26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

WABUNGE WAHOJI UTEKELEZAJI WA BAJETI

 

 

Na RAMADHAN HASSAN, DODOMA


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, imehoji hatua ya utekezaji wa bajeti ya serikali katika miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019.

Imehoji pia mikakati na kazi za Wizara ya Fedha katika kuweka mipango kwenye bajeti zijazo.

Wakichangia kwenye semina ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Bajeti na Kilimo iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), baadhi ya wabunge hao walisema ni vema kuwa na mipango ya muda mrefu ambayo itakuwa dira kwa watendaji kwenye utekelezaji wake.

Akichangia katika semina hiyo, Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza (CCM), alisema kuna baadhi ya miradi, licha ya kupangwa kwenye bajeti bado kumekuwa na changamoto kwenye utekezaji wake.

“Mpango wa bajeti kwa muda mrefu hasa kwenye masuala ya afya na kilimo inachukua asilimia ndogo sana, nataka kujua bajeti ya serikali inalenga nini na sisi katika utekelezaji, hayo maazimio tunayafuata kiasi gani,” alihoji Njeza.

Naye mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), alishauri Wizara  Fedha na Mipango, kutafuta njia  mbadala ya kupanga vizuri mapato ya ndani ili kuepuka utegemezi.

Change amekishauri kitengo cha mipango kufanya tathmini ya kina katika kuweka vipaumbele.

“Changamoto ya mapato ya ndani kutopatikana kwa wakati imekuwa ikijitokeza mara kwa mara hivyo inabidi tuhakikishe tunatafuta mbadala ili kuepuka mambo kama hayo yasijitokeze tena,” alisema Chenge.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia aliitaka wizara hiyo kuja na majibu ya chombo ambacho huwa kinafanya kazi ya kuandaa mipango.

Awali, akiwasilisha mada kwenye semina hiyo, Kamishna Msaidizi wa Bajeti kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Charles Mwamwaja alisema ili kutatua changamoto za utekelezaji wa bajeti, lazima uwepo ushirikishwaji tangu awali katika ngazi zote na kupitia kamati mbalimbali za Bunge.

Alisema bado kuna changamoto kwenye utekelezaji wa bajeti kwa sababu mahitaji mengi hayawiana na mapato.

Alisema jambo la kushangaza ni wakati wa uchambuaji bajeti, wahusika wanaona ni ya msingi lakini mapato hayaoneshi jambo ambalo alieleza kuwapo haja ya kufanya kazi ya ziada.

“Changamoto nyingine ni mapato ya ndani na nje kutopatikana kwa wakati jambo ambalo linaathiri utekelezaji wa bajeti mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwekeza vya kutosha kwenye sekta binafsi ili tufanikiwe kutekeleza bajeti,” alisema.

Akizungumzia namna ya kupunguza changamoto hizo, Dk Mwamwaja alisema kwa sasa inabidi kuwianisha mahitaji ya serikali na mapato na kuwa na mikakati ya kuimarisha upatikanaji wa mapato ya ndani na kupunguza utegemezi.

Alisema nchi inatakiwa kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kujenga uchumi wa kati.

“Hili linatakiwa kuanza ushirikishwaji wa kamati za bunge katika ngazi za awali. Ili kama kuna changamoto hususani katika ukusanyaji wa mapato zitatuliwe mapema,” alisema.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles