26.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge vijana wafundwa kuhusu ajira majimboni

Patrick Kihenzile
Patrick Kihenzile

NA MAREGESI PAUL,DODOMA

WABUNGE vijana nchini, wametakiwa kuwa na takwimu za vijana wasiokuwa na ajira katika majimbo yao.

Ushauri huo ulitolewa mjini hapa jana na mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Uchumi na Kijamii (ESRF), Patrick Kihenzile, alipokuwa akizungumza katika semina ya wabunge vijana iliyofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Katika maelezo yake, Kihenzile alisema kama wabunge hao watakuwa na takwimu hizo, zitawasaidia kujua idadi ya vijana wanaohitaji msaada na kuangalia namna ya kuwasaidia kwa urahisi, tofauti na ilivyo sasa ambapo takwimu hizo hazijulikani.

“Sehemu kubwa ya Watanzania ni vijana na wengi hao hawana ajira za uhakika. Kwa hiyo, nawashauri wabunge vijana muwe na ‘data base’ ya vijana wasiokuwa na ajira katika majimbo yenu kwani mkijua idadi yao, itakuwa rahisi kuwasaidia,” alisema Kihenzile.

Naye Mbunge wa Serengeti, Chacha Mwita (Chadema), alisema vijana wengi wanashindwa kujiingiza katika siasa kwa kuwa hawana fedha za kuweza kushindana na wanasiasa wengine wenye fedha.

“Katika nchi hii, vijana wengi hawana fedha na wanakuwa na wakati mgumu sana pindi wanapotaka kujiingiza katika siasa.

“Kwa mfano, mimi hapa ni mwalimu, nimefanikiwa kuwa mbunge kutokana na hisani tu, yaani ni vigumu sana kushinda siasa wakati huna fedha.

“Kwa hiyo, nashauri Serikali iliangalie hili kwani linarudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa,” alisema Mwita.

Kwa upande wao, Mbunge wa Viti Maalumu, Agness Marwa (CCM) na Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Msabaha (Chadema), waliwataka vijana nchini kwa nyakati tofauti wawe na umoja na washirikiane kila wanapotakiwa kufanya hivyo.

Pamoja na hayo, walilalamikia muundo wa elimu ya Tanzania kwa kile walichosema elimu hiyo haiwaandai vijana kujiajiri na badala yake inawaandaa kuajiriwa serikalini jambo ambalo haliwasadii kimaisha.

Awali, Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge hao Vijana, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza (Chadema), alisema umoja huo ni muhimu kwao kwa kuwa unawaweka pamoja na kuwafanya washirikiane katika masuala mbalimbali ingawa wanatoka katika vyama tofauti tofauti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles