Na Mwandishi wetu, Bagamoyo
Wito umetolewa kwa vyombo vya habari nchini kutoa kipaombele zaidi katika kusambaza taarifa muhimu zinazohusu maendeleo ya teknolojia ya mbegu.
Imeelezwa kuwa taarifa hizo zitachangia kilimo cha kisasa na kuwezesha usalama wa chakula na uimara wa uchumi katika kukabiliana na ongezeko la idadi ya watu na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi.
Wito huo umetolewa Novemba 3,2023, Mkoa Pwani katika kongamano la wahariri wa vyombo vya mbalimbali na Mkurugenzi wa Shirika Linalojihusisha na Kuendeleza Mifumo ya Chakula Barani Afrika ( AGRA ), Vianey ambaye Rweyendela amesema vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika kuunda maoni ya umma na kupeleka sera.
“Kwa kuwapatia wataalamu wa habari ukweli tunawasaidia kutoa taarifa na elimu kwa jamiii pana hivyo kuchangia katika kufanikisha kupokelewa kwa mazoezi bora ya kilimo,” amesema Rweyendela.
Amesema AGRA nchini imechangia maendeleo mapya ya aina 44 za mbegu zilizoboreshwa za mahindi, muhogo, maharage na soya, kwa kushirikiana na taasisi za utafiti za serikali na wadau wa sekta binafsi.Takribani aina 30 za mbegu miongoni mwa hizo zimeingia sokoni kwa mafanikio.
Naye Ofisa wa Mpango wa Mbegu Nchini (AGRA), Ipyana Mwakasaka ameeleza kua AGRA imekua na mchango muhimu katika kuimarisha sekta ya mbegu kwa kutoa msaada kwenye thamani nzima ya mnyororo wa mbegu, unajumuisha kujenga uwezo wa wazalishaji wa mbegu kampuni za mbegu za ndani na wadau mbalimbali, hivyo kuchangia kwenye ukuaji katika sekta ya kilimo.
“Matumizi ya mbegu bora nchini kwa sasa ni asilimia 20 hii inaonyesha kwamba ikiwa kiwango Cha matumizi ya mbegu bora kitaongezeka nchini itakua katika nafasi nzuri ya kufikia lengo lake la kua na ghala kubwa barani Afrika,”amesema Mwakasaka.
Amesema ili kuinua wakulima wadogo katika mpito wao kutoka kilimo cha kujikimu hadi kilimo cha biashara, taarifa sahihi ni muhimu, taarifa potofu na za kubuni zinaongeza umasikini kwa wakulima wadogo.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Chini ( TEFF ) ,Deodatus Balile aliipongeza AGRA kwa kujitolea kwao kuongeza uwezo wa waandishi wa habari katima sekta ya kilimo.
“Kua na weledi wa kina kuhusu mambo magumu ya kilimo ni muhimu kwa Tanzania inavyoazimia kua mzalishaji mkuu wa chakula barani Afrika,”amesema Balile.
Naye Mtaalamu wa Uboreshaji wa Mimea na Mwasayansi wa Utafiti, Dk. Emmarold Mneney amesema ili Tanzania kulisha Afrika kunahitaji kuwekeza zaidi katika uvumbuzi wa mbegu.
“Kuelewa teknolojia ya mbegu na uhusiano wake na mabadiliko ya tabia ya nchi ni ufunguo wa uzalishaji mbegu endelevu na mustakabali wa kilimo chenye ustawi nchini,”amesema Mneney.
Naye Meneja wa Kituo cha Taifa cha Rasilimali za Mimea za Kijenetiki katika TARI – HQ, Dk. Geradina Mzena, amesisitiza umuhimu wa teknolojia ya uzalishaji wa mbegu kwa ajili ya kilimo cha mahindi.
“Mustakabali wa kilimo cha mahindi upo katika kutumia nguvu ya teknolojia ya uzalishaji wa mbegu za mseto na bora ili kuimarisha usalama wa chakula na uimara katika uso wa mabadiliko ya madhari ya kilimo,” amesema Dk. Mzena.
Naye Ofisa wa Taasisi ya Uthibisho wa Mbegu Nchini ( TOSCI ), Zera Mwankemwa amesisitiza kuwa ushirikiano na wadau TOSCI imeboresha mfumo wa uthibitisho kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa mbegu bora hasa wakulima wadogo ambao ni nguzo ya kilimo nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Biashara ya Mbegu Nchini (TASTA) ,Baldwin Shuma amesema umuhimu wa Tanzania kupunguza utegemezi wa mbegu zinazoagizwa toka nje ni kuhakikisha kunakuwa na mbegu za kujitosheleza katika uzalishaji ili kuhakikisha usalama wa chakula na uendelevu wa kilimo.