MWANDISHI WETU – Dar es salaam
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo amesema vyuo vikuu vina wajibu wa kuwekeza katika tafiti kwa maendeleo ya jamii.
Dk. Akwilapo alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua kongamano la kimataifa la ujenzi wa maendeleo ya Afrika lililofanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) Dar es Salaam.
Alisema tafiti zina tija kubwa katika maendeleo ya jamii kwa sababu wasomi hutambua majibu sahihi ambayo hutoa dira ya kuisaidia jamii. “Vyuo vina majukumu matatu; kufundisha, kutafiti na kuhudumia jamii, kwa hiyo elimu inayotolewa na vyuo inatakiwa kurudisha huduma kwa jamii kwa kuwa na majibu sahihi ya kusaidia maendeleo ya watu,” alisema Dk. Akwilapo.
Naye Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Profesa. Shadrack Mwakalila alisema kongamano hilo limewakutanisha wanazuoni kutoka mataifa mbalimbali. Alisema kusudio la kongamano hilo ni wanazuoni kuchakata mawazo kwa kuchambua tafifi mbalimbali kwa malengo ya kujenga nchi za kiafrika.
“Kongamano hili la kimataifa ni la kwanza kufanyika hapa chuoni. Ila chuo kina utamaduni wa kufanya makongamano mara kwa mara kwa lengo la kukutanisha wasomi na wadau wa elimu na maendeleo kujadili mambo mengi yanayotokana na tafiti walizozifanya ikiwa ni pamoja na kukumbuka waasisi wa taifa letu,” alisema Profesa Mwakalila.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Utafiti wa Chuo cha Sayansi ya Jamii kwa Afrika kutoka Urusi, Dk. Dmitri M. Bondarenko, alisema chuo chao kimejikita katika tafiti za kutafuta suluhu ya changamoto zinazoikabili jamii.
“Kujenga taifa baada ya uhuru ilikuwa rahisi, lakini changamoto za sasa kutokana na utandawazi zinachochea kupoteza uzalendo hatua ambayo imesababisha changamoto kubwa kwa nchi nyingi kupiga hatua za kimaendeleo,” alisema Dk. Bondarenko.