*Takukuru, PPRA wakesha kusaka ukweli wa bil 179/-
*CAG naye ajipanga kujua ‘figisufigisu’ za ndani
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SIKU chache baada ya Rais Dk. John Magufuli, kutangaza kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu pamoja na maofisa wanne, vyombo vya dola vimepiga kambi katika mamlaka hiyo, ili kutafuta ukweli wa matumizi ya Sh bilioni 179.6 .
Inaelezwa kwamba hivi sasa maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na wale wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya Umma (PPRA) wamelazimika kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma za matumizi ya fedha hizo.
Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kwamba, maofisa hao wamekuwa wakikesha ili kutafuta ukweli wa suala hilo ikiwa ni pamoja na kupitia nyaraka kadhaa.
“Hivi sasa Takukuru, PPRA na hata baadhi ya maofisa wa Ofisi ya CAG wamepiga kambi NIDA ili kutafuta ukweli kuhusu matumizi ya Shilingi bilioni 179.6 kama ni sahihi au laa, kwenye hili tunaamini haki itatendeka,” kilisema chanzo chetu.
Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA ilimtafuta Kaimu Mkurugenzi wa Takukuru, Valentino Mlowola, alikiri kwa maofisa wake kuanza kazi ya uchunguzi NIDA mara baada ya agizo la Rais Dk. John Magufuli.
“Tumeanza uchunguzi, vijana wanaendelea na majukumu waliyokabidhiwa…siwezi kukwambia tumeanza lini na tunamaliza lini….kuweni na subira,”alisema Mlowola.
Kuhusu kesi nne kubwa ambazo ziko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mlowola alisema hadi sasa kesi moja imefikishwa mahakamani na nyingine zinaendelea kuchunguzwa.
“Tulimpatia DPP kesi kubwa nne, kama unakumbuka moja inayohusu wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), tayari imefikishwa mahakamani…tunakwenda hatua kwa hatua,”alisema Mlowola.
KAULI YA CAG
Alipotafutwa Mdibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, alisema kwa sasa wanajipanga kwa ajili ya kuanza uchunguzi katika taasisi walizotakiwa kuzikagua kama ilivyoagizwa na mamlaka husika.
“Bado hatujaanza kazi ila kwa sasa tunaendelea kujipanga ingawa kwa NIDA wapo Takukuru kwa sasa wanaendelea na kazi. Sisi tunajianda kuanza kazi na tasisi nyingine tulizotakiwa kufanya ukaguzi kwa mujibu wa sheria.
“Tutafanya hivyo na tunawaomba Watanzania wasiwe na hofu tukikamilisha kazi hii tutaeleza kwa kukabidhi ripoti kwa mamlaka husika kama sheria inavyotutaka kufanya hivyo,” alisema Profesa Assad.
Katika kasi ya utumbuaji majipu uliofanywa na Rais Magufuli pamoja na baadhi ya mawaziri wake, CAG ametakiwa kufanyia uchunguzi Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mamkala ya Bandari Tanzania, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) pamoja na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ambapo wiki hii wakurugenzi wanne walisimamishwa kazi na Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Januari 26, mwaka huu Rais Magufuli, alitangaza kutengua uteuzi wa Mkurugenzi wa NIDA, Dickon Maimu pamoja na maofisa wengine wanne kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Serikali.
Maofisa hao ni Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.
Akitangaza uamuzi huo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema taarifa zilizomfikia Rais zinaonesha kuwa NIDA hadi wakati huo ilikuwa imetumia Sh. bilioni 179.6 kiasi ambacho ni kikubwa.
Alisema Rais angependa ufanyike uchunguzi na ukaguzi jinsi fedha hizo zilivyotumika, maana Rais amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kuhusiana na kasi ndogo ya utoaji wa vitambulisho vya Taifa.
“Rais pia ameelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi maalum wa hesabu za NIDA, ikiwemo ukaguzi wa thaman ya fedha ‘Value for money’ baada ya kuthibitisha idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa.
“Pia aliitaka TAKUKURU ifanye uchunguzi kujiridhisha kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au laa,” alisema.
Kwa upande wa Bandari Januari 16, mwaka huu Serikali ilitangaza kuisafisha Bandari kwa kuwaondoa watendaji wa ngazi za juu na kuwahamishia wizarani ili kuongeza ufanisi katika utendaji, sambamba na kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Akitangaza mabadiliko bandarini, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha inasimamia mapato ya serikali na taasisi zinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Aliwataja watumishi walioondolewa Bandari kuwa ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Peter Gawile, Kaimu Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Killian Challe na Kaimu Mkurugenzi wa Manunuzi, Mashaka Kishanda.
Alisema watendaji hao wamerudishwa wizarani na itafanyika tathmini ili waangaliwe watapangiwa nafasi gani kwa kuwa inawezekana katika Bandari uwezo wao na ufanisi wao ulikuwa mdogo ila inawezekana maeneo mengine wakafanya vizuri zaidi.