Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM
WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona wakati wanapotimiza wajibu wao wa kukusanya habari kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema waandishi wana nafasi kubwa ya kutoa elimu kwa jamii, hivyo ni vyema kuzingatia utoaji wa taarifa sahihi kuhusu corona.
Ummy alisema hayo wakati akipokea msaada wa vifaa kinga, vifaa vya kupima joto la mwili, vipeperushi, mabango na vifaa vya kutoa elimu kwa umma kwa ajili ya waandishi wa habari vilivyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).
Alisema wizara yake imekuwa ikishirikiana na vyombo vya habari kuhakikisha wananchi wanapata taarifa kwa wakati kuhusu corona na kufahamu hatua za kufuata ili wajikinge na ugonjwa huo.
“Msaada huu unagusa wadau muhimu sana kwani hawa ndio wanaotusaidia kupeleka taarifa kwa wananchi. Mmenifurahisha zaidi kuzifikia redio za jamii 34 ambazo zitapata vifaa vya kupima joto la mwili pamoja na vifaa kinga vingine. Redio hizi ni za muhimu sana kwani zinawafikia wananchi wengi waliopo vijijini.
“Kwa upande wa waandishi wa habari, pamoja na majukumu yenu ya kazi za kila siku mnazozifanya, hakikisheni mnatoa taarifa sahihi za corona na siyo habari za kuwatisha wananchi, bali waelimisheni.
“Nanyi hakikisheni mnafuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kujikinga na ugonjwa huu, hii ikiwa ni pamoja na kusimama umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu na mtu wakati mnapotekeleza majukumu yenu,” alisema Ummy.
Akikabidhi vifaa hivyo, mwakilishi mkazi wa Unesco nchini, Tirso Dos Santos, aliipongeza Serikali kwa hatua inazochukua katika kupambana na ugonjwa wa Covid-19.
“Vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za ugonjwa huu kwa wananchi, nasi tumeona tuwape vifaa kinga, mabango na vipeperushi ambavyo vitawasaidia kuufahamu zaidi ugonjwa wa corona na kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi kwa wakati,” alisema Santos.