25.5 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

W/biashara NMB:  Ziara ya Uturuki imetubadili kutoka uuzaji hadi uzalishaji

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

WANACHAMA wa Klabu za Biashara za Benki ya NMB (NMB Business Club), waliotembelea Maonesho ya Biashara, nchini Uturuki, wamerejea nchini, huku wakifichua kwamba ziara hiyo imebadili mbinu, mifumo na falsafa zao kiutendaji na kuwapandisha kutoka daraja la uchuuzi na uuzaji, hadi kuwa wazalishaji wa bidhaa.

Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa tatu kushoto), akisalimiana na Bahati Senga ambaye ni mmoja kati ya wafanyabiashara 15 wanachama wa Klabu za Biashara za benki ya NMB.

Oktoba 17, wafanyabiashara 15 wa klabu hizo waliondoka nchini kwenda Uturuki kwa aziara ya siku tisa – kutembelea Maonesho hayo (Trade Fairs 2022), iliyogharamiwa na NMB, ikifanyika kwa mara ya pili, mwaka huu ikiwa chini ya kaulimbiu isemayo: ‘Tunakufungulia milango ya biashara yako kimataifa.’

Wakizungumza baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wafanyabiashara hao waliishukuru NMB kwa kuwaratibia ziara hiyo na kusema imewaongezea hamasa, mbinu na ‘connections’ zitakazoharakisha kukua kwao kibiashara na wamejifunza namna ya kuwa wazalishaji badala ya waagizaji bidhaa.

Msemaji Mkuu wa wanachama hao, Salvatory Chobaliko, ambaye ni Mkurugenzi wa Kigoma Pharmacy Ltd, alisema kupitia ziara hiyo katika maonesho hayo makubwa, na ile ya kwenye viwanda mbalimbali vya uzalishaji wa bidhaa wanazofungamana nazo, wamejua mbinu za kuharakisha ukuaji kibiashara na kiuchumi.

“Tunaishukuru sana NMB sio tu kwa kufanikisha ziara hii, sambamba na ziara za ndani kwenye viwanda vya nguo, vipodozi, vifaa vya ujenzi, viatu, madawa, usindikaji vyakula na matunda, bali pia kutuunganisha na wafanyabiashara wakubwa na kutubadili kutoka kuwa wachuuzi na waagizaji, hadi kuwa wazalishaji,” alisema.

Chobaliko aliongeza kwa kutoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kuwa mabalozi wema wa yote waliyojifunza katika ziara yao, huku akiwataka kuitumia kubadilika zaidi na kukuza mitaji na mapato yao na kuchangia uharaka wa ukuaji wa uchumi wa taifa, huku akiiomba NMB kuendelea kusapoti wafanyabiashara nchini.

Naye Bahati Senga, ambaye mmoja wa waliotembelea maonesho hayo akiwa pia ni Mkurugenzi wa Bahati Fashion Shop, alikiri kufurahishwa na ziara hiyo katika miji ya Istanbul, Sakarya na Bursa, walikoshiriki mikutano na Wanachama wa Umoja wa Wafanyabiashara (Chamber of Commerce) za miji hiyo.

“Ilikuwa ni ziara iliyotuwezesha kujifunza mambo mengi, kupitia maonesho, ziara kwenye viwanda na mikutano yetu na wafanyabiasahara wakubwa na wenye viwanda. Tumejifunza utengenezaji na uzalishaji wa bidhaa, na tunakuja kuvitumia kubadili bishara zetu na kufungua fursa za ajira kwa Watanzania,” alisema Senga.

Meneja Mwandamizi wa Idara ya Biashara NMB, Theresia Mayanie, ambaye alikuwa mmoja wa viongozi wa benki hiyo aliyeambatana na wafanyabiashara hao, alibainisha kuwa malengo ya ziara yao yamefanikiwa na kwamba wanaamini italeta mabadiliko makubwa kwenye biashara za wateja wao hao na kueleza utayari wa benki kuwasaidia.

“Madhumuni ya ziara hii yalikuwa ni kutembelea maonesho hayo, lakini pia ziara za ndani viwandani na kwenye masoko makubwa. Imekuwa ya mafanikio kwa sababu imewawezesha pia kushiriki mikutano mikubwa na Chemba za Wafanyabiashara, mikutano ya Biashara kwa Biashara (B2B) na kupanua mtandao wa biashara zao.

“Kundi hili la wafanyabiashara walipata nafasi ya kutembelea viwanda vyao na kujifunza namna ya kuzalisha, kuuza na kupata ujuzi ambao utawasaidia kuongeza tija katika biashara zao sasa, kwani waliingia makubaliano mbalimbali ya ubia, mambo ambayo tunaamini yanaenda kunyanyua mitaji na pato lao kwa ujumla,” alisema Mayanie.

Hii ni mara ya pili kwa NMB kuratibu ziara ya aina hiyo, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2019, ambako wafanyabiasahara 10 waliotembelea na Maonesho ya 125 ya Canton Fair 2019, yaliyofanyika mjini Guangzhou, China, kabla ya janga la corona kukwamisha safari hizo miaka miwili ya 2020 na 2021.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles