26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wachimbaji madini Bulumbaka wazidi kuvutana

Na Derick Milton, Simiyu

Baada ya watu waliojiita wamiliki wa mashamba katika Mgodi wa Bulambaka ulioko Wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu, kuandamana wakimkataa mwekezaji aliyepewa leseni ya uchimbaji katika mgodi huo, wamiliki wa maduara kwenye mgodi huo wamemuomba Waziri kuingilia mgogoro huo.

Wakiwa kwenye Ofisi za Madini mkoani, wamiliki hao wa maduara walisema kuwa waliamua kufika kwenye ofisi hizo kwa ajili ya kutafuta suruhisho la mgogoro huo ambao umesababisha shughuli za uchimbaji kusitishwa.

Wamiliki hao wamesema kuwa mbali na hilo, hali ya amani imepotea kwenye mgodi huo, kwa madai kuwa viongozi wa vijiji wamekuwa wakisababisha vurugu na kuhamasisha wananchi wananchi kuzuia shughuli za uchimbaji zisendelee.

“Viongozi wa kijiji ambacho ndiyo kuna mgodi, wakiongozwa na mwenyekiti wa kijiji hicho, wamekuwa wakihasisha wananchi kufanya vurugu kwa kile kinachodaiwa hawamtaki mwekezaji aliyepewa leseni,” alisema Juma Thabiti.

Naye Nzige Mayuma mmiliki wa duara katika mgodi huo, amesema kuwa wao kama wamiliki wa maduara hawana tatizo na mwekezaji aliyepewa leseni, kwani mgodi umefikia hatua ya kuhitaji mwekezaji ambaye atawasaidia huduma mbalimbali.

“Kwa hali ambayo mgodi umefikia unahitaji mwekezaji, sisi hatuna nguvu tena ya kifedha ya kuwezesha baadhi ya huduma kuwepo, kuna baadhi ya vifaa vya uchimbaji vina gharama kubwa mwenye uwezo wa kuvileta ni mwekezaji,” alisema Nzige.

Wamiliki hao walidai kuwa wananchi ambao walifanya maandamano kwenda ofisini kwa mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa na kujiita ndiyo wamiliki wa mashamba siyo wamiliki wa mashamba na hawana mashamba bali walichochewa na mwenyekiti huyo.

“Hao ambao walifanya maandamano siyo wamiliki wa mashamba kama walivyojitambulisha, ni wananchi tu ambao walichochewa na huyo mwenyekiti, amekuwa tatizo sana, amekuwa na nguvu zaidi ya serikali, shughuli zote zimesimama mpaka sasa,” alisema Faksoni Sali.

Wachimbaji hao wamemuomba Waziri wa Madini kuingilia kati mgogoro huo ambao umekuwepo kwa muda mrefu, kwani shughuli zimesimama na wao hawana pesa na tegemeo lao ni madini katika kuendesha maisha.

“Shughuli za madini zikitaka kuendelea huyu mwenyekiti na wananchi wake wamekuwa wakizuia, tunaiomba serikali, hasa Waziri wa Madini atusaidie ili jambo limalizike,” Alisema Sali.

Hussen Makubi ni Makamu Mwenyekiti wa kikundi kilichopewa Leseni BULUWADU 4 MINE, alisema kuwa katika mgodi huo shughuli zote zimesimama na kuiomba Wizara kutafuta suruhisho la mgogoro huo kwani wao wamefuata sheria na taratibu za kupata leseni.

Ofisa Madini Mkoa Joseph Kumburu alipotafutwa kuelezea mgomgoro huo, alisema kuwa ofisi yake haina majibu yeyote, bali wenye majibu ni viongozi wa Wilaya na mkoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles