28.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 19, 2022

Bosi Kampuni ya OBC kizimbani kwa utakatishaji fedha

JANETH MUSHI-ARUSHA

KAMPUNI ya Otterlo Business Limited (OBC) na Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya wawekezaji kutoka Falme za Kiarabu, Isaya Mollel, maarufu kama Isack Mollel,wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka 10 yakiwamo ya utakatishaji fedha na kukwepa kodi.

Mollel alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha jana baada ya kushikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), tangu Februari 21, mwaka huu.

 Kesi hiyo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Niku Mwakatobe.

Jamhuri iliwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Oswald Tibabyekomya akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Martenus Marandu.

 Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 22 ya mwaka huu, Takukuru iliwakilishwa na Mawakili Dismass Muganizi na Hellen Osujaki, huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na mawakili Method Kimomogoro, Daud Haraka na Goodluck Peter.

Akisoma mashtaka hayo, Wakili Tibabyekomya alidai katika shtaka la kwanza la kughushi linalomkabili Mollel, anadaiwa kati ya Septemba 15, mwaka juzi na Aprili 7, mwaka jana katika eneo lisilojulikana jijini Arusha, kwa nia ya kudanganya alitengeneza nyaraka ambayo ni ankara ya malipo (invoice) yenye namba 9091 ya Septemba 15, 2017.

Alidai ankara hiyo inaonesha kampuni hiyo imeagiza gari aina ya Mercedes Benz iliyokuwa na chassis namba WDB62433615367735 kutoka Kampuni ya Everest Motors (FZD) ya Dubai, yenye thamani ya Dola za Marekani 12,800 huku akijua ni uongo.

Shtaka la pili pia ni la kughushi linalomkabili Mollel, ambaye anadaiwa kati ya Septemba 15 na Aprili 2, mwaka jana ndani ya Jiji la Arusha, kwa nia ya kudanganya, alighushi nyaraka ya uongo iliyokuwa na namba 9092 ikionesha kampuni hiyo iliagiza gari aina ya Man Truck kutoka Kampuni ya FZD yenye thamani ya Dola za Marekani 12,000.

 Wakili huyo alitaja shtaka la tatu linalomkabili Mollel kuwa ni kutoa taarifa za uongo kinyume na kifungu cha 203 cha Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004.

 “Machi 7, 2018 katika ofisi za forodha Holili, Mkoa wa Kilimanjaro, akiwa mkurugenzi wa kampuni, alisababisha kutolewa kwa maelezo ya uongo TRA kuwa kampuni imeingiza magari matatu aina ya Man Truck, Mercedes Benz mbili,” alidai

Katika shtaka la nne, Mollel na kampuni hiyo wanadaiwa kukwepa kodi kinyume na kifungu cha 203(e) (iii) cha Sheria ya Usimamizi Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, 2014, kosa wanalodaiwa kulitenda kati ya Julai 2011 hadi Julai 2015 katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Tibabyekomya alidai mahakamani hapo kuwa Mollel akiwa mkurugenzi na kampuni hiyo yenye leseni ya shughuli za uwindaji wa kitalii, walikwepa kodi kwa kutoa maelezo ya uongo kwa TRA yaliyoonesha kampuni hiyo imeagiza magari 31 na kukwepa kulipa kodi Sh bilioni 2.25.

Katika kosa la tano la kukwepa kodi linalomkabili Mollel, anadaiwa kati ya Mei 25, 2013 na Februari 4, 2015 katika Jiji la Dar es Salaam, akiwa mlipa kodi mwenye TIN namba 10183307 akiwa na nia ya kukwepa kodi, alitengeneza nyaraka za uongo kwa TRA kuwa amelipia kodi magari sita.

Tibabyekomya alitaja magari hayo kuwa ni Land Cruiser Pick Up tatu, Nissan Patrol tatu na kudai kutokana na udanganyifu huo amesababisha ukwepaji wa kodi Sh milioni 299.5.

Wakili Tibabyekomya alidai shtaka la sita linalomkabili Mollel ni kukwepa kodi kinyume na kifungu cha 84 (1) (d) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015.

Alidai kati ya Julai 2016 na Februari 2017 katika Mkoa wa Dar es Salaam, akiwa na nia ya kudanganya TRA, alitengeneza nyaraka ya uongo iliyoonesha amelipia kodi magari mawili aina ya Land Cruiser Pick Up na Ford Ranger na kukwepa kodi Sh milioni 111.3.

Shtaka la saba linalomkabili Mollel ni kukwepa kodi ambapo anadaiwa Februari 18 mwaka 2017 akiwa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa nia ya kukwepa kodi alitengeneza nyaraka ya uongo TRA na kuonesha amelipia magari mawili aina ya Mercedes Benz na Nissan Patrol na kukwepa kodi Sh milioni 199.3.

Wakili huyo alidai shtaka la nane ambalo ni utakatishaji fedha, linamkabili Molleli anayedaiwa Aprili 3 mwaka jana katika ofisi za forodha Holili, Kilimanjaro kwa ajili ya kuficha umiliki wa mali – gari aina ya Man Truck lenye namba T 141 DNM, alificha umiliki wa mali hiyo kwa kusajili jina la OBC, akijua mali imetokana na kosa la utakasaji fedha haramu (kughushi).

Katika shitaka la tisa la utakatishaji fedha, Molllel anadaiwa Aprili 3 mwaka jana akiwa ofisi za forodha Holili, alificha umiliki wa garia aina ya Mercedes Benz  iliyokuwa na namba T 150 DNM, kwa kusajili mali kwa jina la OBC huku akijua mali imetokana na kosa la kughushi.

Shtaka la 10 ni la kusababisa hasara ambapo Mollel na kampuni hiyo kwa pamoja wanadaiwa kati ya Januari 2010 na Machi 2018 katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kwa nia ovu walitengeneza nyaraka ya uongo kwa TRA na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 2.8.

 Wakili Tibabyekomya alidai upepelezi wa kesi hiyo haujakamilika. Pia kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo, Mollel hakutakiwa kujibu lolote.

Hakimu Mwakatobe alimweleza mshtakiwa huyo kutokana na makasa ya utakatishaji fedha haramu kutokuwa na dhamana, hivyo atakaa mahabusu hadi kesi yake itakapokamilika.

Aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 18, mwaka huu.

MABISHANO YA KISHERIA

Awali kabla ya kusomewa mashtaka hayo, kuliibuka mabishano ya kisheria baina ya wakili Kimomogoro na Tibabyekomya.

Mabishano hayo yaliibuka baada ya wakili huyo wa utetezi kuomba mahakama iahirishe shauri hilo na kujiridhisha na mashtaka hayo kabla ya kusomwa.

Sehemu ya mahojiano haya ilikuwa kama ifuatavyo:

Wakili wa utetezi: Kabla ya mshtakiwa kusomewa, kiutaratibu ni vema mahakama ikajiridhisha kuhusu usahihi wa mashtaka kwa mujibu wa sheria na sisi tunaomba muda wa dakika 15 ili tukirudi tushauri yasomwe au hayakidhi.

Wakili wa Serikali: Mashtaka haya yanasomwa chini ya kifungu cha 29 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, kinacholetwa hapa na “proposing charge”, kwa ajili ya washtakiwa na mahakama wala utetezi hawana mamlaka ya kuhoji usahihi au vinginevyo kuhusu haya mashtaka.

 Wakili wa utetezi: Hoja ya Wakili Mkuu wa Serikali kuwa mahakama haina mamlaka ya kujiridhisha kuhusu usahihi wa mashtaka, nadhani siyo hoja sahihi, lazima ujiridhishe.

Hakimu: Naomba waendelee kusomewa. 

Wakili wa utetezi: Tunaomba kesi iahirishwe kwa dakika 15.

Wakili wa Serikali: Huu siyo utaratibu, hawawezi (mawakili utetezi) kushauri chochote kabla mashtaka hayajasomwa.

Baada ya mabishano hayo, mawakili wa utetezi walikubaliana na hoja hiyo na mashitaka hayo kusomwa ambapo walidai mahakamani hapo kasoro zilizopo kwenye hati ya mashtaka watakuja kuzizungumzia Machi 18 kesi hiyo itakapotajwa.

Awali akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kaimu Mkuu wa Takukuru mkoani hapa, Frida Wikesi, alidai kuwa walipokea taarifa za Mollel kufanya biashara kwa kukwepa kodi huku akisaidia kampuni hiyo kukwepa kodi.

 “Baada ya kupokea taarifa hiyo uchunguzi wa kina ulifanyika na kubaini zaidi ya Sh bilioni mbili kama tozo na kodi za Serikali zilizokwepwa wakati wa uendeshaji wa shughuli zake na kampuni katika kipindi cha mwaka 2010-2018,” alidai.

 Aidha Mollel anakabiliwa na kesi nyingine katika mahakama hiyo ya kuajiri wafanyakazi 10 raia wa kigeni wasiokuwa na vibali vya kufanya kazi nchini.

Kesi hiyo ilikwama kuendelea kusikilizwa mwishoni mwa wiki kutokana na mshtakiwa huyo kushikiliwa na Takukuru ambapo kwa mara ya kwanza Februari 15 mwaka huu alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka 10.

Kampuni ya OBC ipo eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani hapa ikijishughulisha na shughuli za uwindaji wa kitalii.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
175,312FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles