30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

DK. BASHIRU: UWEZO MDOGO WA KUJITAWALA KIDEMOKRASIA UNAUTIA NAKISI MUUNGANO

 

 

Na EVANS MAGEGE,

WATANZANIA wameadhimisha miaka 53 ya Muungano wa Zanzibar na Tanzania Bara (Tanganyika) Jumatano ya wiki hii.

Kitaifa maadhimisho ya Muungano yalifanyika mjini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali walioongozwa na Rais Dk. John Magufuli.

Pia viongozi wastaafu, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete pamoja na wajane wa waasisi wa Muungano; Maria Nyerere na Fatma Karume nao walihudhuria maadhimisho hayo ya Muungano mjini Dodoma.

Fursa nyingine ya maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano iliandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA), wanazuoni mbalimbali walijumuika ndani ya ukumbi wa Nkrumah uliopo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo walikuwa na jukumu moja tu la kuujadili Muungano na kutoa tathmini zao juu ya miaka 53 tangu Muungano ulipozaliwa.

MTANZANIA Jumapili ilikuwa miongoni mwa wageni waalikwa waliohudhuria mdahalo huo ulioandaliwa na UDASA.

Mada katika mdahalo huo ilikuwa ni ‘Tafakuri ya miaka 53 ya Muungano –Tulikotoka, tulipo na tunakoelekea’.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Bashiru Ally, alikuwa ni mmoja wa watoa mada katika mdahalo huo ambapo alitumia dakika 39,  kuzugumzia maana ya muungano, uwezo wa kujitawala, uhalali wa siasa tawala na hatima ya muungano.

MAANA YA MUUNGANO

Dk. Bashiru Ally anaanza kwa kujenga hoja ya kifalsafa na kinadharia kuhusu maana ya muungano kwa kusema kwamba kielelezo cha muungano ni ushindi wa kihistoria dhidi ya itikadi za ukoloni wa kibeberu.

Anasema kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano mwaka 1964, kilikuwa ni kielelezo cha uasi wa Waafrika dhidi ya siasa tawala za ukoloni.

“Sote tunajua enzi ya ukoloni sera maarufu ilikuwa ni sera ya wagawe ili uwatawale na siasa hizo za kikoloni ukweli zilikuwa si halali kwa Waafrika. Ndio maana natumia neno uasi,  hivyo Waafrika wa Tanganyika na Zanzibar waliamua kuunda chombo chao ili wasionewe, wasipuuzwe, wasinyonywe na wasidhalilishwe tena. Kwa waasisi wa Muungano hicho kilikuwa ni kitendo cha kimapinduzi,” anasema Dk. Bashiru.

Anaelezea maana ya pili ya muungano kuwa ni dira ya ukombozi na mkakati wa kisiasa wa nchi huru kupanua uwezo wake wa kujitawala kidemokrasia.

Anasema baada ya kujitawala kulihitajika  dira zaidi ya kudai uhuru na mtazamo huo ulikuwa ni sehemu ya kujenga mfumo wa uzalishaji mali katika uongozi ambao unawanufaisha zaidi walio wengi kwa kuwapa matumaini ya kuboresha hali zao za maisha kulingana na historia, mahitaji na utamaduni wao.

Anasema mtazamo wa tatu wa kimajumuhi wa Afrika kuhusu maana ya muungano ni kuelezea muungano kama hazina ya kutunza historia ya mapambano ya ukombozi wa Bara la Afrika.

Anafafanua zaidi kwa kusema kuwa Muungano ni shule ya kihistoria kwa Waafrikia wote. Kwamba shule hiyo inaeneza taarifa na maarifa kuhusu chimbuko la utaifa wao, uwezo na udhaifu wa taasisi zao za kisiasa na msingi huo unawahamasisha wananchi kwa kuweka bidii za kujiendeleza.

“Kwa mtazamo huu, Muungano ni zaidi ya historia ya mapambano ya ukombozi wa Tanganyika na Zanzibar, hivyo ukichukua maana hizi tatu utabaini kwamba uamuzi wa kuungana ulikuwa ni uamuzi wa lazima kisiasa na wala haukuwa uamuzi wa hiari,” anasema Dk. Bashiru.    

UWEZO MDOGO WA KUJITAWALA KIDEMOKRASIA

Katika hatua nyingine, Dk. Bashiru anasema kwamba baada ya miaka 53 ya Muungano, uwezo wa nchi kujitawala kidemokrasia bado haujaongezeka kwa kiwango cha kuridhisha.

Anasema kwa msingi huo uwezo wa nchi kujitawala kidemokrasia bado mdogo, hivyo umesababisha nakisi ya uhalali wa Muungano.

 “Kadiri uwezo wetu wa kujitawala kidemokrasia unavyoshindwa kuongezeka  ndivyo uhalali wa Muungano unapopata nakisi. Nakisi ya Muungano ikizidi kuongezeka na kama hatua za haraka hazichukuliwi, Muungano hudhoofika na unaweza kuvunjika kwa sababu wenye Muungano ni wananchi.

“Wananchi kama hawaridhiki na namna Taifa linavyoendeshwa, namna ya matatizo yao, wasiwasi wao, hofu zao na matarajio yao yanavyopotea kiwango chao cha kuuamini muungano kinashuka na wanapopunguza kiwango chao cha imani katika muungano, muungano hudhoofika na chombo chochote kilichodhaifu hakiwezi kusimama,” anasema.

KWANINI NCHI IMESHINDWA KUJITAWALA KIDEMOKRASIA?

Dk. Bashiru anajenga hoja ya sababu zinazosababisha nchi kushindwa kukuza uwezo wa kujitawala kidemokrasia ambazo ni kukosekana kwa uwezo wa kujenga na kubuni mipango na mikakati ya maendeleo ya nchi.

“Simaanishi kwamba hatuna mipango wala sera ila ninachosema mimi mpangilio wa mikakati hii na mipango hii haikidhi mahitaji yetu kwa kiwango tunachokitaka,” anasema Dk. Bashiru.

Katika kushibisha hoja hiyo, Dk. Bashiru anatoa mifano mitatu kama ushahidi wa sababu ya sera na mipango ya nchi kuwa haijakaa sawa.

Mfano wa kwanza unaoonyesha nchi kushindwa kupanga mipango yake vizuri ni pengo la walionacho na wasionacho kuzidi kuongezeka kwa kiwango cha kutisha.

“Leo tunavyozungumza wavuja jasho wengi (namaanisha wale wajasilia jasho si wajasiriamali) na walio kwenye kundi hili ni wahunzi, wakulima wadogo, wavuvi wadogo, wakwezi, madereva wa bajaji na bodaboda, walinzi na hata watumishi wa umma katika nafasi za chini.

“Ukichunguza kwa undani katika nchi yetu inayokuwa kwa kasi ya kutisha au kiholela, utagundua mamilioni ya wakazi mijini hawapati ujira wa kumudu gharama za mahitaji yao ya kuishi kama binadamu na miji inafurika kwelikweli, kwa mfano bei ya unga wa sembe ni 2,400 leo inanitisha hata mimi ambaye si mvuja jasho wala si mjasilia jasho. Mimi ni mtumishi wa umma kati ya watumishi wa umma wanaolipwa vizuri,” anasema.

Anasema kodi za nyumba hazina udhibiti wowote, kwamba mkataba wa nyumba ukiisha mpangaji anaishi roho juu na kapangiwa alipe kwa miezi sita au mwaka au vyombo vyake vitolewe nje.

“Pia nauli za usafiri, gharama za maji na bei za umeme bado zipo juu sana na hakuna dalili yoyote kwamba gharama hizi zitashuka,” anasema.

Anaongeza kuwa mipango miji badala ya kuwa na mipango ya makazi bora imegeuka na kuwa mipango ya kuwadhulumu wenye ardhi hasa wale wanyonge.

“ Yote haya ninayoyasema yamewakatisha tamaa wananchi na usitegemee watu hawa wakawa na imani sana na mfumo unaotawala, hata kama utawaona wako kimya au hata kama utawaambia kaa kimya hili halihitaji daktari wa sikio kwa sababu linaonekana na tunaishi nalo,” alisema

SIASA ZA UTAWALA HAZIAMINIKI

Dk. Bashiru anataja mfano mwingine kuwa kwa miaka 20 ya mageuzi ya kisiasa, aina ya siasa zinazotumika kuitawala nchi haziaminiki tena hasa kwa wavuja jasho.

Anasema kwa msingi huo kwa sasa nchi ina mazingira machafu ya kisiasa kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Siasa zilizozaa muungano kwa mujibu wa historia zilikuwa ni siasa za kimapinduzi na wavuja jasho walishiriki sana katika siasa hizo kwa kuanzisha hivyo vyama vilivyoleta Muungano wa Afro- Shiraz Party na TANU. Hivyo vyama ndivyo vilivyokuwa ni vyama vya wakulima na wafanyakazi, leo hali imechafuka wakulima na wafanyakazi hawana lao katika siasa za nchi hii, wamebaki kuwa watazamaji.

“Siasa za aina hii zinalipunguzia Taifa uwezo wa kujitawala kidemokrasia. Na kutokuaminika kwa uwezo wa kujitawala ni tatizo sugu tangu enzi ya mfumo wa chama kimoja na tofauti ni kwamba wakati ule kulikuwa na viongozi wanaohitaji na wanaosikia na wenye upeo wa kifalsafa wa kujua nchi inakwenda wapi, ila kwa sasa hali imekuwa mbaya sana,” alisema Dk. Bashiru.

MATARAJIO YA SIASA ZA VYAMA VINGI YAMEYOYOMA

Dk. Bashiru anasema kwa mtazamo wake kuwa matarajio ya wananchi juu ya mfumo wa siasa za vyama vingi yameyoyoma, kwa sababu ndani ya mfumo huo sauti za wakulima na wafanyakazi kupitia katika vyombo vyao haipo.

“Vyama vya Ushirika ambavyo bado vina nguvu viko wapi? Vyama vya wafanyakazi upo utitiri wa majina kwa msajili lakini hatuvioni vikipaza sauti na hivi ndio ombwe la wavuja jasho la kutetea haki zao na kupeleka maoni yao katika msingi wa Serikali.

“Kwa sasa ombwe hilo limezibwa na wajasiriamali wa kisiasa na kiuchumi na hivi sasa msisitizo umewekwa si katika ushirikishaji wa wananchi katika kuleta maendeleo yao lakini ni katika siasa za uchaguzi,” anasema.

Anaongeza kuwa mipango ya masafa mafupi ya wanasiasa wanaopenda madaraka na wafadhili wao ndio inayotumika kuwa kipaumbele cha Taifa.

 “Unaweza ukapata matatizo kuhoji Ilani ya uchaguzi ya chama tawala kana kwamba Ilani ya uchaguzi ya miaka mitano ndio mpango wenyewe wa Taifa. Nimeangalia chaguzi nyingi tangu mwaka 2000, nikabaini kila uchaguzi unaopitia ulaghai, matumizi makubwa ya pesa na ahadi za uongo tena bila haya.

“Na awamu inayofuata hakuna mtu anayeomba radhi kwa makosa yaliyotendekea, macho makali na meupe hivi hivi wanaomba tena na tena. Na vikao vya vyama vyote vinavyotaka kuingia madarakani na kutaka kushika hatamu na vile vinavyotaka kung’angania madarakani kwa kushika hatamu mpango wao ni ushindi kwanza na baada ya hapo ni kupongezana na kugawana vyeo, wanaokosa vyeo wananung’unika na wanaopata wanafurahia lakini bila uhakika, wakitetemeshwa wanakasirika. Lakini wanashindaje? Someni ripoti za chaguzi zote na hata watu wanavyoshinda uchaguzi, si wote lakini kwa kiwango kikubwa mnajua wenyewe,” anasema Dk. Bashiru.

Anasema unapofika wakati wa uchaguzi wananchi huanza kufadhaika na baada ya hapo mshindi anatangazwa, anaapishwa na kuanza kutekeleza ilani ya uchaguzi.

Anaongeza kwa kusema siasa za namna hizo haziwezi kuaminika kwa wavuja jasho na kama haziaminiki haziwezi kuhalalisha utawala kuwa upo katika imani za watu.

ITIKADI ZA KIZAYUNI NA UBEBERU

Dk. Bashiru anasema nchi inakumbatia itikadi za uzayuni na ubeberu kwa maana ya sera na mipango inayowekwa na viongozi si ya itikadi ya nchi.

“Ziwe ni sera kwenye Kilimo, Viwanda hata Elimu kwa namna moja ua nyingine zinatokana na ushawishi wa kibeberu na hili ni kinyume itikadi iliyozaa muungano. Tukumbushane kidogo itikadi iliyozaa muungano kwa kiasi kikubwa ulikuwa ni uasi dhidi ya ubeberu lakini wote tunajua kwamba ukishakumbana na uzayuni na ubeberu, maana yake unajipunguzia uwezo wako wa kujitawala kidemokrasia.

“Unaweza ukajiongezea uhakika wa kuendelea kuwapo madarakani lakini kutawala kidemokrasia uwezo wake haupo na tunajua kihistoria ubeberu umekuwa chanzo kikuu cha machafuko na maafa ya kijamii duniani, sasa badala ya kuogopa itikadi hizi kama ukoma na badala ya kupanga kuendeleza uwasi wa kihistoria dhidi ya itikadi hizi sisi tumeamua kuziabudu kama vile ni Msahafu Mtakatifu. Mkichunguza kwa undani mtagundua itikadi za ubeberu zimezaa sera zetu za maendeleo nyingi sana na sasa hivi zimeingia kwa kasi katika sera zetu za Mambo ya Nje,” anasema Bashiru.

Dk. Bashiru anafafanua kwamba sera za Taifa za mambo ya nje zimeyumba kwa kiasi kikubwa.

“ Sitaki kutaja majina hapa…..tumeambiwa kwamba kuwa na uhusiano wa kibalozi na Israeli kunatuongezea idadi ya watalii. Kijiografia Israeli ina idadi ya watu wangapi hata kama wangekuja wote na mifugo yao. Na tunaambiwa haya tusiyazungumze, migogoro ya watu wengine haituhusu sisi lakini itikadi iliyozaa muungano wasingethubutu hata kusema hayo. Jenga hoja tu kwamba hali imebadilika, uzayuni umebadilika, ubeberu umebadilika na kwa maana hiyo hawa si maadui wetu tena, weka mezani hoja tujadili.

“Kinachonisikitisha kimya kimetawala hata kwa jambo zito kama hili lenye uhitaji wa kujadiliwa kwa kina pasipo kuwashtua watu….na tunaambiwa katika muundo wetu wa sera kuna Kamati ya Bunge inayohusika na masuala ya usalama na nchi za nje, utasikia wanachachama kuhusu Lugumi mara ripoti ya CAG , hili mbona hatuambiwi ni lini uzayuni umekuwa ni sera isiyotisha duniani,” anasema.

TUJIFUNZE HISTORIA YETU

Dk. Bashiru anapendekeza umuhimu wa kupanga kwa kujifunza historia ya nchi kwa sababu kuna tatizo la ufahamu ukiachilia mbali tatizo la kupuuza.

“Unapokuwa na ufahamu wa kihistoria, unakuwa na nafasi ya kuepuka makosa yaliyofanywa pia unakuwa na uwezo wa kupanga kwa ubunifu ili uende mbele. Ukiwasikiliza wanasiasa wetu kwa ukweli kwa kiwango kikubwa, wana tatizo la ufahamu kwa sababu kuna mambo mengi ya msingi tumeshayafanya na hatutakiwi kuwa tunakosea mara kwa mara na Mwalimu Nyerere ameshasema anashangaa kuona watu wanakumbatia makosa waliyoyafanya na anashangaa kuona watu wanapuuzia mazuri ambayo yamekwishakufanywa,” anasema.

WATANZANIA WANAOGOPA KUZUNGUMZA

Dk. Bashiru alitoa pendekezo jingine la kuwataka Watanzania kuacha tabia ya woga, wazungumze mambo kwa ajili ya mustakabali wa Taifa.

“Kuna wengine wanasingizia kuwa wamezuia kuzungumza. Nendeni mitaani kule mkajumuike, watu wanazungumza wafuateni watu wazungumze, wale wavuja jasho wanazungumza nini kuhusu hatima ya maisha yao. Kwa hiyo tufungue milango ya mazungumzo.

“Kwa mfano kama tuna sera ya viwanda je tumezungumza na wananchi? Wanauelewa wa kutosha kuhusu ni aina gani ya viwanda wanavyovitaka na  dhana ya viwanda kwao ni nini? Lazima tuzungumze na yawekwe mazingira mazuri ya kisiasa ya watu kuzungumza hasa wale wazalishaji wadogo,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles