33.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge 150 wasimama kuhesabiwa kwa Lowassa

EdwardLowassaNa Mwandishi Wetu, Dodoma
WABUNGE 150 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamemwomba Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, muda ukifika achukue fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Kauli hiyo waliitoa juzi mjini hapa katika hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika Kilimani nyumbani kwa kigogo mmoja wa CCM ambaye aliwaalika wabunge wa chama hicho akiwemo Lowassa.
Wakizungumza katika ghafla hiyo wabunge hao walimwelezea Lowassa kuwa ana vigezo vyote vya kuipeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huo.
Aliyekuwa wa kwanza kuzungumza katika hafla hiyo alikuwa Mbunge wa Ngara, Deogratias Ntukamazina (CCM), ambapo alisema wabunge marafiki wa Lowassa wanamwomba agombee nafasi hiyo ya juu ya nchi kutokana na kuwa na sifa na kuwa kiongozi imara na bora.
“Mimi as senior citizen huu ni mwaka muhimu, Oktoba tutakuwa na uchaguzi mkuu wa kumchagua kiongozi atakayeisukuma mbele nchi yetu,” alisema na kuongeza.

“Sote tunafahamu chama chetu bado hakijatangaza taratibu, lakini sisi wabunge marafiki zako tunakuomba muda ukifika chukua fomu kwa sababu unatosha,” alisema.
Ntukamazima alisema sifa kuu za kiongozi ni yule mwenye elimu, maono, uchapakazi, uwezo na tabia nzuri,vitu ambavyo Lowassa anavyo.
“Kule kwangu Ngara wananiuliza yule waziri mkuu aliyeleta hizi shule za kata yuko wapi, mimi nawajibu atarudi na kila mtu mitaani anataja jina lako kwa hiyo sauti ya wengi ni sauti ya mungu,” alisema Ntukamazina.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu, Diana Chilolo (CCM), aliunga mkono kauli ya Ntukamazina na kusema kuwa Lowassa ni chaguo la wengi.

Maji Marefu
Kwa upande wake Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM) alimwelezea Lowassa kuwa ni binadamu mwenye upendo wa hali ya juu.
Ngonyani maarufu kama ‘Profesa Maji Marefu’ alisema yuko tayari kufukuzwa CCM lakini hatoacha kusema ukweli wake wa kile anachokiamini kuhusu Lowassa.
“Huyu mzee mbali ya uwezo mkubwa wa kufanyakazi lakini ana huruma… katika hili nipo tayari kufukuzwa CCM kwa msimamo wangu wa kusema ukweli juu ya kumuunga mkono Lowassa.
“Nasema bila kificho mimi ni mganga wa tiba asilia ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa waganga wote nchini, sisi tutahakikisha tunakuunga mkono ndugu yetu lakini utuhakikishie kama utagombea urais,” alisema Ngonyani
Alisema kitendo cha kumwona Mbunge wa Viti Maalumu, Marry Chatanda katika hafla hiyo ya chakula cha jioni ni ishara ya kudhihirisha kukubalika kwa waziri mkuu huyo wa zamani.
“Nilipoingia kumwona huyu Chatanda yuko hapa! Haa!! Basi…,” alisema Ngonyani.

Marry Chatanda na ugomvi
Chatanda ambaye pia ni Katibu wa CCM, Mkoa wa Singida, alikuwa ni hasimu mkubwa kisiasa wa Lowassa hasa alipokuwa katibu wa chama hicho Mkoa wa Arusha hali iliyofikia kwa viongozi hao kufanyiana vitimbi katika majukwaa ya kisiasa ndani na nje ya CCM.
Hata alipopewa nafasi ya kuzungumza Chatanda alikiri kuwa alikuwa hamuungi mkono Lowassa pamoja na kwamba wanafahamiana kwa muda mrefu ila anaungana na wale wanaomwomba agombee urais.
“Mimi na Edward hatuna ugomvi, wapambe wake ndiyo walikuwa wanatuchonganisha na kwa kweli sikuwa kabisa namuunga mkono.

“…lakini wagombanao ndiyo wapatanao mimi sasa hivi nimeingia mwili mzima kumuunga mkono Edward na hakuna wa kunitoa,” alisema Chatanda huku akishangiliwa na wabunge wenzake.

Komba awaka
Katika hafla hiyo ya chakula cha jioni ya aina yake, Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba (CCM), alimzungumzia Lowassa alivyoshangiliwa katika maadhimisho ya miaka 38 ya CCM mjini Songea.
Alisema baada ya kuingia uwanjani hapo umati wa watu ulilipuka kwa shangwe hali inayoashiria safari njema kwa mwanasiasa huyo.
“Ule umati wa watu ulivyokushangilia pale uwanjani Songea inaonesha kuwa wewe ndiyo chaguo la wengi, sikilizeni niwaambie miye nilikuwepo uwanjani wale wengine wote hawakushangiliwa pamoja na kutegemea mbali na jukwaa ili watu wawaone lakini huyu Lowassa alivyoteremka mbele tu ya jukwaa kuu uwanja mzima ulilipuka,” alisema Komba

Zungu anena
Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu (CCM), alimwelezea Lowassa kama kiongozi shupavu, makini.

Zungu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje inayoongozwa na Lowassa, alisema umakini wa kiongozi huyo umekuwa ukiwafundisha mambo mengi.

Yahya Kassim Issa
“Lowassa ni mwenyekiti wangu katika Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje uwezo wake naujua hata pale tunapobabaisha au kudanganya kidogo, anagundua, kwa kweli tunajifundisha mengi kutoka kwake” alisema mbunge huyo wa Chwaka, Zanzibar (CCM).
Hata hivyo Lowassa bado hajatangaza rasmi nia ya kuwania urais, lakini hata hivyo aliposimama kujibu kauli za wabunge hao, alisema suala la urais ni jambo zito na anamwachia Mungu.
“Ndugu zangu nafarijika sana kwa kauli zenu lakini hili suala la urais ni kubwa, tumuachie huyu aliye juu (Mungu), yeye akiamua liwe linakuwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles