24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge, Butiku wataka haki Zanzibar

Dk. Ashatu KijajiElias Msuya, Dodoma na Tunu Nassor, Dar

MGOGORO wa uchaguzi wa Rais wa  Zanzibar, jana uliibuka katika mjadala wa mapendekezo ya mwelekeo wa mpango wa maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 ambako baadhi ya wabunge wa upinzani walisema hauwezi kutekelezeka ikiwa amani haitapatikana.

Akisoma mapendekezo ya mpango huo, Naibu Waziri wa Fedha, Dk. Ashatu Kijaji, alisema una lengo la kutekeleza mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano (2016/17-2020/21) na mpango elekezi wa miaka 15.

Alitaja vipaumbele vya mpango huo kuwa ni viwanda vya kuimarisha kasi ya ukuaji wa uchumi, miradi mikubwa ya kielelezo ya kuwezesha uchumi kupaa, miradi inayoendelea hususan maeneo wezeshi kama barabara, reli, bandari, maji na mawasiliano kwa maendeleo ya viwanda na maeneo yatakayolenga kufungamanisha maendeleo ya viwanda na maendeleo ya watu.

Lakini akichangia mjadala huo, Mwenyekiti wa Chadema ambaye ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, alisema mpango huo hauwezi kutekelezwa kutokana na sintofahamu ya amani na hasa mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar.

“Tunapozungumzia mipango ya maendeleo kama hii, lazima kuwe na mazingira mahsusi ya kufanikisha. Mipango yote bila kuwa na amani, hakuna mwekezaji atakuja kuwekeza. Hivi sasa kuna yanayoendelea Zanzibar halafu tunazungumzia maendeleo…” alisema Mbowe.

Mbowe pia  aliukosoa mpango huo akisema haukuwashirikisha wadau mahususi hasa wananchi.

“Mipango yetu ya nchi bado inapangwa kijamaa, inapangwa Dar es Salaam, tunafikiri Tanzania yote iko huko… tunawashirikisha wananchi katika mipango ya maendeleo?

Naye Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea, alisema suala la Zanzibar litaathiri uchumi wa nchi.

“Tuzungumze masuala ya uchumi siyo siasa. Bajeti yetu inategemea misaada ya wahisani. Kinachoendelea Zanzibar kinatutia doa na kitakimbiza  wahisani,” alisema Mtolea.

Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Ngwali (CUF), alisema kuzungumzia maendeleo bila kuwa na amani ni sawa na kujenga nyumba kwa matofali ya barafu.

“Kuna msemo wa Kiswahili unaosema; ‘unaweza kujenga nyumba ya ghorofa kwa kutumia matofali ya barafu’. Tunazungumzia amani wakati msingi wa amani na utawala bora haupo,” alisema Ngwali.

Alizungumzia pia suala la takwimu, alisema hakuna uhalisia.

“Takwimu zinazotolewa kwenye mpango hazina uhalisia, kwa mfano, tuna bandari na tumezungukwa na nchi zisizo na bahari lakini tumejiwekea lengo la kukua kwa asilimia tisa?” alihoji.

Baadhi ya wabunge hasa wanaotoka mikoa ya Kigoma na Tabora, walizungumzia kudorora kwa usafiri wa reli na kusema kuwa utadhoofisha utekelezaji wa mpango huo.

Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko (CCM), alisema mpango huo hauwezi kukamilika kama Serikali haitaboresha ujenzi wa reli wenye viwango.

“Nchi za Kenya na Uganda tayari wamejenga reli ya ‘standard gauge’, Tanzania haina reli. Utazungumziaje maendeleo ya viwanda wakati hakuna reli,” alihoji Nsanzugwanko.

Mbunge wa Urambo Mashariki, Margaret Sitta (CCM), alisema kilimo hakiwezi kuendelea kama hakutakuwa na usafirishwaji wa mazao ya wakulima kwa njia ya reli.

“Naungana na Nsanzugwanko na Sakaya kuhusu ujenzi wa reli. Kwa sasa tunayo reli ya kati, lazima ijengwe kwa standard gauge ili tuwe na uwezo wa kubeba tani 450 kwa wakati mmoja. Kenya wameshaanza na wametupita,” alisema Sitta.

Kuhusu kilimo, alisema mpango huo haujaainisha mazao makuu ya biashara kama vile chai, kahawa, tumbaku na jinsi ya kuwakwamua wakulima kwa matatizo ya masoko.

“Kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaoingia vyuo vikuu, lakini mpango unasema wanaokwenda kwenye elimu ya ufundi ni 50,000 tu kwa mwaka, tunakwendaje kwenye uchumi wa viwanda?” alihoji Sitta.

Baadhi ya wabunge pia walikosoa takwimu za upatikanaji wa maji wakisema takwimu za mpango huo hazina uhalisia.

Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate (CCM), alisema wakati mpango huo ukionyesha kuwa maji hupatikana kati ya asilimia 68-86 vijijini na asilimia 86 mijini, maeneo mengi maji hayapatikani.

“Takwimu za maji zinaonyesha maji yanapatikana kwa asilimia 68-86 vijijini na asimilia 86 mijini, kule jimboni kwangu yanapatikana kwa asilimia 10. Nilikuwa Dar es Salaam maji hakuna kabisa,” alisema Bilakwate.

Naye Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama alisema:

“Takwimu za maji siyo za kweli, kule jimboni kwangu yanapatikana chini ya asilimia 10. Nadhani walipokuwa wakiandika takwimu hizi hawakuangalia umbali wa maji yanakopatikana hadi kwa wananchi,” alisema.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alisema kuna kuporomoka kwa kasi kwa kilimo jambo linalohatarisha ukuaji wa viwanda.

“Ripoti ya mpango uliopita wa mwaka 2011-2015, unaonyesha kuporomoka kwa kilimo. Ripoti ya Benki ya Dunia inaonyesha jinsi watu wanavyoacha kilimo Tanzania kutoka asilimia 77 hadi 66. Sasa tunakwenda kwenye viwanda, ni lazima Wizara ya Fedha iwekeze kwenye viwanda na mazao ya wakulima,” alisema Bashe.

Akihitimisha mjadala huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema suala la Zanzibar waachiwe Wazanzibari wenyewe wasuluhishane kwani hata nchi wahisani walishagombana wao kwa wao hadi wakafika hapo walipo.

“Hili la Zanzibar kama ni utengamano lazima uanzie kwa wananchi wenyewe. Suala la kuogopa ‘donors’ halisaidii, wao pia walishapigana sana. Wazanzibari wakae wasuluhishane wenyewe,” alisema Dk. Mpango.

Kuhusu uhalisia wa takwimu na maendeleo ya wananchi, Dk. Mpango alisema si kweli ukuaji wa uchumi haufanani na maendeleo ya wananchi.

“Takwimu hizi zinapatikana kutoka ngazi za chini, hivyo kinachofanyika ni uhalisia. Sipendi kuwa mwanasiasa, umeme vijijini hamuuoni, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kiko hapa, Bwawa la Mugumu yote yanatokana na mpango wa maendeleo uliopita,” alisema Dk. Mpango.

 

Butiku asisitiza haki itendeke Zanzibar

 Naye Mkurugenzi  Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku amesisitiza kutendewa haki kila upande katika mazungumzo yanayoendelea kuhusu  mgogoro wa siasa  Zanzibar.

Butiku aliyasema hayo jana alipohojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW)kuhusu mgogoro huo.

“Nasema kwa kusisitiza haki itendeke Zanzibar kwa sababu misingi ya taifa letu tangu uhuru na Mapinduzi Matukufu ni haki, amani na umoja,” alisema Butiku na kuongeza:

“Mimi napenda kuamini kuwa siku ya uchaguzi Wazanzibari waliamua jambo na uamuzi wao ndiyo ambao mpaka sasa hatujapata maelezo ya kutosha kwa nini hapo katikati walisema ulikosewa.

“Nadhani walioamua jambo hilo hawakukosea isipokuwa waliohesabu mpaka kutoa matokeo ndiyo waliokosea “.

Alisema mpaka sasa hawajapata maelezo makosa hayo yalisababishwa na nani? Na kitu gani?  Kwa kuwa  hayakusababishwa na wananchi wa Zanzibar.

“Naamini Wazanzibari wangetendewa haki angalau uamuzi walioufanya ujulikane kwao wote na sisi,” alisema Butiku.

Hata hivyo   alisema ana hakika Rais John Magufuli amezungumza na Wazanzibari na kwa kushirikana pamoja wanaweza kutafuta jibu.

Alisema Zanzibar si ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na CUF peke yao, bali ya Wazanzibari  wote  hivyo anaamini siku ya uchaguzi Wazanzibari walitoka kwa wingi na kwa amani kwenda kupiga kura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles