25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

VYOMBO VYA DOLA VINAIJUA HATARI YA DELTA YA RUFIJI?

Waziri wa Mambo ya ndani, Mwigulu Nchemba

 

Na Balinagwe Mwambungu,

MIJI midogo ya Mkuranga, Ikwiriri na Kibiti, iko Kusini mwa Jiji la Dar es Salaam na hivyo inatarajiwa kwamba kutokana na ukaribu huo, watu wake ni waelewa wa mambo mengi ya kijamii, kiuchumi na kiutawala.

Nimewahi kufanya kazi na wakazi wa Delta ya Rufiji nilipokuwa kiongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET). Mwanzoni watu wa Delta walirubuniwa na viongozi ili waukubali mradi wa ufugaji wa samaki aina ya kamba, lakini baada ya kuwaelimisha ubaya wa mabwawa ya kamba, walituelewa na kutuunga mkono kuukataa mradi ule.

Lakini niseme pia kwamba Delta ya Rufiji haifikiki kirahisi kutokana na jiografia yake. Kwa hiyo, watu wenye nia ovu wanaweza kujificha Delta ambako si rahisi kufika vyombo vya dola.

Wakati wa kampeni dhidi ya mradi wa kamba Rufiji, tulikuwa tunakwenda na kukaa huko mambo yakiwa magumu Dar es Salaam. JET tulishinda na mradi huo haukutekelezwa.

Lakini hivi karibuni kumekuwa na habari mbaya kutoka Rufiji.

Mwanzoni iliripotiwa kwamba wanafunzi wa shule ya sekondari wilayani Rufiji, walikuwa wanawabaka walimu wao wa kike na kwamba hata walimu wa kiume walikatishwa tamaa na utovu wa nidhamu, wengi wao ama waliomba uhamisho au waliacha kazi.

Mkoa wa Pwani hususan Wilaya ya Rufiji, ni miongoni mwa wilaya ambazo ziko nyuma kielimu. Mojawapo ya sababu ni wazazi kutowakazania watoto wao elimu ya kawaida na badala yake wanawapeleka madrasa.

Aidha, utamaduni wa watu wa Pwani hupenda ngoma na kuwapeleka watoto kwenye jando na unyago, hivyo huvuruga ratiba za shule. Matokeo yake, watoto hawafanyi vizuri kwenye mitihani ya mwisho.

Kwa mtoto wa kike ni mbaya zaidi maana akishachezwa ngoma, wazazi hawataki aendelee na masomo kwa kisingizio kwamba ameshakua mtu mzima; amekwishafundishwa mambo ya utuzima!

Matukio ya kutisha ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara yanaifanya Rufiji iwe wilaya ya kuogopwa. Rufiji inaandika historia isiyopendeza machoni na maskioni mwa Watanzania.

Rufiji na Mkuranga ni wilaya za kuangaliwa kwa jicho la pekee kutokana na mauaji ya askari polisi. Polisi ni walinzi wa raia na mali zao, iweje watu wanaohakikisha tunaishi kwa amani, wageuziwe kibao; wawindwe kama wahalifu?

Jambo hili ni geni sana nchini mwetu.

Mwanzoni ilidhaniwa kwamba ni genge la majambazi; kuanzia mauaji ya polisi na askari mgambo kwenye Kituo cha Mkuranga, ambapo watu hao walipora silaha. Yakafuatia mauaji ya askari polisi wanne wa Kituo cha Mbande, Mkuranga ambapo askari wanne waliuawa.

Kabla ya hapo, kulikuwa na uvamizi wa Kituo cha Polisi, Sitakishari, Ilala Dar es Salaam ambako wahalifu waliua polisi na kuteka silaha za kivita.

Katika tukio la Mbande, genge hilo hilo lilipora silaha; halikuingia Benki ya CRDB iliyopo hapo.

Baadaye Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, akasema majambazi wanne kati ya 14 waliohusika, waliuawa katika pori la Dondwe lililoko Mkuranga mpakani na Chanika, Ilala katika mapambano na polisi.

Mambo haya yanaashiria nini kwa mustakabali wa nchi yetu? Jamii ya Kibiti, Mkuranga, Ikwiriri na Rufiji ni lazima itoe mchango katika kutafuta suluhisho.

