
Zahanati ya Nyakafulu iliyopo katika Kata ya Nyakafulu Wilaya ya Mbongwe mkoani Geita, inakabiliwa na changamoto ya nyumba za watumishi ambapo huwalazimu watumishi hao kuchelewa kutoa huduma kila siku.
Akifafanua juu ya changamoto hiyo, Mtendaji wa kata hiyo, Ezekiel Shedrak, alisema wagonjwa hupata usumbufu hasa nyakati za usiku wanapokuja kutibiwa ikiwemo wajawazito kujifungulia koridoni.