26 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Wachezaji Ligi Kuu kupimwa corona

ASHA KIGUNDULA – DAR ES SALAAM

BODI ya Ligi(TPLB),imesema itahakikisha wachezaji wote wanafanyiwa uchunguzi wa maambulizi ya virusi vya corona kabla kushiriki Ligi Kuu Tanzania(VPL), Ligi Daraja la Kwanza(FDL) na Ligi Daraja la Pili(SDL).

Bodi ya Ligi imetoa msimamo huo baada ya watendaji wake kukutana jana kujadili mustakabali wa ligi hizo.

Ligi hizo zimesimama kutii agizo lililotolea juzi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambaye alitangaza uamuzi wa serikali kupiga marufuku kwa siku 20, shughuli zinazosababisha mikusanyiko ikiwemo michezo, ikiwa ni tahadhari ya kuepuka kusambaa virusi vya corona. 

Jumanne wiki hii, Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alitangaza kugundulika kwa mgonjwa mwenye maambulizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa corona.

Ugonjwa wa corona ambayo kwa sasa umesambaa maeneo mbalimbali duniani, ulianzia China.

Tayari umesababisha vifo vya maelfu ya watu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mtendaji Mkuu wa TPBL, Almas Kasongo alisema, licha ya wachezaji kufanyiwa uchunguzi, michezo iliyosalia ya ligi hizo msimu huu itachezwa bila mashabiki kama tahadhari ya ugonjwa wa corona.
Bodi ya Ligi inatii agizo la serikali kwa kusimamisha michezo yote tunayoisimamia kwa pamoja na TFF ambayo ni Ligi Kuu, ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili na Ligi za Mikoa pamoja na mashindano mengine,”alisema Kasongo.

Alisema wataendelea kuzuia kutofanyika kwa mashindano yoyote yaliyo chini yao wakati wote wa marufuku ya Serikali.

Alisema kwa upande wa Ligi Kuu imesaliwa na michezo nane,  Ligi Daraja la Kwanza michezo minne na  Ligi Daraja la Pili mchezo mmoja kwa kila timu, wakati kwa ligi za mikoa ndiyo zilikuwa zinaanza.

 “Kama Serikali itakuwa imeridhia kwa mwezi huo mmoja shughuli mbalimbali ziendelee, wachezaji watapimwa kabla ya kumalizia mechi zilizobaki ambazo sio nyingi, hata hivyo mechi zilizobaki zitachezwa bila ya kuwa na mashabiki ,”alisema Kassongo. 

Alisema uamuzi wao wa kuchezwa mechi bila mashabiki una lengo lile lile la kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa corona ambao umekuwa tishio katika kila kona ya dunia.

Kassongo alisema Serikali ikitangaza kuruhusu ligi hizo ziendelee, matarajia yao zihitimishe Juni mwaka huu, ili timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa ziweze kufanya usajili na kutuma majina Shirikisho la Soka Afrika(Caf).

 “Tumejielekeza ligi yetu iishe ndani ya mwezi wa sita, ili timu zitakazoshiriki michuano ya kimataifa ziweze kusajili na  kuwasilisha majina Caf,”alisema Kassongo.

Ligi mbalimbali maarufu duniani za soka pia zimesimama kutokana na tishio la corona, miongoni mwao ni Ligi Kuu Italia maarufu Serie A, Ligi Kuu England inayofahamika pia EPL na Ligi Kuu Hispania, La Liga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles