ASHA BANI -DAR ES SALAAM
BARAZA la Habari Tanzania (MCT), limewataka waandishi wa habari kutoegemea upande wowote wakati wa kuripoti taarifa mbalimbali za uchaguzi.
Pia limewataka kuzingatia weledi wa taaluma yao sambamba na kuandika taarifa zenye usahihi zitakazohabarisha umma.
Hayo yalibainishwa Dar es Salam jana na mwakilishi wa MCT, Paul Maimbo wakati wa majadiliano yaliyofanyika kwa njia ya mtandao yaliyokuwa yakilenga kuangalia athari za Covid-19 kwa waandishi wa habari, vituo vya habari pamoja na mchango wao kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
“Katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ulikuwa na shida kidogo ulipoanza, wakati wa uchaguzi ni wakati ambao vyombo vya habari vinatumika sana, hivyo tunasisitiza waandishi wa habari waandike habari za ukweli, wazingatie ukweli na usawa sambamba na kuzingatia vyanzo vya taarifa, ” alisema Maimbo.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema kipindi cha mlipuko wa janga la virusi vya corona, matukio 25 ya ukiukwaji wa haki za binadamu yameripotiwa.
Alisema miongoni mwa changamoto ambazo waandishi wa habari walikumbana nazo katika kipindi hicho ni kutokuwepo kwa utaratibu mzuri wa upatikanaji wa taarifa zinazohusiana na Covid-19.
Kuhusu uchaguzi, Olengurumwa alisema vyombo vya habari ni wadau wazuri, hivyo vinapaswa kuhakikisha vinafanya kazi kwa weledi bila upendeleo katika kipindi chote.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza, Edwin Soko alisema vyombo vya habari vimefanya kazi ya kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha katika kipindi cha mlipuko wa virusi vya corona, licha ya kukumbana na changamoto mbalimbali.