24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Vipande vya Mfuko wa Faida Fund vyaanza kuuzwa, Serikali yapongeza

*Yasema itasaidia Watanzania wengi kujikwamua kiuchumi

*Yasisitiza ni sehemu salama ya wananchi kuwekeza fedha zao

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Serikali imeipongeza Kampuni ya Nyumba ya Watumishi Housing Investment(WHI) kwa kuanzisha Mfuko wa Uwekezaji wa Faida Fund nakwamba kwa kufanya hivyo utawezesha Watanzania wengi kujikwamua kiuchumi.

Pongezi hizo zimetolewa Dar es Salaam Jumanne Novemba 1, mwaka huu na Naibu Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi wakati akifungua mauzo ya vipande vya Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja wa Faida Fund ambao uko chini ta WHI.

“Niwapongeze Watumishi Housing Investment kwa ubunifu wenu na nia njema ya kuhakikisha Watanzania wanaendelea kuwezeshwa kiuchumi kupitia huduma mnazozitoa. mmekuwa mkiwawezesha wananchi kupitia ujenzi wa nyumba ambazo bei zake zimethibitika kuwa nafuu kwa kati ya asilimia 10 hadi 30 ukilinganisha na nyumba zingine za aina hiyo katika soko.

“Na sasa mmebuni na kuanzisha mfuko wa Faida Fund na lengo likiwa ni kuwawezesha Watanzania ili wazidi kujikwamua kiuchumi kupitia uwekezaji wa pamoja, napongeza juhudi hizi na nawahakikishia kuwa Serikali ya Awwamu ya sita itaendelea kuwaunga mkono katika juhudi zenu.

“Kwani sote tunafahamu kuwa watu wengi ambao wamekuwa na hamu ya kuwekeza wamekuwa wakiingia katika uwekezaji wa upatu ambao ni wa kitapeli, lakini kwa hili la Faida Fund ni wazi kuw wananchi wataweza kuwekeza na faida yao itarudi kwani pia wanaweza kufuatilia uwekezaji wao,” amesema Ndejembi.

Aidha, Naibu Waziri huyo amewatoa hofu Watanzania kwa kusema kwamba mfuko huo ni wa uhakika na kwamba Watanzania wajitokeze kuwekeza na faida zake wataziona.

“Mfuko huu ni wa uhakika, hivyo watu wawekeze na matunda yake wataiona, kwani huu unatoa fursa kubwa kwa watumishi wa umma na makundi mengine yanayofanyakazi katika sekta isiyo rasmi kuweza kuwekeza fedha zao.

“Haya yote yanatekelezwa chini ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuona Watanzania wakiumizwa na uwekezaji wa upatu. Ushiriki wa benk ikiwamo CRDB ni wazi kuwa kila mmoja ataweza kufikiwa na uwekezaji huu.

“Hivyo niendelee kuwahimiza Watanzania wa makundi yote ndani na nje ya nchi, watumishi wa umma, sekta binafsi, wafanyabiashara ndogondogo, bodaboda na wengine kuwekeza katika mfuko huu ambao ni salama kwani unasimamiwa na serikali,” amesema Ndejembi.

Akizungumzia miradi ya nyumba ya WHI amesema kuwa imesaidia Watanzania wengi kupata makazi yaliyobora katika maeneo ambayo awali hawakuyatarajia huku akitolea mfano mradi wa Magomeni jijini Dar es Salaam.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Nyumba ya Watumishi Haousing Investment(WHI), Dk. Fredy Msemwa akizungumza katika hafla hiyo.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa WHI, Dk. Fredy Msemwa alisema wanakuja kuongeza urahisi wa huduma hizo kwa wale ambao walikuwa hawapati mwanya wa kuwekeza kutokana na uwezo wa kifedha.

“Sisi kupitia Faida Fund tunakuja kuongezea urahisi wa huduma hizi na tunakuja kuwafikia wale ambao walikuwa hawajafikiwa kama tulivyofanya kwenye nyumba ambapo kulikuwa na makundi ambayo yalikuwa hayajafikiwa.

“Tunatambua kwamba kuna Watanzania wa kawaida ambao walikuwa wanashindwa kuwekeza sababu ya nguvu hafifu ya kumudi kuwekeza katika mifuko iliyotangulia.

“Mfuko wa Faida Fund utakuwa ni mkombozi kwa Watanzania wa kawaida wakiwamo wakulima, mama lishe, bodaboda na wengine, kwa hiyo tunaimani kubwa na Faida Fund katika kuwawezesha watanzania kiuchumi.

“Bado kuna ombwe la huduma za kifedha kwani taasisi kama hizi hapa nchini zipo mbili tu huku kwa majirani zetu zikiwepo takribani 8, kwa hiyo mbali na mambo mengine itasaidia kutoa ajira kwa Watanzania wenzetu wakiwamo vijana, hivyo niseme kwamba kuna fursa kubwa,” amesema Dk. Msemwa.

Amesema ndoto ya Taasisi hiyo anayoiongoza kwa takribani miaka nane sasa ni kuhakikisha kuwa siku moja Watanzania wanakuwa na makazi bora na uhuru wa kifedha.

“Kwa miaka nane nyuma hadi leo tumewezesha familia 900 ambazo zinaishi katika nyumba bora na tunachojivunia hii leo ni kwamba mtu anaweza akanunua nyumba kwa mshahara wake jambo ambalo awali halikuwezekana.

“Ukipita magomeni leo kuna familia 88 ambazo zinaishi zikiwamo za wahudumu wa afya, walimu na kada nyingjne. Na sasa tunataka Watanzania wenzetu wawe na uhuru wa kifedha, hivyo mfumo huu wa Faida Fund utawawezesha wenzetu kuwekeza fedha zao kwa njia ya vipande na kupata uhuru wa kumiliki nyumba na malengo yao mengine.

“Kwa hiyo Faida Fund inakuja kuziba baadhi ya mapengo yaliyopo kwenye uwekezaji wa mifuko, kwani sisi siyo wa kwanza, kuna taasisi zilizotangulia ambazo tutaendelea kichukua mazuri yanayofanywa na watangulizi wetu lengo likiwa ki kiimarisha mfuko huu,” amesema Dk. Msemwa.

Akizungumzia ufunguzi huo wa uuzaji wa vipande amesema kuwa utaendelea kwa siku 60 na baada ya hapo daftari liyafungwa kwa ajili ya ukaguzi na kisha mauzo yataendelea Januari 2023, pia zoezi litafungwa baada ya miezi mitatu na kisha mauzo yatakuwa endelevu.

Amesema mfuko huo rasmi unatarajiwa kuzinduliwa Januari 14, mwakani ukiwa na mwelekeo wa mauzo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Watumishi Haousing Investment(WHI), CPA. Oseah Kasimba akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya WHI, CPA. Oseah Kashimba amesema leo ni siku ya fursa kwa kuanza kwa mfuko wa Faida Fund.

“Na hii inatokana na mazingira mazuri yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo ni jambo la kupongezwa. Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi na wadhamini itasimamia mfuko huu kwa weledi na faida kubwa, na tutahimizana watu wote kununua vipande hivi ili iweze kuchochea maendeleo,” amesema CPA Kashimba.

Nae, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Charles Shirima amesema mifuko inafaida nyingi sana kwani unaponunua vipande unakuwa umewekeza katika sehemu ambayo inasimamiwa vizuri.

Faida Fund ni moja ya vyombo vya uwekezaji wa pamoja ambapo utakuwa ni mfuko wa saba wa uwekezaji kuanzishwa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles