MOHAMED KASSARA NA CALVIN MINJA, DAR ES SALAAM
Kocha mkuu wa timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’, Emmanuel Amunike, amewapiga chini katika kikosi hicho wachezaji sita wa Simba pamoja na kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’, baada ya kugoma kuingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za Mataifa Afrika (Afcon) mwakani dhidi ya Uganda ‘The Cranes’.
Stars inatarajia kushuka dimbani kuikabili The Cranes katika mchezo utakaochezwa Septemba 8, mwaka huu Uwanja wa Nelson Mandela jijini Kampala.
Hivi karibuni, Amunike alitangaza kikosi cha wachezaji 25, kwa ajili ya mchezo huo huku wachezaji saba kati yao wakitokea katika kikosi cha Simba.
Wachezaji waliotemwa ni Shomari Kapombe, Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Shiza Kichuya, Hassan Dilunga na John Bocco.
Mchezaji pekee wa Wekundu hao aliyesalia katika kikosi cha Stars ni kipa, Aishi Manula, aliyejumuika kambini juzi.
Hata hivyo, kocha huyo raia wa Nigeria amewaita wachezaji wengine sita ili kuziba nafasi za wachezaji aliowaengua.
Wachezaji hao ni Paul Ngalema (Lipuli), Salumu Kimenya (Prisons), David Mwantika, Frank Damayo (Azam FC) na Salum Kihimbwa na Kelvin Sabato kutoka Mtibwa Sugar.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidau, alisema Amunike amefikia uamuzi wa kutema wachezaji hao baada ya kushindwa kuwasili kambini katika muda waliopangiwa.
“Wachezaji hao wameshindwa kujiunga na wenzao kambini katika muda waliotakiwa, hivyo kocha ameamua kuachana nao na kuita wengine ili kuziba nafasi zao.
“Kocha alitaka kupata muda wa kutosha wa kukiandaa kikosi chake kwa mchezo huo ndiyo maana tukaahirisha mechi za ligi za Azam, Simba na Yanga.
“Wachezaji wote wanaocheza ligi ya ndani walikuwa wameripoti kambini tangu juzi, isipokuwa wachezaji wa Simba na Azam ambao wao walitakiwa kuripoti baada ya michezo dhidi ya Mbeya City na Ndanda FC,” alisema.
Kidau alisema baada ya kuona wachezaji hao wameshindwa kuripoti kama walivyotakiwa, walifanya mazungumzo na uongozi wa Simba, lakini jitihada za kuwapata zilishindikana.
“Tulijaribu kuongea na Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, ambaye alimwagiza meneja wa timu hiyo kuhakikisha wachezaji hao wanaungana na wenzao haraka iwezekavyo, kocha alitoa muda hadi leo saa 12 asubuhi (jana) wawe wamewasili, hata hivyo hakutekeleza wito huo,” alisema Kidau.
Hata hivyo taarifa nyingine iliyotolewa jana jioni na Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo ilieleza kuwa Fei toto ameenguliwa katika kikosi cha timu hiyo.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikuweka wazi sababu zilizosababisha kiungo huyo kuondolewa katika kikosi cha Stars.