SANAA, YEMEN
WAASI wa Houthi nchini Yemen wamesema watasitisha mashambulizi ya makombora yanayofanywa na ndege zisizo na rubani dhidi ya muungano wa kijeshi unaoongzwa na Saudi Arabia.
Hayo yamekuja huku kukiwa na shinikizo kutoka jumuiya ya kimataifa kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa takriban miaka mine sasa.
Kiongozi wa Houthi, Mohammed al- Houthi alisema iwapo muungano huo wa kijeshi utatafuta kufikiwa kwa amani basi hata kundi lake litanuia kufanya hivyo.
Aliongeza kuwa kusitishwa kwa mashambulizi ni ishara ya nia njema na itaunyima muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kisingizio cha kutofanya mazungumzo ya kutafuta amani na kukomesha mashambulizi ya kuidhibiti Yemen.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen, Martin Grifitths anapanga duru mpya ya mazungumzo ya kutafuta amani nchini Sweden.