Taasisi za kidini hapa nchini, ni lazima ziingilie kati, jambo hili linaweza na tayari limeipaka matope nchi yetu. Viongozi wetu wa dini wana mchango mkubwa wa kuhakikisha waumini wanatii maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Tunapenda watu warejee katika kuaminiana, kushirikiana kwa ajili ya maendeleo yetu sote.

Si jambo jema endapo mauaji haya yakaendelea na kuilazimisha Serikali kufanya maamuzi magumu na kutoa amri ya kuzuia watu kutembea kwa uhuru. Wakazi wa maeneo hayo wataathirika, watashindwa kufanya shughuli zao za kila siku.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, alitoa kauli kali kwamba wananchi wa sehemu hizo wanafurahia mauaji ya polisi na akasema kwamba polisi halitasalia jiwe juu ya jiwe.

Baada ya mauaji ya Mbande, Kamanda Sirro alitoa kauli tofauti na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Marijan, ambaye alilihusiha tukio la Mbande na Umoja wa Kutetea Uhuru Tanzania (UKUTA) waliokuwa wametangaza maandamano nchi nzima Sepetemba mosi mwaka jana.

Kamanda Marijani alikwenda mbali zaidi na kusema kwamba viongozi wa vyama vya siasa (Chadema), walihusika kuwahamasisha wafuasi wao kuwashambulia maofisa wa Polisi.

Lakini yaliyojiri baadaye ni wazi kwamba polisi wamekubali kutumika kisiasa. Wameacha kufanya kazi yao, kutoa matamshi ya kisiasa ambayo yangeweza kuchochea vurugu nchini.

Polisi wanaunganisha uhalifu na siasa. Mbona tukio la mauaji ya waumini katika Msikiti wa Rahman, Ilemela, Mwanza hawakusema kama yalihusisha siasa?

Mauaji ya askari wa  Kituo cha Kimanzichana, Mkuranga walisema ni genge la majambazi. Lakini mtu waliyemshuku kuwa kiongozi wa genge hilo, alikamatwa kule Pemba! Kuna uhusiano gani kati ya Mkoa wa Pwani na Pemba? Inafikirisha! Hebu polisi wajiongeze kama mtandao umekuwa mpana kiasi hicho, basi si mtandao wa majambazi. Silaha wanazopora baada ya kuwaua polisi, wanazipeleka wapi?

Polisi walimkamata kijana mmoja baada ya mauaji ya Mbande eti alikuwa akishangilia. Jambo hili limejirudia katika tukio la Ikwiriri kwamba watu walionekana kushangilia!

Ndio maana nimesema awali kwamba jamii husika inalijua fika kundi hili na madhumuni yake. Utamaduni wa kushangilia watu wakiuliwa si utamaduni wa Kitanzania.

Polisi wasitafute majibu mepesi kwa jambo zito kama hili. Haingii akilini kwamba gari ya polisi inapigwa risasi, baada ya kupoteza njia, watu wenye silaha wanawaua polisi wanane kwa risasi na kupora silaha zao, halafu polisi wanasema ni kikundi cha majambazi!

Jeshi la Polisi limekuwa linatoa majibu mepesi na kuwalaumu wanasiasa wa upinzani, hili la Ikwiriri, je, nalo ni la wanasiasa?

Polisi wanatakiwa kufanya ‘home work’; wasitoe majibu rahisi rahisi. Kundi hilo hilo limehusika na vitisho kwa viongozi wa vitongoji na vijiji. Kundi linaloendeleza vitisho na kuwaua polisi, ndilo hilo hilo lililotoa orodha ya majina ya viongozi 18 (wote wa CCM), huko huko Rufiji na Mkuranga kwamba viongozi hao watauawa kwa vile walikuwa sehemu ya Serikali na kweli waliuawa na hakuna aliyekamatwa.

Polisi bado wanadai hiki ni kikundi cha majambazi; majambazi gani hawachukui kitu chochote isipokuwa silaha!

Mbona hatujasikia wamepora maduka au benki au kuvamia mabasi ya abiria kama inavyotokea sehemu nyingine.

Je, uchaguzi unaotarajiwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi ngazi za chini, utafanyika sehemu hizo za Rufiji na Mkuranga? Watu wameingiwa na hofu ya kuuliwa kwa kuwa tu ni viongozi.  Mazingira tata yanazua hofu. Jengeni mazingira rafiki ili wanachama wajitokeze kuomba uongozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles